WANAFUNZI TISA SHINYANGA WADAI KULAZIMISHWA KUZICHANA SARE ZA SHULE KWA VIWEMBE NA MWALIMU

Muonekano wa moja ya sare ya shule ambayo imechanwa na viwembe.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

WANAFUNZI Tisa wa shule ya Sekondari Town Manispaa ya Shinyanga kidato cha Nne, wamedai kulazimishwa kuzichana sare zao za shule kwa kupewa wembe na Mwalimu wa nidhamu wa shule hiyo Jabiri Mwita.

Tukio hilo limetokea jana majira ya asubuhi wakati wa ukaguzi wa usafi shuleni hapo.

Mmoja wa wazazi wa Mwanafunzi aliyechaniwa nguo na Mwalimu huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema amesikitika kumuona mtoto wake akirudi nyumbani majira ya asubuhi kutoka shule huku nguo zake zikiwa zimechanwa na viwembe.

“Nikiwa bado nyumbani sijakwenda kazini nilishanghaa kumuona mtoto wangu akirudi nyumbani huku nguo zake zikiwa zimechanwa na viwembe, nilipo mhoji mbona nguo zako zimechanika akasema mwalimu wa nidhamu Jabiri Mwita aliwapa wembe akawaambia wazichane huku akiwasimamia,” anasema Mzazi huyo.

“Nilipomuuliza amechaniwa peke yako akasema wamechaniwa wanafunzi 9 wote wa kidato cha Nne, sababu wameambiwa nguzo zao ni fupi ndipo akawapatia kiwembe na kuanza kuzichana kwamba wazipanua,”ameongeza mama wa mtoto huyo.

Aidha, amesema hali yake ya kiuchumi siyo nzuri na amesikitika mtoto wake huyo kuchaniwa nguo na yupo kidato cha Nne, hali ambayo italazimika mtoto wake kutokwenda shule hadi siku apate pesa ya kumshonea sare nyingine,

Naye Mkuu wa shule ya Sekondari Town Mwalimu Komanya Mathias Busasi, ametolea ufafanuzi suala hilo kwamba Mwalimu wa nidhamu Jabiri Mwita, jana alikuwa akifanya ukaguzi wa mavazi kwa wanafunzi wa kike wanaovaa Sketi fupi na wavulana kuvaa nguo za kubana (Model).

Anasema wanafunzi hao walishaonywa tangu Januari juu ya mavazi yao ya shule, na tayari wazazi wao walishaandikiwa barua za kwenda shuleni hawa kutii, ndipo Mwalimu huyo akawaambia wanafunzi hao wazipanue suluari zao chini kwa kuzitatua kutoa uzi ili wazipanue na walizichana wao wenyewe.

“Nilipigiwa simu na mzazi mmoja akinieleza kuwa mtoto wake amechaniwa suruali na Mwalimu tena zimechanwa chanwa sana, nikamueleza kuwa wanafunzi waliambiwa na Mwalimu wazipanua kwa kutoa uzi kwenye mshono ili waziongezee ukubwa,”anasema Busasi.

Aidha, amewataja wanafunzi watatu ambao bado hawajaripoti shule mara baada ya suruali zao kuzichana kwa wembe kuwa ni Daniel Masasi, Noel Modesti na Nassoro Abdul, huku wengine wakirudi shule na wanaendelea na masomo, na kueleza kuwa Mwalimu huyo hakufanya kwa lengo baya bali ni katika kufuatilia nidhamu za watoto.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464