SERIKALI YAAGIZA ELIMU ITOLEWE KWA WANANCHI CHANJO YA ZIADA(BOOSTER)-UVIKO -19
Wakuu wa wilaya za Shinyanga, Johari Samizi (kushoto) na Kahama Mboni Muhita (kulia) wakifuatilia kikao.
Mmoja wa wataalamu kutoka Shirika la THPS, Dkt. Appolinary Bukuku.
Sehemu ya wajumbe wa kikao cha tathimini ya chanjo ya Uviko-19 mkoani Shinyanga wakifuatilia kikao.
Na
Suleiman Abeid
HALMASHAURI
za wilaya mkoani Shinyanga zimeagizwa kuanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu
chanjo ya ziada (booster) kwa watu ambao walichanja chanjo ya kinga ya virusi
vya Uviko-19 ili kuimarisha zaidi kinga zao dhidi ya ugonjwa huo hatari.
Agizo
hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme wakati akifungua
kikao cha tathimini ya Chanjo ya kinga ya Uviko-19 ambacho kimefanyika kwenye
ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya mkuu wa mkoa.
Kikao
hicho kimewakutanisha wakuu wa wilaya, wataalamu kutoka Idara ya Afya ngazi ya
mkoa na Halmashauri, wadau wa afya kutoka Shirika la THPS na wakurugenzi wa
Halmashauri za wilaya katika mkoa wa Shinyanga.
Mndeme
amesema Serikali kupitia wizara ya afya imepanga kufanyika kwa chanjo ya ziada
(booster) kwa wale waliopata chanjo ya awali lengo ikiwa ni kuongeza kinga
zaidi kwa walengwa.
Mbali
ya halmashauri za wilaya lakini pia Mndeme ameagiza kuwepo kwa ushirikishwaji
wa makundi mbalimbali katika kufanikisha chanjo kama ilivyofanyika kwenye
chanjo ya awali ambapo mkoa wa Shinyanga ulivuka lengo kwa kuchanja asilimia
100.6.
“Mkoa wa Shinyanga
tumefanya vizuri sana katika nchi yetu kwa suala hili la chanjo, tuna kila
sababu ya kujipongeza, kwa hiyo tunaamini kinga ni bora kuliko tiba. Lakini
pamoja na kufikia lengo la kutoa chanjo hii ya Uviko-19 bado kuna wateja
wanaofikia miaka 18 wataendelea kuwepo kila mwaka,”
“Serikali
kupitia wizara ya afya imepanga kufanyika kwa utoaji wa chanjo ya ziada yaani
booster, kwa wale wote waliopata chanjo za awali lengo kuongeza kinga zaidi kwa
walengwa, tuendelee kutoa elimu na kushirikisha wadau wote katika zoezi hili,”
amesema Mndeme.
Mkuu
huyo ameagiza kushirikishwa kwa makundi mbalimbali ya kijamii katika zoezi la
utoaji chanjo hiyo ya ziada wakiwemo viongozi wa dini, machifu waliopo mkoani
Shinyanga, vyombo vya habari, viongozi wa serikali za vijiji na vitongoji
washirikishwe, ili watu wengi waweze kufikiwa.
“Tunataka kila
mwananchi ashirikishwe, kwa sababu kulingana na sensa ya mwaka 2022 tunao sasa
wananchi wengi na vijana wengi ambao wanaongezeka kuanzia miaka 18 na kuendelea
ambao mwaka 2022 hawakuwa katika umri huo, lakini sasa kuanzia mwaka huu
wamefikia umri wa miaka 18, wote sasa tuwafikie,” ameeleza.
Hata
hivyo mkuu huyo amewataka watendaji wote na wataalamu wa afya wakatoe elimu
hiyo kwa kutumia hekima zao badala ya kutumia nguvu na watoe elimu ambayo
itawawezesha wananchi kuelewa na waondoe upotoshaji dhidi ya chanjo hiyo ya
Uviko-19 inayokwenda kutolewa kwa wananchi.
“Wataalamu wametuambia hapa kwamba bado
ugonjwa upo, Covid 19 sasa kama bado ipo, sasa tukapate chanjo, twendeni
tukatoe chanjo hii na tumwambie mwananchi chanjo hii ni bure na hakuna gharama
yoyote, maana Serikali tayari imeishagharimia na tuwaeleze haina madhara kwa
mtoto wa kiume wala mtoto wa kike,” amesema Mndeme.
Mndeme
amesema walengwa ambao wanakusudiwa kupatiwa chanjo hiyo ya ziada (booster) ni
1,071,395 ambao walipatiwa chanjo za awali na kwamba kwa sababu za ongezeko la
umri wa vijana wanaofikia miaka 18 inawezekana malengo hayo yakaongezeka na
kufikia watu wengi zaidi.
Amesema
zoezi la utoaji wa chanjo hiyo ya ziada linatarajiwa kuanza rasmi Juni 19, 2023
na itakapofika Septemba 30, 2023 walengwa wote wawe wamefikiwa na kupatiwa
chanjo hiyo na ofisi yake ipate taarifa ya kazi hiyo Oktoba mosi 2023 na kwamba
watakaoshindwa kufikia malengo yaliyowekwa watalazimika kujieleza.
Kwa
upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Faustine Mulyutu
amesema mwananchi anapopata chanjo mara nyingi ndivyo anavyoimarisha kinga zake
za mwili na kwamba inapotajwa chanjo za booster siyo kwamba ni chanjo mpya.
“Chanjo hizi za booster siyo mpya ni zile
zile ambazo imelenga kuimarisha kinga ya mwili ya mwananchi, kwa hiyo
tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kuchanja kama walivyojitokeza
mara ya kwanza na tukaweza kufikia malengo, na hii ilitusaidia sana kupunguza
vifo pamoja na magonjwa yaliyosababishwa na Uviko-19,” amesema Dkt. Mulyutu.
Naye
mmoja wa wataalamu kutoka Shirika la THPS ambaye ni Mkurugenzi wa huduma za
kinga kwenye mradi wa afya hatua, Dkt.
Appolinary Bukuku amesema Shirika lake limeamua kushirikiana na uongozi wa
Serikali ya mkoa ili aweze kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia viongozi wake.
“Sisi THPS ni miongoni
mwa wadau wa masuala ya afya hapa nchini na tumeona namna bora ya kushirikisha
jamii juu ya hii chanjo tumeanza na mkuu wa mkoa, tumemwalika hapa amekuja
ameongea na wakuu wa wilaya pamoja na wakurugenzi ambao ndiyo viongozi wenye
watu,”
“Kadri ya maagizo ya
mkuu wa mkoa, yatashuka chini kupitia wakuu wa wilaya kwenda kwa viongozi wa
kata, vijiji na vitongoji kama alivyoagiza maana wao ndiyo wenye watu na
wataweza kufikisha ujumbe ngazi ya chini, sisi kazi yetu ni kutoa elimu kwa
jamii,” Dkt. Appolinary Bukuku.
Amefafanua kuwa shughuli kubwa inayofanywa na shirika lake ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii na kwamba inapotokea jamii kuwa na mikutano wao hupata nafasi ya kutoa elimu inayohusu umuhimu wa kuchanja chanjo ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Uviko-19
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464