MADAWATI 120 yaliyochongwa mwaka 2022 kwa gharama ya sh 9,000,000 kwenye shule ya sekondari Manghu iliyopo kata ya Salawe halmashauri ya wilaya ya Shinyanga yamedaiwa kutengenzezwa chini ya kiwango.
Diwani wa kata hiyo Joseph Buyugu aliyasema hayo Jana kwenye kikao Cha kawaida cha baraza la madiwani cha robo tatu ya mwaka 2022/23 ambapo alidai shule hiyo imepokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu.
Diwani Buyugu alieleza kwenye kikao cha baraza kwamba madawati hayo yamekosa ubora mbao zilizotumika hazina kiwango na madawati hayo wanafunzi wakikaa lazima sare za shule zichanike.
"Nimelalamika nikaiomba ofisi ya mkurugenzi kuyakarabati madawati hayo upya kwani hata vyuma vyake vya miguu vilivyowekwa vinaweza kutoboa vigae siyo imara nakujikuta serikali inaingia hasara"alisema Buyugu.
Diwani Buyugu alisema taarifa ya kamati ya fedha haoni kuelezea kuhusu bajeti ya marekebisho ya madawati hayo jambo ambalo alihoji kuwa ni kilio cha muda mrefu na hakuna utekelezaji.
Ofisa Elimu Sekondari Sterwat Makali alisema madawati hayo waliyarekebisha na waliunda kamati kwaajili ya kuchunguza madawati kuangalia ubora wake.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Ngassa Mboje alisema madawati hayo yakaangaliwe tena kwani mhusika kwenye kata anadai bado tatizo liko vilevile hakuna kilichorekebishwa.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Johari Samizi alisema atakwenda kutembelea shule hiyo ili kuweza kuona tatizo la madawati liko wapi Kama kuna shida hatua itachukuliwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464