UMOJA wa vijana wa chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Shinyanga umesema wako bega kwa bega na mwenyekiti wa Chama Taifa Rais Samia Suluhu Hassan, huku wakiwataka wanafunzi wa vyuo kuwa na weledi, maadili na uzalendo.
Hayo yamesemwa jana na mgeni rasmi Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Shinyanga Clement Mandinda katika maafali ya Seneti kwa wanavyuo na vyuo vikuu kwa mkoa wa Shinyanga ambapo ameeleza kuhitaji nidhamu kwa vijana.
Madinda akiwa ameambatana na wajumbe wa umoja huo amesema vijana ndiyo tegemeo la Taifa hili wanataka kuona wanajitegemea kujinyanyua kiuchumi na fursa nyingi zitafunguka kwani serikali ya mkoa wa Shinyanga inaleta wawekezaji kwa uwanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo eneo la Buzwagi.
“Mama Samia ambaye ni Rais wetu katupa heshima vijana kwenye vyuo kaongeza fedha za mkopo na vyuo vya kati vitaanza kupata mkopo, hivyo sisi vijana tuanze kutembea kifua mbele”amesema Madinda.
Mjumbe wa baraza la UVCCM Taifa kutoka mkoa wa Shinyanga Monalisa Daniel Faustine amesema vijana wanahitimu vyuoni wanapokuwa mitaani wanatakiwa wawe vijana wa kuigwa na kama bado hawajapata ajira wasibweteke,wapinge ukatili wasidanganyike kutumia madawa ya kulevya na kuuza miili yao.
“Wakati mnasubiri ajira mnaweza kujitafutia kazi ambazo ni tofauti na taaluma mliyosoma, kuunda vikundi kutumia kazi za mikono yenu kutokaa vijiweni na kushawishika, serikali inawaona chama kinawaona msidanganyike”amesema Mbaraza.
Mwenyekiti wa Seneti mkoa wa Shinyanga Gerald Majaliwa amesema vijana waliopo vyuoni wazingatie masomo yao soko la ajira pia linaangalia nidhamu na ufaulu mzuri wasiishie walipo bali wajiendeleze kimasomo.
Katibu wa Seneti mkoa wa Shinyanga Jackson Mwigarubi amesema kuna vyuo vya kati mkoa wa Shinyanga na wanachama, wa Chama Cha Mapinduzi ni 1825 na hali ya kisiasa katika upande wa vyuo ni nzuri jambo la mama ni jambo letu sote, hivyo wanahitaji kuwepo na vyuo vikuu vingi kama maeneo mengine.
Mkuu wa chuo cha sayansi ya afya Kahama ambaye ni Mlezi wa CCM chuoni dk Nicodemus Kaje amesema wanaendelea kuwafundisha vijana pia maisha ya siasa kwani siasa ni maisha, wanatakiwa kufuata weledi na chama cha Mapinduzi ndiyo chama chenye mikakati na mipango mizuri.
Piter Frank kutoka BSL school amesema asilimia 98 ya vijana wamepitia kwenye chama cha Mapinduzi na kulelewa na chama na ukitaka siku zote kufanikiwa upite kwa njia nzuri, aliwataka vijana walioko vyuoni waitumie Seneti ya mkoa watengeneze CV nzuri na wasitafute ajira kwa vyeti pekee watumie na vipaji walivyonavyo.