HUDUMA ZA MAJI ZIBORESHWE KWA WATUMISHI WA MAJI KUTUMIA NAFASI ZAO VYEMA
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza na watumishi wa MWAUWASA (hawapo pichani) wakati wa kikao chake na watumishi hao
Na
Mohamed Saif
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi
Cyprian Luhemeja amewataka watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa
Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kuhakikisha wanatumikia vyema nafasi zao
walizoaminiwa ili kuboresha hali ya
upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo mbalimbali wanayohudumia.
Mhandisi
Luhemeja ametoa maelekezo hayo kwa nyakati tofauti Juni 15, 2023 alipofanya
ziara kwenye Ofisi mbalimbali za MWAUWASA ili kuzungumza na watumishi na
kujadili changamoto zinazowakabili katika ufikishaji wa huduma ya majisafi na
salama kwa wananchi lengo likiwa ni kuzipatia ufumbuzi wa pamoja na kuimarisha
upatikanaji wa huduma ya maji Mwanza.
Ikiwa
ni ziara yake ya kwanza Jijini Mwanza tangu ateuliwe kuwa Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Maji, Mhandisi Luhemeja alitembelea Ofisi zote za Kanda za MWAUWASA
na kuzungumza na watumishi na kisha alihitimisha ziara yake kwenye Makao Makuu
ya Mamkala hiyo katika jengo la Maji House kwa kukutana na watumishi wote.
"Ninaamini
MWAUWASA mnao uwezo wa kufanya vizuri zaidi katika kuwahudumia wananchi, nina
imani mkijipanga vyema hali ya huduma ya maji itaimarika," alisema Naibu
Katibu Mkuu Luhemeja.
Alisema
Jiji la Mwanza ni Jiji la Kimkakati na kwamba linahitaji kuwa na huduma bora na
ya uhakika ya majisafi na salama hasa ikizingatiwa kuwa Serikali imewekeza
fedha nyingi kuhakikisha huduma inaimarika.
"MWAUWASA ni
Mamlaka ya Maji ya pili kwa ukubwa baada ya DAWASA, mpo kimkakati na Mkoa wa
Mwanza ndio kitovu cha Kanda ya Ziwa na huu Mkoa unaakisi masuala yote ya
kiuongozi Kanda ya Ziwa," alisisitiza Mhandisi Luhemeja.
Aidha,
Mhandisi Luhemeja aliwaasa watumishi wa MWAUWASA kuhakikisha wanatanguliza
mbele uzalendo, nidhamu, ubunifu, kuheshimiana na kufanya kazi kwa pamoja kwa
maslahi mapana ya wananchi wanaowahudumia.
Mhandisi
Luhemeja alisema Serikali imewaamini watendaji wa MWAUWASA na hivyo kuwapa
dhamana ya kuwafikishia wananchi wa Mwanza huduma ya maji na aliwasisitiza
kuhakikisha wanaienzi amana hiyo ili dhamira ya Serikali ifikiwe kikamilifu.
"Malalamiko ni
mengi, hakikisheni mnajipanga vyema, mnasimamia kikamilifu usambazaji wa maji
ili kufikisha huduma kote mnapopaswa kufikisha. Uzuri wa maji unaweza
kuyahifadhi sio kama umeme kwahiyo mjitahidi wananchi yawafikie,"
ameelekeza Mhandisi Luhemeja.
Alisema
upotevu wa maji ni mkubwa na aliielekeza Menejimenti ya MWAUWASA kuhakikisha
inajipanga na inakuja na mikakati dhabiti ikiwa ni pamoja na kuishirikisha
Wizara ya Maji katika harakati za kupunguza upotevu wa maji ili kuongeza
upatikanaji wa maji wanayozalisha.
"Ninawahakikishia sisi kama Wizara, chini ya
uongozi wa Waziri wetu Mhe. Jumaa Aweso hatutawaangusha, tutaendelea
kushirikiana nanyi kwa maslahi mapana ya wananchi ili dhamira ya Rais wetu
mpendwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua Mama ndoo ya maji kichwani
inafikiwa kikamilifu," alisisitiza Mhandisi Luhemeja.
Naibu
Katibu Mkuu Mhandisi Cyprian Luhemeja anaendelea na ziara yake Mkoani Mwanza ya
kukagua miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa.
.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464