MAKABIDHIANO YA MRADI WA USAWA WA KIJINSIA YAFANYIKA BUGARAMA, H/SHAURI YA MSALALA - SHINYANGA

MAKABIDHIANO YA MRADI YAFANYIKA BUGARAMA, H/SHAURI YA MSALALA - SHINYANGA

Na. Shinyanga RS.

Hafla ya makabidhiano ya Mradi wa Kufikia Usawa wa Kijinsia kwa kuwawezesha Wanawake na Wasichana Balehe kwa kuwainua kiuchumi yamefanyika jana kati ya Serikali ya Mkoa wa Shinyanga na Wadau katika Kata ya Bugarama iliyopo Halmashauri ya Msalala Mkoa wa Shinyanga ambapo Mgeni rasmi Mhe. Christina Solomon Mndeme aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita.

Katika makabidhiano hayo Mhe. Mboni aliwaeleza wananchi, wadau wa masuala ya kijinsia na wanafunzi waliokuwa wamehudhuria hafla hiyo kuwa Serikali inawashukuru sana wadau wote walioshiriki katika kutekeleza ujenzi wa mradi huo wakiwamo KOICA, UNFPA, UN WOMEN na watekelezaji wa mradi huo (KIWOHEDE, TAHA, TGNP, C-SEMA) kwa kushiriki kikamilifu tangu mwanzo hadi mwisho ambapo leo mradi unakabidhiwa.

“Leo hii tunakabidhiwa majengo mawili yaliyojengwa ambayo ni HUDUMA JUMUISHI (ONE STOP CENTER) na DAWATI LA JINSIA LA POLISI ambavyo hivi vinahusika katika kuhakikisha kuwa vinatoa huduma Rafiki na zinazojitoshereza, lengo ni kuhakikisha kuwa wahanga wa vitendo vya ukatili wanapatiwa huduma zinazostahiki kwa walengwa waweze kuedelea kuishi salama bila kuhisi unyonge wala udhaifu wakati wote,” alisema Mhe. Mboni.

Kando na hayo, Mhe. Mboni alitoa angalizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala Ndg. Charles Fussi na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kahama (OCD) kuhakikisha kuwa majengo haya hayabadilishi matumizi kwa namna yoyote ile huduma zilizokusudiwa kutolewa kwenye majengo haya zinasimamiwa kwa weledi mkubwa na utoe matokeo makubwa zaidi ya haya.

Akitoa salamu kwa niaba ya Pro. Siza Tumbo ambaye niKatibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga Ndg.Tedson Ngwale alisema kwamba kukamilika kwa mradi huo ni furaha kwa Serikali na kwamba mradi huo ndiyo utakuwa wa mfano katika kufikia Usawa wa Kijinsia na kuwawezesha wanawake na mabinti kiuchumi na kwamba mradi huo utakuwa ni endelevu huku akiwaahidi wadau hao ushirikiano Zaidi katika miradi mingine.

Katika hafla hiyo, Mhe. Mboni aliweza kutembelea na kuona shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Kikundi cha Wanawake (LUMOLUMO WOMEN GROUP) kilichopo Kijiji cha Namba Moja Kata ya Segese Halmashauri ya Msalala ambacho kinaendesha shughuli za kilimo na kuweza kujipatia mafanikio makubwa ambapo mpaka sasa wanayo Akiba ya Milioni 5 Benki huku wakiomba Milioni 22 waweze kufungua duka kubwa ombi ambalo lilipokelewa na Mhe. Mboni na kuahidi kulishughulikia kupitia kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye alisema watapewa kupitia mkopo wa asilimia 10.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464