NaKareny Masasy,
Shinyanga.
WAMILIKI wa vituo vya kulelea watoto mchana na makao ya watoto yatima mkoani Shinyanga wametakiwa kufika tarehe 30 mwezi Septemba mwaka huu kuhakikisha wanasajili vituo vyao na nakufuata miongozo na sheria ya wizara ya maendeleo,jinsia wanawake na makundi maalum kama inavyotaka.
Kwani mkoa wa Shinyanga una vituo vya kulelea watoto wadogo mchana 88 kati ya hivyo vilivyosajiliwa ni vituo 24 sawa na asilimia 27 tu huku makao ya watoto yatima yapo matano yaliyosajiliwa ni makao mawili tu.
Hayo yamesemwa jana tarehe na kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Nuru Mpuya alipokuwa mgeni rasmi kwa niaba ya katibu tawala mkoa kwenye kikao cha wamiliki wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana ,makao ya watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu.
Dk Mpuya amesema kumekuwepo na uholela wa uanzishaji wa vituo hivi pasipo kufuata sheria,taratibu na miongozo hivyo kuanzia leo wamiliki wafanye usajili na baada ya muda uliopangwa timu itapita kukagua na kujirizisha kama utaratibu ulifuatwa.
“Katika Maazimio matano tuliyopitisha mojawapo tunataka kufikia tarehe 30 mwezi Septemba vituo vyote viwe vimesajiliwa na tukikuta mmiliki hujasajili hatua zitachukuliwa za kisheria kwa kutozwa faini,pia wamiliki wote wawe wanawasilisha ripoti zao kwa maafisa ustawi katika halmashauri”alisema dk Mpuya.
Mpuya amesema agizo kwa wakurugenzi wote wa halmashauri hakuna kituo cha kulelea watoto wadogo mchana au makao ya watoto yatakayofunguliwa kuanzia leo pasipo kupata usajili.
Ofisa ustawi wa jamii mkoa wa Shinyanga Lyidia Kwesigabo amesema hivi sasa kufanyike vikao vya mara kwa mara na kila robo ya mwaka walete ripoti ili kuelezana changamoto kwani siku moja alifanya ukaguzi nakukuta kituo kimoja hakina sifa hata moja ya kuwa kituo na walichukua jukumu la kukifungia.
“Jamani tusiwe wepesi wamiliki kulalamika tumefungiwa vituo tuangalie na sisi tumetimiza masharti yanayohitajika ambapo usajili unapatikana wizarani tena bure tusione shida kusajili ili watoto wawe salama katika malezi yao ya ukuaji”alisema Kwesigabo.
Akisoma sheria na miongozo inayosimamia uanzishwaji wa vituo hivyo ofisa ustawi wa jamii kutoka Manispaa ya Kahama Abdulraham Nuru alisema vituo hivi ni kutoa elimu changamshi siyo kufundisha pia kuna sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009, kuna sheria ya watu wenye ulemavu Namba 9,2010 kifungu cha 7,sera ya afya ya mwaka 2007 zinatakiwa kufuatwa.
Kaimu ofisa Elimu mkoa Dedan Rutazika amesema malalamiko ya wakaguzi na uthibiti ubora wa shule kuwafungia ni wale wamiliki kukiuka taratibu wamekuwa wakifundisha kwenye vituo vyao badala ya kutoa elimu changamshi.
Katibu msaidizi wa umoja wa wamiliki wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana Olivia Maganga ambaye pia mmiliki wa kituo cha Goshen amesema wanaomba muda wa mwaka mmoja ili waweze kujipanga kuweza kusajili na taratibu na miongozo,sheria na sera wako tayari kufuata.