Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude ametoa pole kwa ndugu na familia ya Magreth Juma (18) ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Mpalanga iliyopo Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma kufuatia kufariki dunia kwenye ajali ya gari iliyotokea Alhamisi Mei 11, 2023 katika kijiji cha Chidilo wilayani humo.
Mhe. Mkude ametoa pole hizo alipohudhuria mazishi ya binti huyo yaliyofanyika katika kijiji cha Kalitu Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na kusema kuwa Serikali imeguswa sana na msiba huo kwa kupotelewa na nguvu kazi ya Taifa.
“Serikali imechukua hatua kwa kugharamia mazishi, kusafirisha mwili wa marehemu, chakula na jeneza,” amesema Mhe. Mkude.
Amesema Magreth ni mmoja kati ya wanafunzi wawili waliofariki kwenye ajali iliyohusisha gari aina Mitsubishi Center iliyokuwa imebeba wanafunzi 51, walimu wawili na dereva mmoja ambao walikuwa wakielekea shule ya sekondari Maganga kushiriki mashindano ya michezo ya UMISETA.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Usalama barabarani Wilaya ya Bahi, ASP Bakari Ramadhani amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari hilo uliosababisha gari kumshinda dereva, kuacha njia na kupinduka ambapo hadi sasa dereva wa gari hilo anashikiliwa na jeshi la polisi.