Maduka Saba Jengo la UWT yateketea Moto Shinyanga
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MADUKA Saba yaliyopo katika Jengo la Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT) Mkoa wa Shinyanga yameteketea kwa Moto.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Majira ya Saa 9 usiku.
Wafanyabiashara wakielezea tukio hilo, wamesema walipofika majira ya saa 10 Alfajiri mara baada ya kupata taarifa juu ya tukio hilo la Moto walikuta mali zote zimeshateketea Moto.
Mmoja wa Wafanyabiashara hao Edward Flavianus amesema alipofika eneo la tukio hakufanikiwa kuokoa mali yoyote, sababu vitu vyote vilikuwa tayari vimeungua moto .
“Nilipigiwa simu majira ya saa 10 Alfajiri nilipofika hapa eneo la tukio nilikuta mali zangu zote zimeteketea moto hakuna ambacho tumefanikiwa kuokoa, na moto huu inaonyesha ulianza kuwaka majira ya saa 8 usiku,”amesema Flavianus.
Nao baadhi ya Wafanyabiashara ambao Maduka yao hayakuteketea Moto, wamelipongeza Jeshi la Zima Moto na Uokoaji kwa kufika kwa wakati eneo la tukio, na kufanikiwa kuzuia moto huo usiteketeze maduka yote.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga Mrakibu Martin Nyambala, amesema Jeshi hilo lilipata taarifa ya Moto huo majira ya Saa 9 usiku, na walipofika eneo la tukio walifanikiwa kuzima Maduka Sita. lakini Saba yaliteketea Moto.
“Chanzo cha Moto huu bado kina chunguzwa, lakini tunatoa wito kwa Wafanyabiashara wawe na vizimia moto kwenye maduka yao, pamoja na kutoa taarifa mapema hasa kwa walinzi wanapoona matukio ya moto wasipige simu kwanza kwa mabosi wao, bali wapige kwa Jeshi la Zimamoto kwa namba 114,”amesema Nyambala.