Na mwandishi wetu
SIKU YA MTOTO WA AFRIKA: TAMWA ZNZ YASISITIZA “MATUMIZI SAHIHI YA KIDIJITALI KWA USTAWI BORA WA MTOTO”
CHAMA Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kinaungana na nchi nyingine barani Afrika kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika kwa kusisitiza ulinzi wa mtoto katika nyanja zote.
TAMWA- ZNZ inaadhimisha siku hii kwa kuangalia zaidi ulinzi wa mtoto dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia ambao amekuwa anafanyiwa mtoto na kuathiri ustawi wa maisha yake.
Katika kuangalia ulinzi wa mtoto, TAMWA ZNZ imeandaa kongamano litakalowashirikisha wadau mbalimbali wanaotetea haki za watoto ambapo ripoti maalumu ya kusisitiza ulinzi wa mtoto itawasilishwa na kujadiliwa kuangalia nini kifanyike katika kuhakikisha mtoto anakuwa salama.
Kongamano hilo litafanyika tarehe 15/06/2023 katika ukumbi wa Rahaleo Studio kuanzia saa 2:30 asubuhi ambapo litawashirikisha watoto wenyewe, asasi za kiraia, taasisi za kiserikali, wazazi, walimu na viongozi wa dini ambapo kaulimbiu ya TAMWA ZNZ katika maadhimisho hayo ni “Matumizi Sahihi ya Kidijitali kwa Ustawi Bora wa Mtoto.”
Pamoja na mambo mengine, wadau wa haki za watoto watajadili kwa kina masuala ya ulinzi wa mtoto kwa ujumla wake kwa kuangalia mbinu sahihi zitakazosaidia kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji kwa watoto.
Katika hali zote hizo hawa ni watoto na wanahitaji kulindwa ili waweze kupita vizuri kwa mafanikio katika kipindi chote cha mpito hasa kwa vile nchi na dunia inazungumzia kutokumuacha nje mtu yeyote katika maendeleo.
Takwimu zilizotolewa mwezi Januari na ofisi ya mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinaonesha kuwa jumla ya watoto 1, 173 waliathirika na vitendo vya udhalilishaji na ukatili mwaka 2022 kati ya matukio 1,360 yaliyoripotiwa.
Hivyo TAMWA Zanzibar inasisitiza kwa taasisi zinazosimamia haki za watoto na jamii kwa kuangalia jinsi gani mtoto atalindwa dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia ambao huathiri mustakabali wa maisha yao kwa ujumla.
Aidha Sheria ya Mtoto No.6 ya 2011 imelenga kuimarisha ulinzi, matunzo na haki za watoto. Ni kinyume na sheria kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na ndio maana sheria hii ilitoa ulinzi wa mtoto katika nyanja zote kwa kuzingatia zaidi umri usiopungua chini ya miaka 18, kama inavyoeleza katika kifungu namba 19 (1) (b) cha Sheria hiyo ambacho kinasema “kwa madhumuni ya Sheria hii, mtoto yuko katika mazingira magumu na anahitaji matunzo na ulinzi ikiwa mtoto huyo; anajihusisha na tabia ambayo inaweza kuwa na madhara kwake au kwa mtu mwingine yeyote.”
Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 16 ya mwezi Juni inatokana na mauaji ya kinyama waliofanyiwa watoto waliokuwa wakiishi katika kitongoji cha SOWETO nchini Afrika ya kusini na serikali ya Makaburu ya nchi hiyo tarehe 16 Juni 1976, ambapo watoto hao waliandamana zaidi ya nusu maili wakidai haki ya kupewa Elimu bora na mazingira ya kufundishwa kwa lugha yao, ambapo kwa harakati hizo watoto zaidi ya 100 waliuawa na askari polisi wa utawala wa makaburu wa Afrika ya Kusini wakati huo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464