RC MNDEME AZITAKA HALMASHAURI KUIMARISHA VYANZO VYA MAPATO YA NDANI NA KUDHIBITI MIANYA YA UPOTEVU WA FEDHA ZA UMMA.

Na. Shinyanga RS.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Solomon Mndeme kuanzia sasa amezitaka Halmashauri zote ndani ya Mkoa wa Shinyanga kuimarisha na kubuni vyanzo vya mapato yake ya ndani na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma.

Amebainisha hayo jana katika ukumbi wa Hospitali uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wakati akihutubia kikao maalumu cha kupokea na kujadili mapendekezo kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mkoa wa Shinyanga kwa mwaka wa fedha 2021/2022 huku akizipongeza Halmashauri ya Kishapu ambayo alianza nayo asubuhi na Shinyanga zote kwa kupata Hati Safi.

Akizungumza kwa nyakati tofauti alipokuwa Kishapu na Shinyanga amezielekeza Halmashauri kuwa na ubunifu wa vyanzo vingine vya mapato na kuvisimamia kwa weledi, uzalendo na kujituma ili kuweza kuwahudumia wananchi wake vizuri na kuhakikisha kuwa taratibu za matumizi ya fedha za Serikali yanafuata Sheria,Kampuni na miongozo mbalimbali ili kupunguza kama siyo kuondoa kabisa Hoja za CAG.

"Nazielekeza Halmashauri zote ndani ya Mkoa huu wa Shinyanga kuhakikisha kuwa mnaimarisha na kubuni vyanzo vya mapato yenu ya ndani sambamba na kudhibiti mianya yote ya upotevu wa fedha za umma jambo ambalo mkilitekeleza litatuondolea kabisa hizi hoja za CAG kwakuwa sehemu kubwa ya hoja hizi zinaepukika kabisa na kuanzia sasa kila vikao vyenu vya kila mwezi au katika mabara ya robo mtenge muda kujadili hoja hizi siyo mpaka kipindi cha ukaguzi liwe ni zoezi endelevu kwenu," alisisitiza Mhe. Mndeme.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mndeme ameonekana kutoridhishwa na kitendo cha Halmashauri ya Kishapu na Shinyanga kushindwa kufikia asilimia 100 ya lengo la makusanyo ya mapato kwa mwaka huu unaoishia tarehe 30 Juni, 2023 wakazi Halmashauri nyingine zimefikisha na kuvuka lengo ambapo mpaka sasa Kishapu imefikisha 85% na Shinyanga 75% na kuwataka kufikisha asilimia zilizobakia kabla ya Juni 30, 2023.

Kwa upande wake Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mkoa wa Shinyanga Ndg. Patric Malando amezikumbusha Halmashauri kuwa na utaratibu wa kufuata taratibu na miongozo pamoja na sheria za ufungaji wa kitabu cha hesabu, kutoa taarifa kwa umma na kuifikia Ofisi yake wanapokuwa wanahitaji msaada wowote kuliko kusubiria wakati wa ukaguzi.

Pamoja na kuwapongeza sana viongozi wa Halmashauri hizo, lakini amewataka kuendelea na ushirikiano wao ambao ameuona, amempongeza pia Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi kwa kuchapa kazi vema kabisa na akawapongeza wakurugenzi wote kwa kuendelea kuaminiwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kumsaidia kazi.

Mhe. Mndeme amefanya vikao maalumu katika Halmashauri ya Kishapu na Shinyanga ikiwa ni muendelezo wa ushiriki wake kikamilifu katika mabaraza ya Waheshimiwa Madiwani kwa lengo kuhakikisha kuwa Shinyanga haipati kasoro itokanayo na Ofisi ya CAG, na kesho atahudhuria na kushiriki katika ya Manispaa ya Shinyanga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464