Na Mwandishi wetu.
Waandishi habari wameshauriwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuongeza juhudi za mapambano ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Hayo yamebainishwa jana na Mratibu wa Mfuko wa Ruzuku wa Wanawake Tanzania(WFT-Trust) Groly Mbia wakati akihitimisha mafunzo ya siku mbili ya Mtandao wa waandishi wa Habari za Ukatili Tanzania(TAJOGEV) yaliyofanyika mkoa wa Shinyanga.
Amesema, Taasisi yao inafanya kazi na wadau mbalimbali kutoka sekta zote ambao wanania ya kutokomeza ukatili wa kijinsia ndani ya jamii dhidi ya wanawake na watoto.
" Kuna jambo la kujifunza kwa waandishi kutoka mikoa mingine, kwa waandishi wa habari Shinyanga, na amini hata mkirudi katika mikoa yenu mtaweka umoja na asasi za kiraia huko mkoani kwenu ili kuwa na sauti ya pamoja ya kupaza sauti"amesema Mbia.
Aidha,anasema mfuko huo utaendelea kushirikiana na Taasisi za kihabari zilizo na mawazo yenye kulenga kuondoa mifumo kandamizi ya ukatili ndani ya jamii.
Katika hatua nyingine amesema milango iko wazi kwa klabu za waandishi wa habari kutoka mikoa mingine kuomba Ruzuku.
Nao baadhi ya Waandishi wa habari ambao wameshiriki mafunzo hayo,wamesema yatawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao katika kuandika habari za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464