HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA YAPELEKA MGANGA ZAHANATI YA BUGOGO




Na Mwandishi wetu.

Shinyanga

ZAHANATI ya Kijiji Cha Bugogo kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga   iliyodaiwa  kufungwa baada ya  Mganga aliyekuwepo kufariki Sasa imefunguliwa na kuletwa mwingine ambaye ameanza kutoa huduma.

Zahanati hiyo ilikuwa na watumishi wawili  ambapo muuguzi pekee ndiye  aliyebaki na kuelemewa na  utoaji wa huduma zote  ikiwemo uzalishaji wa wajawazito na  huduma za kliniki  kwa watoto takribani zaidi ya miezi sita.

Wakiongea na  Shinyanga Press Club blog leo Mei 16,2023 baadhi  ya wananchi wa Kijiji hicho  akiwemo Diana Tungu alisema  Zahanati hiyo  imefunguliwa na kuanza kutoa huduma na mganga ameanza kufanya kazi.

"Tulikuwa tunakwenda  kituo cha  afya Samuye  umbali wa kilomita 15 kupata huduma hata Kijiji jirani cha Mwamala ni mbali tumeteseka hasa wajawazito na watoto"alisema Tungu.

Muuguzi Lenny Kinkoro alisema  alipata changamoto kubwa  kuwa peke yake kwenye  utoaji wa huduma kwa Wagonjwa takribani  Wagonjwa 20 kwa siku na wajawazito wanaojifungua takribani 12 kwa siku na huduma za kliniki kwa watoto.

"Kupatikana mganga imekuwa nafuu kwani wakati mwingine Wagonjwa wengine ninawaacha  kwenda kutoa  huduma za   mkoba   Kijiji Cha Bunonga ambacho hakina Zahanati kabisa" alisema  Kinkoro.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Bugogo  Seleli Mabula alisema  Mganga wameanza kumuona jana akifanya kazi Sasa wamefika watumishi wawili hawatoshi aliomba Serikali iongeze wengine angalau wawe watumishi wanne.
 
Diwani wa kata hiyo Hamis Masanja  alisema kata hiyo ina vijiji vinne  ambavyo ni Bugogo,Bunonga,Mwamala na Ibanza  ikiwa Kuna jumla ya wakazi zaidi ya 12,000.

"Kijiji Cha Bunonga kina wakazi zaidi ya 4000 hakina Zahanati na Kijiji Cha Bugogo kina watu zaidi ya 3000 na wote wanategemea huduma kutoka kwenye Zahanati hii"alisema Masanja..
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464