MTUME DKT. NYAGA ATUNUKIWA UBALOZI WA KUDUMU WA AMANI DUNIANI, ASEMA JAMBO


NA MWANDISHI WETU, Nairobi

MTUME na Nabii Dkt.Peter Njue Nyaga wa Urejesho TV Africa na Kanisa la RGC Miracle Center lililopo Tabata Chang'ombe jijini Dar es Salaam ametunukiwa Ubalozi wa Kudumu wa Amani Duniani kutokana na kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya katika mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki na Afrika.


Ubalozi huo ametunukiwa na International College of Peace Studies U.S.A siku ya Mkesha Mkubwa wa kuliombea Taifa la Kenya amani uliofanyika Mei 5, 2023 katika Ukumbi wa Nairobi Cinema uliopo jijini Nairobi nchini Kenya.


Ni mkesha ambao ulienda sambamba na sherehe za mwaka mmoja wa Urejesho TV Africa ambayo kwa kipindi hicho imepiga hatua kubwa ya kusambaa kote barani Afrika na duniani kwa ujumla kueneza habari njema za neno la Mungu.


Kazi kubwa ya Balozi wa Amani Duniani ni kusuluhisha migogoro yote ambayo inasababisha kusiwe na amani, maana yake kusuluhisha migogoro baina ya taifa na taifa, kukutanisha marais na viongozi wa vyama mbalimbali ambao wametofautiana.


Pia, kusuluhisha migogoro ya madhehebu ya kidini kwa maana ya watumishi wa Mungu. Kusuluhisha pia migogoro ya mashamba au kama nchi ina vita.

Dkt.Nyaga ambaye mbali na kuwa mtumishi wa Mungu aliyekirimiwa kipawa cha kipekee katika kuhubiri na kueneza neno la Mungu huku maelfu wakipokea uponyaji, pia ni mbobezi katika masuala ya diplomasia na utatuzi wa migogoro baada ya kutunukiwa ubalozi huo amesema,kwa uweza wa Mungu anaamini atatimiza majukumu hayo kwa uaminifu na ukamilifu wa hali ya juu. 


"Hivyo nitafanya kazi ya kusuluhisha na kupatanisha watu mbao hawana maelewano katika jamii iwe ni Serikali, iwe ni makanisa iwe ni dini, iwe ni watu binafsi iwe ni mashamba, kazi ya Balozi wa Amani ni kupeleka amani mahali hakuna amani na pia kupeleka injili ya Bwana Yesu Kristo ya amani duniani kote. 


"Kwa hiyo mimi Mtume Dkt.Nyaga sasa ni Balozi wa Amani Duniani kote, kwa hiyo endapo kuna mahali ambapo kuna mgogoro baina ya Taifa kwa Taifa au ya vyama au ya makanisa, au ya mashamba mimi nimesomea kusuluhisha jamii ya aina hiyo,"amesema Balozi na Mtume Dkt.Nyaga.


Aidha, jambo hilo lilipokelea kwa shangwe kubwa na maelfu ya watu kutokea Kenya, Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika yote kutokana na weledi mkubwa alionao Dkt.Nyaga wa kuleta urejesho na upatanisho katika jamii hata kabla ya kuwa Balozi. 


Wamesema, baada ya kutambuliwa na Serikali na Jumuiya za Kimataifa kuwa ni Balozi wa Amani Duniani, itampa mawanda mapana Dkt.Nyaga kuifikia jamii kubwa ili kuendelea kuifanya Dunia na jamii kuwa mahali salama pasipokuwa na migogoro kwa ustawi bora wa vizazi vya sasa na vijavyo.

Miongoni mwa waliompongeza Balozi na Mtume Dkt.Nyaga ni Msemaji Mkuu wa Mitume na Manabii Tanzania,Askofu Dkt.Peter Rashid Sharifu Abubakar ambaye amesema, hiyo ni heshima kubwa kwa mwana Afrika Mashariki kutunukiwa Ubalozi wa Kudumu wa Amani Duniani.


"Shalom Shalom?...mitume,manabii,wainjilisti, wachungaji na walimu. Maaskofu na maaskofu wakuu duniani kipekee kabisa ninachukua fursa hii kumpongeza sana Mtume Dkt.Peter Njue Nyaga kwa siku ya Mei 5, 2023 kutunukiwa Ubalozi wa Amani Duniani kote, katika sherehe iliyofanyika Ukumbi wa Nairobi Cinema kuanzia saa 12:00 jioni. 


"Mtume wa Urejesho, Dkt.Peter Njue Nyaga sasa amekuwa Balozi wa Amani atakayekuwa anasuluhisha migogoro yote ya kidini na migogoro yote ya Serkali katika nchi zote duniani. 


"Kwa sababu hiyo kwa niaba ya watumishi wote ndani ya huduma tano maaskofu na maaskofu wakuu tunazosababu za msingi kabisa kumshukuru Mungu kwa kuona mtumishi mwenzetu katika Kristo Yesu amepewa nafasi hiyo, tuzidi kumuombea na kumtukuza Mungu wetu Jehovah Shammah.


"Ni imani yangu kuwa, kupitia heshima hii kuu kwa Mtume Dkt.Peter Njue Nyaga, Dunia imetetemaa...sherehe kila Taifa na pongezi kila Taifa. Mbingu zimesikika zikishangilia, Makerubi na Maserafi yakiimba kwa shangwe kuu mno.


"Huyu ni Missionary wa kwanza katika Taifa letu hili la Tanzania kutoka nchini Kenya kutunukiwa Ubalozi wa Amani Duniani (Ambassador), Mheshimiwa Dkt.Peter Njue Nyaga, anachoweza kufanya Mungu, hakuna mwanadamu anaweza kufanya,"amefafanua Msemaji wa Mitume na Manabii.


Msemaji Mkuu wa Mitume na Manabii Tanzania,Askofu Dkt.Peter Rashid Sharifu Abubakar amefafanua kuwa, "Kwa hiyo tuzidi kumuombea na kumtukuza Mungu kwa kazi njema. 


"Naomba niongee na wewe sasa, Mheshimiwa Balozi na Mtume Dkt.Peter Njue Nyaga, Mtume wa Urejesho, Mungu amekuchagua na kwa kuwa Mungu amekuchagua si mwanadamu kwa kuwa Mungu amekuchagua, na kwa kuwa Mungu amekuchagua katika nafasi hiyo, mimi binafsi sina shaka na wewe, sina hofu na wewe, sina tashwishi na wewe.


"Nafasi hiyo Mungu amekuweka ni halali yako na ni haki yako, Mheshimiwa Balozi na Mtume Dkt.Peter Njue Nyaga, Mungu akubariki sana,"amefafanua Dkt. Abubakar huku akiwapongeza watu wote ambao walishiriki katika sherehe hizo kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa ajili ya kuungana na shujaa wa injili Balozi na Mtume Dkt.Nyaga.


Wakati huo huo, Balozi Dkt.Nyaga amesema atasimama imara kuiunganisha Dunia kama ilivyoelezwa katika neno la Mungu kupitia Biblia Takatifu katika kitabu cha Yohana 14:27, "Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga."


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464