KAMATI YA AMANI,WAZEE NA MACHIFU WATAKA LUGHA ZA STAHA KUJADILI MKATABA WA BANDARI


KAMATI YA AMANI,WAZEE NA MACHIFU WATAKA LUGHA ZA STAHA KUJADILI MKATABA WA BANDARI

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

KAMATI ya Amani na Maridhiano Mkoa wa Shinyanga wameungana na Wazee na Machifu mkoani humo,wametoa tamko la kulaani baadhi ya Wanasiasa kutumia lugha zisizo na staha kujadili Mkataba wa Bandari na kufikia hatua ya kumkashifu Rais Samia.

Tamko hilo limetolewa leo Julai 8, 2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya Amani na Maridhiano Mkoa wa Shinyanga Sheikh Balilusa Khamisi, akiwa na Baadhi ya Wazee na Machifu wa Mkoa huo.
Amesema hawajapinga suala la Mkataba wa Bandari ya Dar es salaam na Serikali ya Dubai kujadiliwa, wanachotaka lijadiliwe kwa kujenga hoja na siyo kutumia lugha zisizokuwa na staha dhidi ya viongozi wa kitaifa na kudiliki hata kumkashifu Rais.

Amesema Serikali imetoa Ruhusa kwa wadau kuendelea kutoa maoni yao juu ya Mkataba wa Bandari na kwamba yatazingatiwa, lakini baadhi ya wanasiasa badala ya kutoa maoni yao wamekuwa wakitoa kauli na lugha zisizokuwa na staha na kumtukana Rais jambo ambalo linaweza sababisha uvunjifu wa Amani.
“Kupitia kikao hiki tunatoa tamko kwamba sisi Wazee. Machifu na Viongozi wa Kamati ya Amani na Maridhiano Mkoa wa Shinyanga, hatukubaliani, tunapinga na kulaani vikali kitendo cha baadhi ya wanasiasa kutumia Lugha zisizokuwa na Staha dhidi ya viongozi wa kitaifa kujadili Mkataba wa Bandari na kumkashifu Rais,”amesema Sheikh Khamisi.

Naye Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga Chifu Kidola Njange amesema kutumia lugha zisizo na Staha kujadili Mkataba huo wa Bandari, kunaweza kusababisha uchochezi, chuki, na kuondoa umoja katika Taifa, na kuiomba Serikali kuchukulia hatua watu wanasiasa ambao wanatumia lugha chafu kujadili Bandari.
Mzee Zengo Mikomangwa, amewataka Wabunge na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wasikae kimya na kujifungia ndani, bali watoke na kufanya Mikutano ya hadhara kuwaeleza vizuri wananchi juu ya Mkataba huo wa Bandari kwa kina, na siyo kuwaruhusu baadhi ya Wanasiasa kupotosha Wananchi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464