RPC MAGOMI AFUNGA MAFUNZO YA UTAYARI AWAMU YA KWANZA KWA WAKAGUZI NA WAKAGUZI WASAIDIZI WA JESHI LA POLISI SHINYANGA


RPC MAGOMI AFUNGA MAFUNZO YA UTAYARI AWAMU YA KWANZA KWA WAKAGUZI NA WAKAGUZI WASAIDIZI WA JESHI LA POLISI SHINYANGA
Na Mwandishi wetu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amefunga mafunzo ya utayari Awamu ya kwanza kwa Wakaguzi na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la polisi Mkoani Shinyanga.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania leo Jumatatu Julai 3,2023 katika Viwanja vya polisi Barracks Kambarage Manispaa ya Shinyanga, Kamanda Magomi amesema mafunzo hayo ya miezi miwili yalilenga kuwajengea uwezo na ukakamavu askari hao ili kuweza kufanya kazi zao kwa weledi na uadilifu katika kupambana na uhalifu.

“Mazoezi haya ni muendelezo wa ratiba ya kawaida kwa askari wa vyeo mbalimbali ndani ya jeshi la polisi, miongoni mwa mambo mbalimbali yaliyofanyiwa mazoezi/mafunzo ni pamoja na gwaride la Heshima, Riot drill, Pivot drill, Section battle drill pamoja na kufunga na kufungua silaha”,amesema Kamanda Magomi.

Ameeleza kuwa, pia kulikuwa na mafunzo ya darasani katika masomo ya sheria, sayansi ya jinai, usalama barabarani, huduma ya kwanza, polisi jamii, na masomo ya ulinzi wa mipaka kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania lakini pia walifundishwa kuhusu masuala ya rushwa pamoja na masomo ya afya ya akili kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Kamanda Magomi amewasisitiza wakaguzi hao kwenda kutumia ujuzi walioupata kwa ajili ya manufaa ya wananchi ili kuleta tija na kujenga imani kwa wananchi hao.

Aidha Kamanda Magomi amewataka wakaguzi hao kwenda kushirikiana na sungusungu waliopo katika maeneo yao huku wakizingatia kauli mbiu ya Jeshi la Polisi ya “Nidhamu Haki Weledi na Uadilifu, Ndiyo Msingi wa Mafanikio Yetu”.

Kutamatika kwa mafunzo haya ya awamu ya kwanza, kumetoa fursa kwa Kamanda Magomi kufungua mafunzo ya utayari kwa wakaguzi awamu ya pili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janet Magomi akizungumza wakati akifunga mafunzo ya utayari Awamu ya kwanza kwa Wakaguzi na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la polisi Mkoani Shinyanga.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464