MADAWATI YA SHS MILIONI TISA,YADAIWA KUWA CHINI YA KIWANGO-HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA


Diwani wa kata ya Salawe,Joseph Bulugu akiwasilisha hoja yake juu ya kiwango cha madawati.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakisikiliza hoja za madiwani katika baraza.

Na mwandishi wetu.

MADAWATI 120 yaliyochongwa mwaka  2022  kwa gharama ya sh  9,000,000 kwenye shule ya sekondari Manghu iliyopo  kata ya Salawe halmashauri ya  wilaya ya Shinyanga   yamedaiwa  kutengenzezwa chini ya kiwango.

Diwani wa kata hiyo  Joseph Buyugu aliyasema hayo jana kwenye kikao Cha kawaida cha baraza la madiwani  cha robo tatu ya mwaka 2022/23 ambapo alidai shule hiyo imepokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu.

Diwani Buyugu alieleza kwenye kikao cha baraza kwamba  madawati hayo yamekosa ubora  mbao zilizotumika hazina kiwango  na madawati hayo wanafunzi wakikaa lazima  sare za shule zichanike.

"Nimelalamika nikaiomba  ofisi ya mkurugenzi  kuyakarabati madawati hayo upya  kwani  hata vyuma vyake vya miguu vilivyowekwa vinaweza kutoboa  vigae siyo imara nakujikuta serikali inaingia hasara"alisema  Buyugu.

Diwani Buyugu alisema taarifa ya kamati ya  fedha haoni  kuelezea  kuhusu bajeti ya marekebisho ya madawati hayo jambo ambalo alihoji kuwa ni kilio cha muda mrefu na hakuna utekelezaji.

Ofisa Elimu Sekondari Sterwat  Makali  alisema  madawati hayo  waliyarekebisha  na waliunda kamati kwaajili ya kuchunguza madawati  kuangalia ubora wake.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Ngassa Mboje  alisema madawati hayo yakaangaliwe tena kwani mhusika kwenye kata anadai bado tatizo liko vilevile hakuna kilichorekebishwa.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Johari Samizi alisema  atakwenda kutembelea shule hiyo ili kuweza kuona tatizo la madawati liko wapi Kama kuna shida hatua itachukuliwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464