
Na Suzy Luhende, Shinyanga Press blog
Kamati ya utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Shinyanga mjini leo imehitimisha ziara yake kwa kuwataka wanafunzi wote wa shule ya sekondari Mwamalili kuacha utoro, badala yake wahudhurie vipindi vyote vya masomo na wasome kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao za baadae.
Agizo hilo limetolewa leo Mei 25,2023 na katibu wa Jumuiya ya wazazi Wilaya ya Shinyanga mjini Doris Kibabi kwenye ziara ya kamati ya utekelezaji wa Jumuiya hiyo ya kukagua uhai wa Chama na Jumuiya zake katika kata ya Mwamalili wilayani Shinyanga mkoani hapa.
Kibabi ametoa agizo hilo baada ya mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Mwamalili Colleta Mgatta kutoa taarifa kwamba, zaidi ya wanafunzi 40 hawakuhudhulia shuleni kwa wakati, hali ambayo ilisababisha sungu sungu wawafuatilie na kuwarudisha shuleni kwa nguvu, ambapo pia bado wanasuasua kufika shuleni.
"Ndugu zangu idadi hii ya zaidi ya wanafunzi 40 ni kubwa mno tunaomba wazazi muwalete watoto hao waendelee na masomo kwani elimu ndiyo ufunguo wa maisha yao, na mtoto akisoma baadae atakusaidia wewe mzazi,lakini mkikaa nae kwamba aolewe ataolewa na umri mdogo atakapopata ujauzito na kutaka kujifungua anaweza kupata ugonjwa wa visitura ama kuhatarisha maisha yake kutokana na kujifungua akiwa na umri mdogo hivyo tuwe na hruma na watoto wetu,"amesema Kibabi.
"Niwasisitize wanangu mkawahamasishe wanafunzi wenzenu ambao wanaendekeza utoro waache mara moja waje wahudhulie vipindi vyote, kwani kuolewa na kuowa kupo tu mtaolewa na kuowa msiwe na haraka ila malizeni kusoma kwanza, na kama kuna watoto wanafunzi wameolewa ama wanachunga mifugo tunaomba mtupe taarifa tuwafuatilie mara moja warudi shuleni,"ameongeza Kibabi.
Aidha Kibabi aliwataka wanafunzi kuacha kuiga mambo mabaya yasiyokuwa na maadili ya kitanzania ushoga, usagaji na uvutaji bangi, wasikubali kushawishika kwa chochote badala yake wawe na hofu ya Mungu, kwani vitendo hivyo havimpendezi Mungu.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Mwamalili James Furushi ameishukuru serikali kwa kuleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo mbalimbali ukiwemo ujenzi wa daraja ambalo limetumia zaidi ya shilingi milioni 400 na milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa choo cha shule ya msingi Ujamaa kata ya Mwamalili.
"Katibu kawaeleza kuhusu janga la ushoga na usagaji,na vitendo vingine visivyo vya maadili, hivyo Mungu hapendezwi na vitendo hivyo, mtu yeyote akiwaambia jambo hilo kataeni kujigeuza kuwa mwanamke, pia watoto wa kike, msikubali kushawishika msije mkabebeshwa mimba za utotoni mkashindwa kutimiza ndoto zenu,amesema Fulushi.
Kamati hiyo leo ilikuwa inahitimisha ziara zake,ambapo imetembelea kata 17 zote za manispaa ya Shinyanga na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, kukagua uhai wa chama, kuhamasisha wanachama wapya kujisajili kwenye mfumo,kubuni miradi mbalimbali na kuwataka wanachama na Jumuiya zake kuwa na Umoja mshikamano na upendo, na kusikiliza kero zilizokuwepo na kuzitatua.


Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Shinyanga mjini Doris Kibabi akitoa maelekezo kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Mwamalili

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Shinyanga mjini Doris Kibabi akiwa na kamati yake ya utekelezaji daraja liliojengwa kwa sh zaidi ya 400 milioni


Diwani wa kata ya Mwamalili James Furushi akizungumza ambapo ameishukuru serikali kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo




Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Shinyanga mjini Doris Kibabi akitoa maelekezo kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Mwamalili


James Nkuli mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi kata ya Mwamalili akizungumza




Viongozi mbalimbali wa kata ya Mwamalili wakimsikiliza katibu wa Jumuiya ya Wazazi Doris Kibabi






Wanafunzi wa Shule ya sekondari Mwamalili wakimsikiliza katibu wa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Shinyanga mjini Dorisi Kibabi




Katibu Kibabi akisisitiza jambo kwa diwani wa kata ya Mwamalili



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464