JAMII IPATIWE ELIMU YA TIBA YA SAIKOLOJIA ILI KUPUNGUZA ATHARI ZA UDHALILISHAJI.
Mwanasaikolojia Hussein Mohamed akizungumza wakati wa mafunzo
Na mwandishi wetu.
JAMII imetakiwa kujengewa uwezo wa kutambua na kuweka mkazo kwenye upatikanaji wa tiba ya saikolojia na ushauri nasaha ili kuwasaidia waathirika wa matukio ya udhalilishaji kukabiliana na changamoto za kisaikolojia zinazowaathiri baada ya kufanyiwa vitendo hivyo.
Ushauri huo umetolewa na wanasaikolojia Zanzibar wakati wa mafunzo kwa familia za waathirika wa matukio hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark (DANIDA) kuwajengea uwezo kukabiliana na hali baada ya kukukumbwa na vitendo hivyo kwa lengo la kupunguza athari za kisaikolojia na kijamii zinazoweza kujitokeza.
Wameeleza ukosefu wa elimu kuhusu umuhumu wa tiba ya saikolojia na ushauri nasaha inapelekea waathirika wengi kuchukua maamuzi yanayoongeza zaidi vitendo vya ukatili kwenye jamii ikiwa ni pamoja kujichukulia hatua mkononi ikiwemo kujiua na wakati mwingine kuwaumiza wengine kimwili na kisaikolojia.
Aidha walibainisha kwamba zipo njia mbalimbali za kutoa huduma ya saikolojia na ushauri nasaha ambazo ni muhimu kutolewa kwa waathirika ikiwa ni utoaji wa huduma kwa waathirika pamoja na familia zao ili kutambua namna ya kukabiliana na hali husika bila kuwaathiri zaidi.
Hussein Mohamed ambaye ni mwanasaikolojia ameeleza suala la tiba ya saikolojia na ushauri nasaha ni changamoto katika jamii kutokana na kukosekana uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa tiba hiyo na kupelekea waathirika wengi kuumizwa zaidi kisaikolojia bila kupata msaada sitahiki.
“Bado uelewa kuhusu umuhimu wa tiba ya saikolojia ni ndogo katika jamii, na hii inapelekea kuwaongezea matatizo zaidi waathirika na familia zao kwani wanakosa tiba sahihi namna ya kukabiliana na hali ile baada ya kupata changamoto hiyo jambo ambalo ni hatari,”alieleza mwanasaikolojia Hussein Mohamed.
Kutokana na changamoto hiyo, aliwataka wadau mbalimbali kuwekeza nguvu katika kuhimiza na kutoa elimu kwa jamii kuelewa umuhimu wa tiba ya saikolojia na ushauri nasaha ili kusaidia kupunguza athari zitokanazo na vitendo hivyo katika jamii.
Alieleza, “Kama tunavyokwenda hospitali kutafuta matibabu ya maradhi mbalimbali, na tiba ya saikolojia ni muhimu tuiwekee kipaumbele na kuitilia mkazo zaidi ili itusaidie kukabiliana na athari za kisaikolojia ambazo huwaathiri waathirika na familia zao baada ya kufanyiwa vitendo hivi.”
Kwa upande wake mwanasaikolojia Asia Saleh, aliwahimiza wazazi na walezi kuwa tayari kuwatafutia msaada wa kisaikolojia waathirika wa matukio hayo ili kuepusha madhara zaidi.
“Wazazi jitahidini kuwakutanisha mapema waathirika wa udhalilishaji na washauri nasaha ili wawasaidie kuwarejesha katika hali zao za kawaida na kuwaepusha na athari zaidi za kisaikolojia zinazoweza kuwakumba kutokana na kufanyiwa vitendo hivyo,” alisema Asia.
Katika hatua nyingine alitaja baadhi ya dalili zinazoweza kujitokeza iwapo mtoto amefanyiwa udhalilishaji na kuwataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ili kubaini mabadiliko yote kwa watoto na kuchukua hatua.
Alieleza mwanasaikolojia huyo, “mara nyingi mtoto akifanyiwa udhalilishaji anakuwa na wasiwasi uliopitiliza, kupoteza kumbukumbu na inaweekana akawa na hasira za mara kwa mara, kwasababu ya kitendo alichofanyiwa kinamuathiri kwa kiasi kikubwa.”
Mapema afisa wa kupinga udhalilishaji wa TAMWA Zanzibar, Zaina Abdalla, alisema chama hicho kinatoa elimu ya ushauri nasaha kwa waathirika na familia zao ili kuwajengea uwezo wa kuendelea kudai haki zao katika vyombo vya maamuzi bila kukata tamaa.
“TAMWA Zanzibar imeandaa mafunzo haya ya saikolojia na ushauri nasaha kwa familia za waathirika wa udhalilishaji kuwasaidia kutambua namna ya kukabiliana na hali yake ili kuwa na ujasiri wa kwenda kutoa ushahidi kwenye vyombo vya sheria na kupata haki zao,” amesema Zaina.
TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark (DANIDA) linatekeleza mradi wa kutumia jukwaa la habari kumaliza vitendo vya udhalilishaji Zanzibar ambapo kupitia mradi huo waathirika wa matukio hayo wanajengewa uwezo wa kisaikolojia ili kuwa tayari kusimama kutoa ushahidi katika vyombo vya sheria na kupata haki zao.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464