TANZANIA, INDIA ZAKUBALIANA KUSHIRIKIANA SEKTA YA MADINI*

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Kheri Mahimbali na Balozi wa India nchini Binaya Pradhan wamekipeana mikono ya salamu baada ya kusaini mikataba wa ushirikianio.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Kheri Mahimbali na Balozi wa India nchini Binaya Pradhan wamekubaliana kushirikiana kuendeleza maeneo ya utafiti katika madini ya Kimkakati.

Na mwandishi ,Dar es Salaam

Zikiwa zimepita takribani Siku 3 tangu Serikali ya Tanzania na Wabia kutoka Kampuni za Australia wasaini Hati ya Makubaliano ya Mikataba Mitatu ya uchimbaji Mkubwa na wa Kati kwa madini ya kimkakati, Aprili 20, 2023 Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Kheri Mahimbali na Balozi wa India nchini Binaya Pradhan wamekubaliana kushirikiana kuendeleza maeneo ya utafiti katika madini ya Kimkakati.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kilichohudhuriwa na watalaam kutoka pande zote na kufanyika katika Ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar s Salaam.

Mbali na eneo hilo, pia nchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika Sekta ya madini na kuendeleza utafiti wa jiofizikia kwa kutumia ndege (high resolution survey), kwa kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

Pia, makubaliano mengine ni kushirikiana katika mafunzo kwenye sekta ndogo ya uongezaji thamani madini hususan madini ya vito na kuendeleza rasilimali watu katika shughuli za uongezaji thamani madini.

Aidha, pande zote zimekubaliana kukamilisha taratibu za makubaliano hayo ili utekelezaji wa shughuli hizo uanze.

Makubaliano hayo ni matokeo ya jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali kupitia wizara ya Madini katika utekelezaji wa mikakati yake ikiwemo ya kufungua migodi ya uchimbaji mkubwa na kuweka msistizo katika uchimbaji wa madini ya kimkakati yakiwemo ya kinywe (graphite).

Aidha, mkakati huo unakwenda sambamba na juhudi za Wizara kuendelea kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini ili zifanyike nchini kwa kuwawezesha vijana wengi wa kitanzania kupata ujuzi katika shughuli za uongezaji thamani madini   pamoja na kuendelea  kukiimarisha Kituo chake cha Jemolojia Tanzania (TGC) kinachotoa mafunzo  ya uongezaji thamani madini ikiwemo ukataji na unga’rishaji wa madini ya vito, utambuzi na usanifu wa madini.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464