WATU WALIOGOPA KUMSOGELEA; RAIS SAMIA AKAMSHIKA MKONO NA KUOKOA MAISHA YAKE


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akitazama maendeleo ya mkono wa Mtoto Hamimu Mustapha Baranyikwa (15) mwenye matatizo ya ngozi ambaye ni mkazi wa Nyakanazi Mkoani Kagera mara baada ya kuzungumza naye na kumpa Mkono wa Eid Ikulu Jijini Dar es Salaam. Mhe. Rais Samia aligharamia matibabu ya mtoto huyo kwa muda wa miezi sita katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam.


* Hatimaye, ndoto ya mtoto Hamimu ya kukutana na Rais yatimia

* "Ni mimi" Rais Samia alimwambia mtoto huyo baada ya kushindwa kuamini macho yake alipofika Ikulu

Mwandishi Wetu

HAYAWI, hayawi... sasa yamekuwa. Ndoto ya mtoto Hamimu Mustapha Baranyikwa (15) aliyokuwa akiililia kwa muda mrefu ya kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan hatimaye imetimia. 

Hamimu, ambaye alilazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili kwa miezi 6 akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa ngozi kwa ufadhili wa Rais Samia, aliinama chini na kijishika kichwa baada ya ombi lake la kukutana na Rais kutimia.

Mtoto huyo aliomba akutane na Rais kumshukuru kwa kuokoa maisha yake kwa kumpatia matibabu hadi kupona.

Wakati watu walikuwa wanamnyanyapaa na kumkimbia kutokana na ugonjwa wake wa ngozi, Rais Samia alimshika mkono na kukagua mikono yake kwa upendo wa ajabu.

Mwanzo hakutanabahi kuwa aliye mbele yake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, lakini baada ya kugundua, mtoto Hamimu alishikwa na hisia kali. 

Mtoto huyo alishikwa na butwaa pale ambapo Rais Samia alipojitambulisha kwake huku akiinama chini bila kuamini.

"Sura inakuja kama ya Mama Samia," alisema Hamimu baada ya kukutana uso kwa uso na Rais.

Rais Samia akamjibu mtoto huyo: "Sasa huyu ndiyo Mama Samia, si ulisema unataka kumuona?"

Huku akiinamisha kichwa chake na kujishika na mikono usoni, Hamimu huku akiwa haamini kama ndoto yake kweli imetimia akamuuliza Rais, kweli "ni wewe?"

Baada ya mtoto huyo kushikwa na butwaa, Rais Samia huku akitabasamu akamuuliza: "Hamimu, vipi sasa? Si ulisema unataka kuniona."

Ndipo Hamimu alipojibu: "Nimefurahi kukuona, Asante."

Hamimu alifika Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumshukuru Rais Samia kwa msaada wa matibabu aliompatia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Rais Samia alimuona mtoto huyo kwa mara ya kwanza wakati wa ziara yake ya kikazi Nyakanazi, mkoani Kagera, tarehe 16 Oktoba, 2022 na kuagiza apatiwe matibabu haraka baada ya familia ya mtoto huyo kuhangaika kwa muda mrefu bila msaada wowote.

Akiwa Muhimbili, Hamimu alisimulia mtihani wa maisha aliopitia akiwa na umri mdogo tu wa miaka 15.

"Nilisikia Rais Samia anapita Nyakanazi na mimi kwetu ni pale pale Nyakanazi. Wazazi walinikataza, wewe usiende na hali hiyo uliyokua nayo watu wanakukimbia. Unaenda kufanya nini, watakupiga," alisema. 

"Kaka yangu akaniambia wewe nenda, itakavyokuwa itakuwa. Ninachojua (Rais) anaweza kukusaidia. Mimi kweli niliamka usiku sana ili wazazi wasinione, maana kama wangeniona wangenikataza."

Hamimu, ambaye wazazi wake walihangaika kumpeleka kwa waganga wa kienyeji na hata kuuza mali za familia bila mafanikio, alikuwa amekata tamaa kama angekuja kupona ugonjwa wake wa ajabu 

Ngozi yake ilikuwa imeharibika, uso wake ukawa hautazamiki hadi watu wazima na watoto wakawa wanamkimbia na alishindwa hata kukunja na kukunjua vidole vya mikono yake kutokana na maradhi hayo.

Wahenga wanasema penye nia pana njia. Rais Samia alipofika Nyakanazi wakati wa ziara yake ya mkoa wa Kagera, alimuona mtoto huyo amekaa pembeni ya barabara akiwa amenyong'onyea akawatuma wasaidizi wake waende kuongea naye wajue tatizo lake ni nini.

Kufuatia ushauri wa daktari, Samia aliagiza mtoto huyo asafirishwe haraka kutoka Nyakanazi hadi hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili iliyopo Dar es Salaam kwa uchunguzi na matibabu.

Siku chache baada ya maagizo ya Rais, Hamimu akaanza kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Muhimbili tarehe 21 Oktoba, 2022 hadi tarehe 19 Aprili 2023, madaktari wake walipomruhusu kwenda nyumbani baada ya matibabu.

Mwisho
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464