SHIRIKA LA TCRS KWA KUSHIRIKIANA NA WANANCHI WA WILAYA YA KISHAPU WAMEANZA MKAKATI WA KUTUNZA VISIKI HAI VYA MITI YA ASILI KWA LENGO LA KUKABILIANA NA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIA NCHI


Shirika lisilo la Kiserikali la Tanganyika Christian Refugee Service(TCRS) kwa ufadhili wa Finnish Evangelical Lutheran Mission (FELM) kwa fedha kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland kwa kushirikana na wananchi wa Wilaya ya Kishapu pamoja na Serikali ya wilaya; wanatekeleza mkakati wa kutunza visiki hai vya miti ya asili inayojiotea yenyewe kwa lengo la kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwenye maeneo ambayo miti ya kupandwa haiwezi kustahimili kutokana na ukame uliokithiri.
Hayo yamebainishwa na mwakilishi wa Mkurugenzi wa TCRS Bi. Suzy Leonard Ukio wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani yaliyofanyika katika kata ya Maganzo Wilayani Kishapu ambapo TCRS imeshiriki kwa kufadhiliwa na Shirika la kimataifa la Finish Evangelical Lutheran Mission lenye makao yake makuu nchini Finland.
Aidha Bi. Suzzy Ukio amesema katika kampeni ya kutunza Visiki hai TCRS kwa muda wa miaka mitatu iliyopita imefanikiwa kupanda miti ya aina mbali mbali zaidi ya 320,000 na kwa msimu wa 2022/2023 imetunza miti ya visiki hai takribani 4,800 katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kishapu.
Katika maadhimisho hayo yaliyoenda sambamba na kufanya usafi katika maeneo ya makaburi, maeneo ya dampo na kupanda miti katika maeneo ya wafanya biashara na pembezoni mwa Barabara ya Shinyanga - Mwanza kwa kusisitiza kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani mwaka 2023, kauli mbiu isemayo “ TUNZA MAZINGIRA, OKOA VYANZO VYA MAJI KWA USTAWI WA VIUMBE HAI NA UCHUMI WA TAIFA”. Wananchi wa wilaya ya Kishapu wamoenekana kufarijika na Shirika la TCRS na kuliomba liendelee kuwaunga mkono ikiwa ni pamoja na kutoa elimu katika shughuli za upandaji wa miti na kuitunza, utunzaji wa visikihai na usafi wa mazingira kwakuwa wilaya hiyo ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi.
Katika maadhimisho hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Bw. Emmanuel Johnson amewataka wananchi kuwa na tabia ya kutunza mazingira yao ya makazi na ya biashara kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira huku akipiga marufuku mifuko ya plastiki ambayo imepigwa marufuku na Serikali.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Maganzo Mheshimiwa Rwinzi Mbaru kidiga amesema kuwa amepokea maelekezo ya serikali kuhusu kuwasimamia wananchi katika masuala ya kutunza mazingira na kupanda miti na kuahidi kulichukua swala hilo kwa uzito na kwa vitendo.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464