RC MNDEME AZINDUA RASMI SHUGHULI ZA UZALISHAJI WA ALMASI MGODI WA MWADUI

RC MNDEME AZINDUA RASMI SHUGHULI ZA UZALISHAJI WA ALMASI MGODI WA MWADUI

Na Marco Maduhu, KISHAPU

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, amezindua Rasmi shughuli za uzalishaji wa Madini ya Almasi katika Mgodi wa Mwadui (Williamson Diamond LTD) uliopo wilayani Kishapu, mara baada ya kusimamisha uzalishaji kwa kipindi cha miezi Nane kutokana na bwawa la awali la kuhifadhia Majitope kupasuka.

Mndeme amezindua uzalishaji huo wa Almasi leo Julai 17, 2023 akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama, pamoja na Mbunge wa Kishapu Boniphace Butondo, ambapo bwawa la awali lilipasuka Novemba 7 mwaka jana, na kusababisha shughuli za uzalishaji wa Almasi kusimama.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Chrisitna Mndeme akibonyeza Batani kuzindua Rasmi shughuli za uzalishaji wa Madini ya Almasi Mgodi wa Mwadui.

Amesema amefarijika kuona uzalishaji wa Almasi unaanza tena, na kuagiza Mgodi huo uanze pia usanifu wa bwawa jingine jipya, ili hilo la sasa hivi likijaa tena uzalishaji usisimame na kusababisha Serikali kukosa mapato, pamoja na wananchi kushindwa kutekelezewa miradi ya maendeleo kupitia fedha za CSR.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Chrisitna Mndeme akibonyeza Batani kuzindua Rasmi shughuli za uzalishaji wa Madini ya Almasi Mgodi wa Mwadui.

“Niliagiza ujenzi wa bwawa hili jipya la kuhifadhia Majitope mlikamilishe haraka na uzalishaji muanze mwezi Agost, pia akaja Waziri wa Madini Dotto Biteko naye akaagiza hadi Julai 15 muwe mmeanza uzalishaji, lakini mmetekeleza Maagizo haya kwa wakati na leo nazindua Rasmi shughuli za uzalishaji wa Almasi kuanza tena,”amesema Mndeme.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akifungua mtambo wa kusafirisha Majitope kutoka eneo la uzalishaji Madini kwenda kwenye Bwawa la kuhifadhia maji hayo.

“Maelekezo yangu kwenu muongeze kasi ya uzalishaji wa madini ili kufidia muda ambao muliupoteza, na mrudi katika kiwango chenu cha juu cha uzalishaji wa Almasi, na pia bwawa hili jipya mlifanyie ukaguzi wa mara kwa mara ili nalo lisije kupasuka na kuleta madhara kwa wananchi,”ameongeza.
Naye Mbunge wa Kishapu Boniphace Butondo, amepongeza Mgodi huo kuanza tena shughuli za uzalishaji wa Madini, jambo ambalo amesema litarudisha tena kasi ya maendeleo kwa wananchi wa Kishapu, pamoja na Halmashauri kuongeza Mapato kupitia kodi ya ushuru wa huduma.
Mbunge wa Kishapu Boniphace Butondo.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Almasi Mwadui Mhandisi Ayoub Mwenda, amesema bwawa hilo jipya la kuhifadhia Majitope lina kipindi cha miaka miwili, ambapo wataanza pia usanifu wa ujenzi wa bwawa jingine jipya ambalo litakuwa la kipindi kirefu, huku akiahidi kwamba wataongeza kasi ya uzalishaji wa madini.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Almasi Mwadui Mhandisi Ayoub Mwenda (kulia) akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme.

Aidha, Mhandisi mwelekezi kutoka Kampuni ya City Enginering Aniel Macha, ambao walikuwa wanajenga bwawa hilo jipya la kihifadhia Majitope, amewatoa wasiwasi wananchi kwamba ujenzi wa bwawa hilo ni imara, na halitaweza kupasuka sababu wameweka vipimo ili likitokea tatizo wawahi kulifanyia ukarabati na walifuata taratibu zote za kihandisi na vibali vya ujenzi.
Mhandisi mwelekezi kutoka Kampuni ya City Enginering Aniel Macha.

Amesema mbali na kulijenga bwawa hilo kwa ubora zaidi, pia watakuwa wakifanya ukaguzi kila baada ya miezi mitatu, ili kuendelea kujiridhisha kwa uimara wake na kufanya matengenezo pale wanapokuta kama kuna tatizo.
Viongozi wakiangalia bwawa jipya ambalo limejengwa la kuhifadhia Majitope katika Mgodi wa Almasi Mwadui na kuanza kutumika.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, (kulia) akimpongeza Meneja Mkuu wa Mgodi wa Almasi Mwadui Mhandisi Ayoub Mwenda kwa kutekeleza maagizo ya Serikali kwa wakati na kuanza tena shughuli za uzalishaji wa Almasi.
Muonekano wa baaadhi ya Mitambo ya uzalishaji wa Almasi.
Mitambo ya uzalishaji wa Almasi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme awali akisalimia na Mwenyekiti wa Halmashauri Wiliamu Jijimya alipowasili kuzindua Rasmi Shughuli za uzalishaji wa Almasi katika Mgodi wa Mwadui.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme (katikati) akiwa na viongozi mbalimbali alipowasili kuzindua Rasmi Shughuli za uzalishaji wa Almasi katika Mgodi wa Mwadui mara baada ya kusimama kwa muda wa miezi Nane kutokana na bwawa la awali kupasuka na kusimamisha uzalishaji.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464