MTOTO WA MIAKA 10 AJERUHIWA NA FISI WAKATI AKIFUATA MAJI MTONI

Diwani wa Kiloleli Edward Manyama akimjulia hali mtoto aliyeshambuliwa ña fisi

Suzy Luhende,Shinyanga Press Blog

Mtoto wa miaka 10 anayejulikana kwa jina la Joyce Sengerema mkazi wa kijiji cha Kiloleli Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga amejeruhiwa na fisi katika maeneo ya kichwani,  shingoni na ubavuni wakati akienda kuchota maji kwenye mto Manonga wilayani humo.

Akizungumzia tukio hilo baba mzazi wa mtoto huyo, Kishiwa Maganga amesema mtoto  huyo alijeruhiwa na fisi Mei 27, 2023 majira ya saa 12 alfajiri baada ya kufuata maji mtoni wakati akiwa na dada yake ambapo yeye alisikia kelele na  kupigiwa simu nakuelezwa tukio la mtoto kujeruhiwa na fisi huyo.

"Mimi nilikuwa nimeenda shambani nilipigiwa simu kwamba mtoto wangu ameshambuliwa na fisi wakati akiendea maji lakini kwa bahati nzuri baba mmoja aliyekuwa analima dengu karibu na mto huo aitwaye Kashinje alimkimbiza fisi na kumuokoa mtoto huyo,"amesema baba wa mtoto huyo Maganga.

Maganga amesema mara kwa mara huwa wanafuata maji mtoni majira ya asubuhi, lakini alishangaa kuambiwa mtoto wake ameshambuliwa na fisi.

Shangazi wa mtoto huyo Kang'wa Maganga  ambaye alikuwa kwenye wodi ya watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa amesema tayari mtoto huyo anaendelea kupatiwa matibabu na wauguzi, hivyo anamshukuru daktari na wauguzi, kwani baada ya kufika tu walianza kumhudumia mtoto.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Kiloleli Edward Manyama amesema taarifa ya kushambuliwa  kwa fisi mtoto huyo,  ilimfikia  wakati akifuata maji mto Manonga akiwa na mwenzake ambaye alikimbia  na fisi huyo alimng'ata  baada ya kubaki nyuma  alianza kutembea naye vichakani, watu waliona nakuanza kumfukuza kisha kumuacha kichakani.

Manyama amesema mtoto huyo ameanza kupata huduma za matibabu  hali yake bado haijawa nzuri amewaomba maafisa wanyapori Kishapu kuendelea kuwasaka fisi hao kama ilivyokuwa miaka ya nyuma walivyoshambulia  watoto na mifugo katika kata ya Lagana beledi na kiloleli.

Muuguzi wa zamu kutoka Hospitali ya Rufaa Jesse Samweli alikiri kumpokea mtoto huyo na tayari wameanza kumpatia matibabu 

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi baada ya kutafutwa kwa njia ya Simu kulizungumzia tukio hilo hakuweza kupatikana Ila ndugu waliliripoti kituo cha polisi wilayani Kishapu 


Diwani wa kata ya Kiloleli halmashauri ya Kishapu Edward Manyama akieleza jinsi mtoto huyo alivyoshambuliwa na fisi

Shangazi wa mtoto aliyeshambuliwa na fisi  Kang'wa Maganga akielezea jinsi mtoto huyo alivyoshambuliwa na fisi

Diwani wa Kiloleli Edward Manyama akimjulia hali mtoto aliyeshambuliwa ña fisi
Mtoto Joyce Sengelema akiwa amelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga akiendelea kupatiwa matibabu


Muuguzi wa zamu kutoka Hospitali ya Rufaa Jesse Samweli alikiri kumpokea mtoto huyo ambaye tayari wameanza kumpatia matibabu 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464