JESHI LA POLISI SHINYANGA LIMEKAMATA MADAWA YA KULEVYA


Kamanda wa Jeshi la Poilsi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akionyesha Madawa ya kulevya aina ya Bangi ambayo wameikamata.

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga, limekamata madawa ya kulevya aina ya Bangi Kilo 60 na Gramu 540, Mirungi Bunda 58, Heroine Kete 166, pamoja na Mafuta ya Diesel lita 60 na Petrol lita 20 yaliyotajwa kuibwa kwenye ujenzi wa Reli ya kisasa SGR.
Kamanda wa Jeshi la Poilsi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akionyesha Madawa ya kulevya aina ya Bangi ambayo wameikamata.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi, amebainisha hayo leo Juni 21, 2023 wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, kwa doria walioifanya kwa kipindi cha Mwezi mmoja kuanzia Mei 28 hadi Juni 21 mwaka huu.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema mbali na kukamata Madawa hayo ya kulevya, pia wamekamata vitu mbalimbali vya wizi zikiwamo Television Mbili, Godoro Moja, Subwoofer Moja, CPU Mmoja, Pikipiki Nne, Baiskeli Mbili, pamoja na Silaha aina ya Pistol yenye namba 071T4823 ikiwa na Risasi Tano.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akionyesha Pistol na Risasai Tano ambazo wamezikamata.

“Tumekamata Jumla ya watuhumiwa 19 tunawashikilia katika vituo vyetu vya Polisi, na wengine kati yao wapo nje kwa dhamana kwa kuhusika na Makosa niliyoyataja hapo juu,”amesema Magomi.
Aidha, Kamanda amesema kwa upande wa makosa ya usalama barabarani 3,352 yalikamatwa na kulipwa faini, huku madereva wawili wa mabasi wakiwafungia Leseni zao kutokana na makosa hayo ya kukiuka sheria za usalama barabarani.

Katika hatua nyingine Kamanda ametaja mafaniko ambayo wameyapata katika kesi mbalimbali zilizokuwa zikiendelea Mahakamani, kwamba Mtuhumiwa Mmoja wa Mauaji amehukumiwa kunyongwa hadi kufa, na kesi nyingine ni ya kujaribu kubaka mtuhumiwa amefungwa miaka 20 Jela.
Pikipiki na Baiskeli ambazo zimekamatwa.

Ametaja kesi nyingine walizopata mafanikio kuwa ni kesi mbili za kubaka ambapo watuhumiwa walifungwa miaka 30, kesi ya kumpa mimba mwanafunzi na kutorosha mwanafunzi na watuhumiwa wote wamefungwa miaka 30, na kesi nyingine ya kujeruhi mtuhumiwa amefungwa miaka 30, na kesi ya kujifanya mtumishi wa Serikali mtuhumiwa amefungwa miaka miwili Jela.
Madumu yenye mafuta ambayo yamekamatwa.

“Jeshi la Polisi tunaipongeza Idara ya Mahakama na Wanasheria wa Serikali, kwa kuhakikisha adhabu kali zinatolewa kwa wale wote ambao wanaopatikana na hatia katika matukio mbalimbali ya kihalifu,”amesema Magomi.

Kamanda ametoa wito pia kwa Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, waendelee kushirikiana na Jeshi hilo katika utoaji wa taarifa za uhalifu pamoja na kudumisha Amani.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464