Chama cha ACT Wazalendo kinatarajia kufanya mkutano wa hadhara katika Manispaa ya Shinyanga na Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga ili kueleza kero mbalimbali zinazowakabili wakazi wa Mkoa huo pamoja na ufumbuzi wake.
Hayo yameelezwa leo Juni 03, 2023
na Mratibu wa mkutano wa hadhara Mkoa wa Shinyanga wa Chama cha ACT Wazalendo
Risasi Semasaba wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Chama
hicho Mkoa wa Shinyanga amesema Juni 5 mkutano wa hadhara utafanyika Manispaa ya Kahama na Juni 6 itakuwa ni Manispaa ya Shinyanga.
Amesema Juni 6 ni siku ambayo ACT
Wazalendo itaeleza ahadi zake kwa wanachama na wananchi wa Mkoa wa
Shinyanga,kutokana na kuendesha shughuli zao kwa utafiti kujua changamoto za
Shinyanga ambapo kiongozi wa ACT
Wazalendo Zitto Kabwe na viongozi wengine watazungumza na wananchi.
Risasi amesema licha ya Mkoa wa
Shinyanga kuwa na rasilimali nyingi yakiwemo madini ya dhahabu na Almasi lakini
bado wananchi wa Shinyanga ni masikini wanaachiwa mashimo pamoja na kilimo
kushindwa kuwanufaisha wakulima.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa ACT
Wazalendo Mkoa wa Shinyanga Siri Yasini amesema wanakuja kuwasha moto Shinyanga
kwa kuweka wazi changamoto zilizopo zinazokwamisha maendeleo na kuwataka
wananchi kuchukuwa hatua.
Amesema Juni 5 utafanyika mkutano
wa hadhara Kahama na Juni 6 uwanja wa Nguzonane Shinyanga Mjini ambapo ACT
Wazalendo itakwenda kuweka historia na kuwaomba wananchi kushiriki.
“Hii yote ni kuiona Demokrasia
inaanza kufuata mkondo wake,Demokrasia ni kuhakikisha kwamba mawazo chanya
yanapatikana hii Tanzania ni ya watu wote hivyo kila mmoja anawajibu wa
kuhakikisha maendeleo yanapatikana”amesema Yasini.
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya ACT Wazalendo
Nyangaki Shilungushela amesema wananchi walikuwa gizani kutokana na vyama vya
siasa kunyimwa uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara na wananchi kutoa maoni yao
lakini kwa sasa watumie fursa hiyo.