SHIRIKA LA TCRS LAENDESHA MAFUNZO YA STADI ZA MAISHA KWA WASICHANA BALEHE,WANAWAKE VIJANA NA WENYE ULEMAVU WILAYANI KAHAMA



Washiriki wakipiga ya pamoja mara baada ya kumaliza mafunzo.

Na Frank Mshana, KAHAMA.

SHIRIKA lisilo lakiserikali linalojihusisha na utoaji wa misaada ya kibinadamu na utunzaji wa mazingita TCRS limeunga mkono juhudi za Serikali kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kwa kutoa elimu ya stadi za maisha kwa wasichana balehe, wanawake vijana na wenye ulemavu walioathirika na vitendo vya ukatili kupitia mradi ujulikanao kwa jina “CHAGUO LANGU HAKI YANGU’’ unaofadhiliwa na serikali ya Finland kwa kushirikiana na UNFPA na kutekelezwa na TCRS kwa ushirikiano na WILDAF.
Mwanamina Mavura ni msimamizi wa mradi wa Chaguo langu Haki yangu Kahama amesema katika mradi huo TCRS imefanikiwa kuwafundisha mabinti balehe 98 masuala ya stadi za maisha, ikiwemo masuala ya lishe, masuala ya uzazi wa mpango, ukatili wakijinsia pamoja na mila potofu.
‘’Malengo yakuwafundisha mabinti hao ni kuhakikisha kuwa wanapata haki ya kuchagua na kuweza kufikia malengo wanayotarajia ili kuepuka vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa vikitokea dhidi yao” Amesema Mwanamina Mavura, Msimamizi wa mradi wa “CHAGUO LANGU HAKI YANGU” Kahama.

Mwezeshaji wa mafunzo ya stadi za maisha kupitia mradi wa CHAGUO LANGU HAKI YANGU Bi. Vestina Mtakyawa amefafanua kuwa kama elimu ya stadi za maisha ikiendelea kufundishwa kwa mabinti balehe matatizo yanayowakumba mabinti wanaobeba ujauzito wakiwa chini ya umri wa kuzaa yatapungua huku akizitaja changamoto baadhi zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kushindwa kuwalea watoto baada ya kujifungua, utapiamulo kwa watoto kushindwa kuhimili magonjwa mbalimbali.
Baadhi ya wasichana balehe, wanawake vijana na wenye ulemavu waliopata mafunzo hayo wamesema awali kabla ya kupata mafunzo ya stadi za kazi kupitia mradi wa CHAGUO LANGU HAKI YANGU walipitia changamoto nyingi zana za kimaisha ikiwemo kurubuniwa na wanaume, kupata vishawishi kutokana na umasikini na ukosefu wa kipato cha uhakika hali ambayo ilikuwa ikisababisha wengine kupata magonjwa ya ngono na kushindwa kumudu maisha.
Afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Shinyanga Lidya Kwesigabo amesema baada ya mashirika mbalimbali kushirikiana na Serikali kukabiliana na masuala ya ukatili na vitendo vya ukatili wakijinsia vitendo hivyo
kwa Mkoa wa Shinyanga vimeanza kupungua kwakuwa elimu imeanza kuenea hata kwenye maeneo ya vijijini.

Aidha ametaja sababu za zinazochangia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na umasikini, ukosefu wa kipato, tamaa ya fedha, na mila zilizopitwa na wakati.
Hata hivyo Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga Bi. Lidya Kwesigabo amesema Serikali imedhamiria kushirikiana na mashirika mbalimbali likiwemo Shirika la TCRS pamoja na Vyombo vya Habari kupambana na kutokomeza vitendo vya ukatili wakijinsia mfano ukiwa ni mradi wa CHAGUO LANGU HAKI YANGU.
Washiriki wakipiga picha ya pamoja.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464