Na. Shinyanga MC.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Mussa Samizi ameitaka Manispaa ya Shinyanga kumalizia ujenzi wa Zahanati ya Kata Kolandoto ili kuwaondolea adha wananchi wa Kata hiyo ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya matibabu.
Mhe. Johari ameyasema hayo jana kwenye mkutano wa na wananchi wa Kata ya Kolandoto wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Shinyanga baada ya kusomewa taarifa utekelezaji na wananchi kutoa ombi hilo kwake kwamba ujenzi wa Zahanati hiyo umechukua muda mrefu sana kuanzia mwaka 2010.
"Nimepokea taarifa yenu ya utekelezaji wa miradi, lakini kwenye hili ombi ambalo limetolewa na wananchi hawa wa Kata ya Kolandoto naomba lichukuliwe kwa uzito na umuhimu wa aina yake, uzuri ni kwamba Mkurugenzi wa Manispaa upo hapa na Mstahiki Meya wa Manispaa upo hapa pia, niwaombe mkapitishe bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ya umaliziaji wa Zahanati hii ambayo ni muhimu kwa wananchi wetu ukizingatia kuwa imekuwa ya muda mrefu sana ili kero hii ya wananchi ifikie mwisho sasa mwaka huu," amesema Mhe. Johari.
Katika mkutano huo wa hadhara wananchi walieleza kero zao na kutoa maombi yao ikiwa ni pamoja na kuomba kufanyika kwa ukarabati wa shule ya msingi Kolandoto ambayo ilijengwa tangu mwaka 1962 kwa sasa ina majengo yaliyochoka, kupelekwa kwa Mtendaji katika Kijiji cha Galamba, kupatiwa ufumbuzi wa malalamiko ya waliofanyiwa uthamini kupisha uendelezaji wa mradi wa Uwanja wa Ndege walipwe stahiki zao, kupelekewa huduma ya umeme kwa kijiji cha Galamba, na maji kwa baadhi ya vijiji vya Mwabahabi na Msumbiji.
Hoja hizo zilipatiwa majibu na viongozi mbalimbali walioambatana na Mhe. Johari, ambapo suala la ukosefu wa Mtendaji wa kijiji, Mkurugenzi wa Manispaa aliahidi kumpeleka, huku akiwasihi wananchi kuacha tabia ya kukataa watumishi, kuhusu maji Mhe. Mussa Elias Diwani Kata ya Kolandoto alisema Kolandoto ipo kwenye mpango wa kupelekewa huduma hiyo, na suala la fidia Mhe. Johari amesema hakuna mwananchi atakayedhurumiwa haki yake.
Hii ni siku ya kwanza ya ziara ya siku mbili katika Manispaa ambapo amekagua mradi wa ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa na ofisi 1 shule ya msingi Kolandoto, ujenzi wa vyumba 6 vya madarasa na ofisi 3 katika shule ya msingi Bugweto na ujenzi wa zahanati mpya Kata ya Ibadakuli ambayo ipo hatua za umaliziaji.
Ziara hii inayotekelezwa na Mhe. Johari ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake wa kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kufanya mikutano ya hadhara kwa lengo la kupokea changamoto zinazowakabili wananchi na kuzipatia ufumbuzi.