Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akizungumza na wazee maarufu, viongozi wa dini na machifu wa mkoa wa Shinyanga
Suzy Luhende,Shinyanga Press blog
Wazee wameiomba serikali kuzungumza na kampuni zinazonunua zao hilo ziweze kupandisha bei ya kilo ya Pamba ambayo imeporomoka kutoka sh. 2000 msimu uliopita hadi sh. 1060 msimu huu.
Wazee hao wamewasilisha ombi hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme leo kwenye kikao cha viongozi wa dini, machifu na wazee mkoa wa Shinyanga kilichofanyika leo katika ukumbi wa mkuu wa mkoa, ambapo waliomba serikali isikie kilio hicho kwani wananchi wananjaa ikiongezwa bei wanaweza kununua chakula cha kutosha.
Suzana Masebu ambaye ni mjumbe wa baraza la wazee wilayani Kishapu amesema wananchi walihamasika kulima zao la Pamba kutokana na msimu uliopita kununuliwa kwa bei nzuri, hivyo kushuka kwa bei ya Pamba kumewafanya kushindwa kuhimili bei za mazao ya chakula kutokana na wakulima wengi kujikita katika kilimo Cha Pamba.
"Tunakuomba sana mkuu wetu wa mkoa utuwasilishie kilio cha wakulima wanalia kushuka kwa bei hiyo, kwani wengi wamelima lakini kutokana na tabia nchi mazao ya chakula hayakuiva, hivyo kuna njaa kubwa katika wilaya ya Kishapu, tunaomba bei ya pamba iongezwe ili tuweze kununua chakula"amesema Suzana.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Kishapu Shija Ntelezu amesema wananchi wengi hawajapata chakula kuna njaa,hivyo serikali iliangalie suala la kuongeza bei ili wananchi waweze kununua chakula kwenye maeneo ambayo walipata chakula.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Shinyanga Christina Mdeme amesema ni kweli bei ya pamba iko chini kutoka 2000 hadi 1060 kwa mwaka huu hii imesababishwa na vita vya Ukrain kwani vita hii imechukua muda mrefu, lakini serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ya kumsaidia mkulima wa zao la pamba.
"Serikali inatambua changamoto hiyo hivyo inaendelea kulifanyia kazi ili kuhakikisha wakulima wa zao la pamba wanasaidiwa, pia serikali inaendelea kulekebisha miundombinu ya barabara ili magari yanayobeba pamba yasipate
shida"amesema Mkuu wa Mkoa Mndeme.
Aidha akizungumzia suala la chakula amesema mwaka huu serikali itanunua zaidi ya tani 200,000 ndani ya mkoa wa Shinyanga na kwa sababu ya mabadiliko ya tabia nchi kuanzia sasa wamepiga marufuku uuzwaji wa chakula nje, unatakiwa ufanyike kwa mkulima wa mkoa wa Shinyanga kwa sababu hakuna uhakika wa mvua za mwaka ujao.
"Serikali itanunua mazao ya chakula ndani ya nchi na kuweka kwenye maghara yake, kwani tunatakiwa tujitosheleze sisi wenyewe chakula cha kutosha, kwa sababu halmashauri zote za Shinyanga hazina chakula cha kutosha, hivyo ambaye hana chakula cha kutosha asiuze kabisa, mwenye chakula kingi aangalie familia yake asikiuze chote, Rais wetu anawapenda wakulima ndiyo maana akawaletea pembejeo za bure"amesema Mdeme.
Aidha katika kikao hicho cha wazee, viongozi wa dini na machifu walibariki na kuunga mkono makubaliano ya mkataba kati ya Tanzania na falme za Dubai na kutoa tamko la kulaani vikali wale watu wanaopotosha jamii kupitia mitandao ya kijamii, hivyo kuahidi kuwa mabalozi katika kuelimisha katika maeneo yao ili watu wasiendelee kupotoshwa.
Chifu Charles Kidola akitoa tamko la kulaani watu wanaopotosha mkataba baina ya mkataba wa Tanzania na Falme za Dubai
akizungumza kwenye kikao hicho
Mzee maarufu akichangia hoja kwenye kikao hicho ambapo alimuomba Rais Samia Suluhu atembelee mkoa wa Shinyanga
Chifu Nshoma Haiwa kutoka Kahama akizungumza kwenye kikao hicho na kulaani vikali vitendo vya baadhi ya watu wanaopotosha kwenye mitandao ya kijamii