POLISI WAKAMATA MATAIRI 5 YA ROLI YALIYOIBWA MRADI WA SGR, LITA 310 ZA DIZELI
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
JESHI la Polisi mkoani Shinyanga,limekamata Matairi 5 ya Roli pamoja na mafuta ya dizeli lita 310, yaliyoibwa katika ujenzi wa Mradi wa Reli ya kisasa (SGR), pamoja na watuhumiwa wanne wa ukataji mapanga.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Leonard Nyandahu, amebainisha hayo leo Julai 26, 2023 wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari katika msako ambao wameufanya kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia June 22 hadui Julai 25 mwaka huu.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Leonard Nyandahu.
Amesema kwa kipindi hicho wamekamata vitu mbalimbali vya wizi yakiwamo Matairi 5, Mafuta ya dizeli lita 310, yaliyoibwa katika Mradi wa SGR, Waya wa Fensi Mita 12 mali idhaniwayo ya Mgodi wa Buzwagi, na vifaa vya kupigia Ramli Chonganishi.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga Leonard Nyandahu akionyesha Matairi 5 ya Roli yaliyoibwa mradi wa SGR.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga Leonard Nyandahu akionyesha Mafuta ya Dizeli lita 310 yaliyoibwa mradi wa SGR.
Aidha, amesema pia wamekamata Bunduki 5 na Risasi zaidi ya 300, ambazo zilikuwa zimekodishwa katika makampuni ya ulinzi na watu binafsi ambao wanamiliki silaha hizo, na kuzikodisha kinyume na taratibu.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Leonard Nyandahu akionyesha Bunduki 5 na Risasi.
“Katika Msako huu licha ya kukamata vitu mbalimbali vya wizi, pia tumekamata watuhumiwa 4 ambao wamekuwa wakikodiwa kujihusisha na ukataji wa mapanga, na tumewahoji wamekiri kujihusisha na vitendo hivi katika maeneo mbalimbali,”amesema Nyandahu.
Katika hatua nyingine, amesema wamekamata Magari 3,423 na Pikipiki 882 kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani, ikiwamo kuzidisha abiria, mwendokasi, kutokuwa na lesseni, na Madereva 673 walipigwa faini.
Ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo wa Shinyanga, kufuata sheria za nchi na kuacha kujihusisha na vitendo vya kiuhalifu, pamoja na kuendelea kutoa taarifa za uhalifu kwa Jeshi hilo, ili liwachukulie hatua kali za kisheria watu ambao wanajihusisha na uhalifu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464