RC MNDEME AMEAGIZA KILA HALMASHAURI MKOANI SHINYANGA KUANZISHA DAWATI NA OFISI MAALUMU KWA AJILI YA KUSHUGHULIKIA MASUALA YA MACHINGA

Mkuu wa wilaya ya Kahama Mboni Mhita.

RC Mndeme ameagiza kuanzishwa madawati na Ofisi za kushughulikia masuala ya Machinga.

Na. Shinyanga RS

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Solomon Mndeme ameziagiza Halmashauri zote Mkoani Shinyanga kuanzisha Dawati na Ofisi Maalumu itakayokuwa na jukumu kuratibu na kushughulikia mambo yote yanayohusu Machinga katika maeneo yao.

Agizo hilo amelitoa leo Julai 22, 2023 wakati akifungua rasmi Kongamano la Shirikisho la Umoja wa Machinga Mkoa wa Shinyanga lililofanyika Wilaya ya Kahama lenye lengo la kumpongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya kwa watanzania wote na hasa Machinga nchi nzima.

Mhe. Mndeme ametoa agizo hilo baada ya kupokea risala ya Shirikisho la Machinga lilisomwa kwake na Mwenyekiti wa SHIUMA TAIFA ndugu Ernest Matondo ambayo ndani yake ilieleza umuhimu wa uwepo wa Dawati na Ofisi Maalumu katika kila Halmashauri ambapo Manispaa ya Kahama wao walikwisha anza kutekeleza mpango huu.

"Nimeskiliza kwa makini lisala yenu, yapo tutakayo yabeba kwenda kuyatekeleza, yapo mengine nayatolea majibu hapa hapa na sasa naagiza kila Halmashauri hapa Mkoani Shinyanga ianzishe haraka Dawati na Ofisi Maalumu itakayokuwa na jukumu la kuratibu na kushughulia mambo ya Machinga peke yake agizo hili lianze kutekelezwa haraka iwezekanavyo," alisema Mhe. Mndeme.

Kando na hayo, pia SHIUMA kwa kauli moja wamesema wanamuunga mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye maamuzi ya Serikali ya Tanzania kuingia mkataba wa uboresha wa utoaji huduma katika Bandari yetu na Serikali ya Dubai na kwamba SHIUMA ipo nae baga kwa bega huku wakimtaka kutowasikiliza hao wasiokuwa na nia njema na Serikali.

Aidha Kongamano hili pia limelenga kupinga mambo yote ya ukatili wa kijinsia na mmomonyoko wa maadili katika jamii zetu, kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kupendezesha maeneo yetu kwa faida ya urithi wa Nchi na vizazi vijavyo.

SHIUMA wameipongeza sana Serikali ya Mkoa wa Shinyanga kwa kuwezesha kupatikana kwa suluhu ya machinga ambapo imejenga Soko la Ngokolo (mtumbani), Soko la Ibinzamata, Soko la C. D. T stendi ya Kahama, Soko lq Machinga (mnara wa voda) na soko la mbogamboga Mhunze lililopo Kishapu.

Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) Tanzania ulipata usajili wake wa awali mwaka 2014 kwa jina la Umoja wa Machinga Tanzania.

Mwaka 2018 Umoja ulianza kuimarika zaidi baada ya kufanya kikao kilichojumuisha Mikoa 14 kwa kushirikiana na OR - TAMISEMI chini ya Waziri Mhe. Jafo S. Jafo, Wizara ya Fedha kupitia Naibu Waziri Mhe. Ashantu Kijaji mkutano ambao ulifanyika Dodoma.

Na mwezi Mei 19, 2022 Shirikisho lilifanya mkutano mkubwa uliojumuisha Halmashauri zote 184, Wilaya zote 139 na Mikoa yote 26 kuanzia hapo SHIUMA iliimarika vema kabisa na ukizingatia kuwa ilikuwa imehamishiwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu

na sasa wanajivunia Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea uwezo viongozi wao, na ofisi kila Mkoa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464