RC MNDEME ATOA SIKU SABA KWA NEMC NA TANESCO MKOA WA SHINYANGA KUWAPA KIBALI NA KUUNGANISHA UMEME KWA WAWEKEZAJI MSUMBA STEEL TZ LTD NA STELLAR HMS LTD.

Na. Shinyanga RS.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina S. Mndeme ametoa siku 7 kwa NEMC kuhakikisha wanampatia Kibali muwekezaji Stellar HMS LTD na Meneja Tanesco Mkoa wa Shinyanga Eng. Leo Mwakitobe kwa kumuunganishia huduma ya  umeme muwekaji Msumba Steel Tz LTD, ili waweze kuanza uzalishaji mara moja.

Hayo yamesemwa leo tarehe 12 Juni, 2023 na Mhe. Mndeme alipokutana nao katika Ofisi yake kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wawekezaji Mkoa wa Shinyanga jambo ambalo limepelekea kuchelewa kuanza kwa uzalishaji na kuchelewesha maendeleo kwa wananchi.

"Natoa siku 7 kwa NEMC kupitia kwako Ndg. Abel Sembeka Meneja wa Tathimini za Athari za Kimazingira uliyekuja hapa leo kuhakikisha mnampatia Kibali muwekezaji Stellar HMS LTD pamoja nawe Meneja wa Tanesco Mkoa wa Shinyanga Eng. Leo Mwakitobe kuhakikisha unamuunganishia umeme muwekezaji Msumba Steel Tz LTD ili waweze kuanza uzalishaji mara moja kwakuwa wapo tayari isipokuwa wanashindwa kutokana na changamoto hizo," alisema Mhe. Mndeme.

Kwa upande wake Ndg. Sembeka alimueleza Mhe. Mndeme kuwa taratibu zote za utoaji wa Kibali zipo hatua ya mwisho kabisa na kwamba muwekezaji atakabidhiwa wakati wowote kuanzia sasa.

Aidha Meneja wa Tanesco Mkoa wa Shinyanga Eng. Leo Mwakitobe pamoja na kupokea maelekezo ya Mhe. Mndeme alisema kuwa uchelewaji ulitokana na ukosefu wa Transfoma ambayo ndiyo ingetumika kumuunganishia umeme muwekezaji huku akiahidi kulifanyia kazi japokuwa aliomba aunganishiwe mwezi Julai, 2023.

Awali akitoa utangulizi wake Mheshimiwa Mndeme aliwaeleza wataalamu hao kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anafanya kazi kubwa sana ya kuhamasisha na kushawishi wawekezaji kutoka ndani na nje ya Nchi kuja kuwekezaj kwakuwa Tanzania kuna kila kitu na hakuna urasimu katika kuwawezesha wawekezaji.

"Sasa inapotokea tena kunakuwa na viashiria vya urasimu katika kuwawezesha wawekeze hiyo mimi sintokubaliana nayo na haitakubalika kabisa, na sasa niwatake muache kabisa urasimu na kusiwepo kwa urasimu wala rushwa kahisa wya aina yoyote jambo ambalo litapelekea kumkwamisha muwekezaji katika Mkoa huu wa Shinyanga,"alisema Mhe. Mndeme.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464