Mgodi wa Barrick Bulyanhulu wawainua Wananchi kiuchumi kupitia ufugaji Nyuki
Na Marco Maduhu, KAHAMA
Mgodi huo umekuwa ukiwajengea wananchi uwezo wa kujikwamua kiuchumi kupitia Program ya Biashara yako, Biashara yangu, na kutumia fursa mbalimbali ikiwamo kuanzisha vikundi na kuwezeshwa mitaji.
Moja ya kikundi ambacho kimenufaika na mafunzo hayo ni kikundi cha ufugaji Nyuki cha Twikondele ambacho kipo Kijiji cha Buyange Kata ya Bugarama Halmashauri ya wilaya ya Msalala wilayani Kahama, kilipewa Mizinga 17 ya Nyuki na Mgodi huo wa Barrick Bulyanhulu na sasa wameondokana na umaskini.
Katibu wa kikundi cha ufugaji Nyuki cha Twikondele Daniel Samson, amesema jana kwamba kupitia mafunzo hayo ya uwezeshwaji kiuchumi, waliunda kikundi cha watu 13 wakapewa Mizinga 17 ya Nyuki ambayo wamekuwa wakivuna Asali na kuiuza kwenye Masoko ya ndani na kisha kujipatia kipato na kuinuka kiuchumi.
“Tuna ushukuru Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa kutukwamua kiuchumi kupitia ufugaji Nyuki, na sasa maisha yetu yamebadilika kimaendeleo siyo kama hapo awali,”amesema Samson.
Naye Mwenyekiti wa kikundi hicho cha ufugaji Nyuki Belta Ndeki, ametaja mafaniko ya kimaendeleo ambayo ameyapata, kuwa baadhi ya wanakikundi wamejenga nyumba imara, kununua mashamba pamoja na kusomesha watoto na kuwatimizia mahitaji yao yote ya shule.
Aidha, amesema katika biashara yao ya uuzaji Asali wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa Masoko ya nje, na hivyo kushindwa kuuza Asali nyingi, na kusalia kuuza katika Masoko ya ndani pamoja na kuuzia watu binafsi na kwenye Maonesho ya Biashara mbalimbali.
Naye Kaimu Meneja Mahusiano ya Jamii Mgodi wa Barrick Bulyanhulu Zuwena Senkondo, amesema Mgodi huo umeendelea kuwa karibu na jamii katika kuwajengea uwezo na kukuza uchumi wao, na kwamba katika uwezeshaji wa jamii kupitia ufugaji Nyuki tayari wameshatoa Mizinga 200 kwa vikundi Vitano.
Amesema mbali na kuviwezesha vikundi hivyo kiuchumi kupitia ufugaji Nyuki, wamekuwa wakiwapeleka wanakikundi katika Maonesho Mbalimbali ya Biashara, ili wakajifunze kwa wenzao pamoja kupata mtandao na kupanua wigo wa biashara zao.
Amesema Mgodi huo pia kwa sasa umejenga Kiwanda cha kuchakata Asali, ambacho kitakuwa kikitumiwa na vikundi vya ufugaji nyuki kwa kuchakata Asali yao na kuwa bora zaidi, na kukidhi vigezo vya masoko ya nje.
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya ya Msalala Judica Joel. ameupongeza Mgodi huo kwa kutoa elimu kila Jumamosi ya kuwajengea Wananchi uwezo wa kuchangamkia fursa mbalimbali ambazo zinatolewa na Mgodi huo na hatimaye kujikwamua kiuchumi.
Kaimu Meneja Mahusiano ya Jamii Mgodi wa Barrick Bulyanhulu Zuwena Senkondo, akielezea namna Mgodi huo unavyoshiriki kuwainua wananchi kiuchumi kupitia ufugaji Nyuki.
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya ya Msalala Judica Joel, akielezea namna Mgodi wa Barrick Bulyanhulu unavyotoa elimu kwa wananchi kuchangamkia fursa mbalimbali za Mgodi huo na kujikwamua kiuchumi.
Katibu wa kikundi cha ufugaji Nyuki cha Twikondele Daniel Samson, akielezea namna ufugaji Nyuki ulivyowakwamua kiuchumi na kuuaga umaskini, huku akiwa amevaa mavazi maalumu ya kuzuia kung'atwa na Nyuki.
Mwenyekiti wa kikundi cha ufugaji Nyuki cha Twikondele Belta Ndeki, akielezea mafaniko ya kimaendeleo ambayo wameyapata kupitia ufugaji Nyuki.
Baadhi ya wanakikundi cha ufugaji Nyuki cha Twikondele wakiwa kwenye Mizinga ya Nyuki,huku wakiwa wamevaa mavazi maalumu ya kuzuia kung'atwa na Nyuki.
Muonekano wa baadhi ya Mizinga ya Nyuki.
Baadhi ya wanakikundi cha ufugaji Nyuki cha Twikondele wakiwa kwenye Mizinga ya Nyuki, huku wakiwa wamevaa mavazi maalumu ya kuzuia kung'atwa na Nyuki.