Arusha. Tarehe 18 Mei 2022 - Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Mpango ameipongeza Benki ya CRDB pamoja na taasisi yake ya CRDB Bank Foundation kwa ubunifu iliokuja nao kupitia programu ya IMBEJU ambapo amesema ni wenye manufaa makubwa kwa Taifa.
Dkt. Mpango amesema hayo wakati wa uzinduzi wa semina maalum ya elimu ya fedha na uwekezaji kwa wanahisa wa Benki ya CRDB pamoja na umma iliyobeba kaulimbiu ya “Ushirika wa Benki ya CRDB na Serikali kuwezesha Vijana na Wanawake” iliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).
Katika semina hiyo iliyoambatana na maonyesho ya biashara changa za vijana, Dkt. Mpango ameshuhudia bunifu za baadhi ya vijana zinazoendelezwa kupitia programu ya IMBEJU. Dkt. Mpango amepongeza akisema semina hiyo pia ni fursa kwa vijana kuonekana na wawekezaji.
“Nimefurahi kuona mmewaalika vijana wenye biashara changa pamoja na wanawake katika semina hii. Kwa kufanya hivi mmewapa fursa ya kuonekana na wawekezaji watarajiwa kwani naamini wapo wanahisa ambao wanaweza kuwekeza katika hizi biashara zao kama ambavyo wamewekeza katika Benki ya CRDB,” amesema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango pia amepongeza jitihada za Benki ya CRDB kushirikiana na Serikali kuyawezesha makundi ya kiuchumi bara na visiwani kupitia programu hiyo ya IMBEJU na kwamba sio mara ya kwanza kwani benki hiyo inashirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoa mikopo isiyo na riba kupitia programu ya INUKA na Uchumi wa Bluu.
Aidha, Dkt. Mpango aliipongeza Benki ya CRDB kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha miaka mitano iliyopita yaliyoshuhudia benki hiyo ikiendelea kutengeneza faida inayoiwezesha kutoa gawio kwa wanahisa wake.
“Nimefurahisha kusikia mwaka huu Bodi ya Wakurugenzi imekuja na pendekezo la ongezeko la asilimia 25 la gawio kwa kila hisa. Wanahisa wa Benki ya CRDB mnastahili kutembea kifua mbele kwa ongezeko hili,” ameongezea Dkt. Mpango huku akibainisha kuwa Serikali nao itanufaika na ongezeko hilo kwani ina hisa ndani ya Benki ya CRDB.
Dkt. Mpango ametumi anafasi hiyo kuziomba taasisi za fedha na bennki za biashara nchini kupunguza riba ya mikopo kama ilivyofanywa kwenye kilimo ambako baadhi zinatoa mikopo hiyo kwa asilimia 9.
“Naamini riba hiyo inaweza kushuka zaidi ya hapo. Punguzeni riba pia kwenye sekta nyingine mfano wachimbaji wadogo wa madini, wafugaji na wakulima. Riba kubwa ni kati ya sababu zilizolifanya Jiji la Dar es Salaam kushika nafasi ya 500 kati ya majiji 1,000 duniani katika kukuza biashara ndogo tofauti na majirani zetu Kenya ambao jiji lao la Nairobi lilikuwa miongoni mwa majiji 160 bora katika ripoti hiyo yam waka 2022,” aemesema Dkt. Mpango.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alimweleza Makamu wa Rais kuwa dhamira ya benki hiyo ni kuifanya programu ya IMBEJU kuwa endelevu ndio maana wanashirikiana na wadau mbalimbali ili kuwafikia vijana na wanawake wengi zaidi.
“Tunaamini mafanikio ya programu hii yapo katika ushirikiano, ndio maana tangu mwanzoni tulianza kwa kushirikiana na wenzetu wa COSTECH (Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia) na ICTC (Tume ya TEHAMA) na hivi karibuni tumesaini mkataba na Shirika la Care International,” amesema Nsekela akiainisha kuwa mpaka sasa vijana 709 na wanawake zaidi ya 4,000 wameshanufaika na programu hiyo.
Nsekela amebainisha kuwa lengo la kuijumuisha programu ya IMBEJU katika semina ya wanahisa wa benki hiyo ni kuwaonyesha kwa vitendo mwelekeo wa mkakati mpya wa Benki ya CRDB wa miaka mitano kuanzia mwaka 2023 – 2027 ambao umejikita katika kuleta mageuzi thabiti katika biashara ya benki hiyo kupitia huduma, bidhaa na programu bunifu katika soko.
Mwaka huu, Benki ya CRDB imepata leseni ya kutoa huduma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na leseni ya kampuni tanzu ya CRDB Insurance. Nsekela amesema kwa hatua hiyo, Benki sasa inatoa huduma katika nchi tatu ambazoni Tanzania, DRC na Burundi ambako ilifungua tawi miaka 10 iliyopita.
“Tunayo CRDB Bank Foundation ambayo imejikita kuwahudumia vijana na wanawake. Kwa hatua zote za kimkakati tunazozichukua, tunaamini miaka michache ijayo, ufanisi wetu utaongezeka hivyo kuongeza thamani ya uwekezaji wa wanahisa wetu,” amesema Nsekela.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay amesema ikiwa benki ya kizalendo inayomilikiwa na Watanzania kwa zaidi ya asilimia 80, wanajivunia kuendelea kuwekeza katika ubunifu uliochangia kukua kwa thamani ya uwekezaji wa wanahisa wake ikiwamo Serikali.
Katika semina hiyo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwamo faida za kuwekeza katika hisa. Dkt. Laay aliwataka Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji katika hisa husasan za Benki ya CRDB ili nao wanufaika na gawio nono ambalo limekuwa likitolewa na benki hiyo kila mwaka.
Dkt Laay pia alitumia fursa hiyo kuwaalika wanahisa wa Benki ya CRDB kuhudhuria Mkutano Mkuu utakaofanyika kesho katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) na kupitia mtandao. “Mkutano utaanza saa 3 asubuhi, watu wa mtandaoni wataweza kujiunga kupitia link https://escrowagm.com/crdb/login.aspx au kupitia SimBanking App,” amesema Dkt. Laay.
Benki ya CRDB imeweka mwongozo wa jinsi ya kushiriki mkutano mkuu kwa njia ya mtandao kupitia tovuti yake ya www.crdbbank.co.tz, mitandao ya kijamii ya Instagram na Twitter, na maelekezo yametumwa kwa ujumbe mfupi kwa wanahisa wote.
Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Kyaro Assistive Tech, Colman Ndetembea inayozalisha vifaa vya usaidizi kwa ajili kusaidia watu wenye ulemavu, wakati alipowasili katika ufunguzi wa Semina ya Wanahisa ya Benki ya CRDB ambayo mwaka huu imebeba ujumbe wa uwezeshaji wa vijana na wanawake kupitia program ya IMBEJU. Wengine pichani ni kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, Mweneykiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza wakati wa kumkaribisha Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango wakati alipowasili katika ufunguzi wa Semina ya Wanahisa ya Benki ya CRDB ambayo mwaka huu imebeba ujumbe wa uwezeshaji wa vijana na wanawake kupitia program ya IMBEJU, uliofayika leo kwenye Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Tully Esther Mwamapa akizungumza wakati wa kumkaribisha Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango wakati alipowasili katika ufunguzi wa Semina ya Wanahisa ya Benki ya CRDB ambayo mwaka huu imebeba ujumbe wa uwezeshaji wa vijana na wanawake kupitia program ya IMBEJU, uliofayika leo kwenye Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464