MIKOPO UMIZA KWA AKINA MAMA ILIVYOSUMU KWENYE NDOA ZAO
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
TATIZO la ukopaji mikopo kwa akina mama kwenye Taasisi za ukopeshaji fedha (maarufu mikopo umiza au kausha damu), limekuwa tatizo la kukochea Migogoro ya kifamilia na hata miji kuvunjika na wengine kujitoa uhai.
Shinyanga ni miongoni mwa Mikoa hapa nchini ambapo wanawake wamekuwa wakijiingiza kwenye mikopo hiyo, na wakati mwingine hawatoi taarifa kwa waume zao kwamba wamechukua mikopo, na wakishindwa kurejesha marejesho wakopeshaji huenda kufilisi mali na kusababisha migogoro ya familia.
Miaka kadhaa iliyopita Mwanamke mmoja Mkazi wa Tambukaleli Manispaa ya Shinyanga Sarah Bundala (55) alijitoa uhai kwa kujinyonga, mara baada ya kushindwa kurejesha marejesho akihofia kuja kupigwa na mumewake, sababu alishamkataza kujiingiza kwenye mikopo, lakini hakusikia na alisha mlipiaga baadhi ya marejesho, bali aliendelea kukopa kwa kificho.
Tukio jingine limetokea mwezi uliopita mwanaume mmoja mkazi wa Kambarage Manispaa ya Shinyanga anayefahamika kwa jina la Kulwa Juma, alimanusura avunje mji wake mara baada ya mkewake kukopa fedha bila ya kumtaarifu na akashindwa kurejesha marejesho.
Anasema mkewake huyo hana kazi na alishaghaa kwanini wamekwenda kujiingiza kwenye mikopo na wala hakumtaarifu, bali alichukuana na mashoga zake na kupelekana kwenye Taasisi za Mikopo.
“Siku moja nikiwa nimetoka kazini nimepumzika ndani ghafla nikashaghaa watu wanabisha hodi wakaingia ndani na kujitambulisha ni wakopeshaji wakekuja kuchukua fedha zao au mali ambazo ziliwekwa dhamana, kwa kuwa na mimi siku na taarifa wala fedha wakachukua vitu ndani na kutufilisi,”anasema Kulwa.
Anasema ilibidi achukue muda kutafakari na kuona si vyema achukue maamuzi ya haraka kuvunja mji, bali alikaa na mkewake wakazungumza na akamuomba msamaha naye akasamehe, lakini ndani wamebaki hawana vitu vyote vimekwenda na wakopeshaji.
Mwanamke anayefahamika kwa jina la Zai Abdul mkazi Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, anasema baadhi ya wanawake wanakwenda kukopa huku wakiwa hawana biashara sababu ya kukumbwa na mashoga zao na pesa ambazo wanazipata hufanyia matanuzi na wakati wa marejesho ukifika ndipo huanza kahanghaika.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Dome Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga Solomoni Najulwa, anasema Taasisi hizo za mikopo zimekuwa zikisaidia akina mama wengi ambao wanania ya kufanya biashara, na wao ndiyo wamekuwa wakiwasainia barua za kuwadhamini ili wapate mikopo.
Anasema changamoto inakuja ni pale baadhi ya wanawake kutokuwa waaminifu na kudanganya kuwa wanabiashara kumbe hakuna, na mikopo ambayo huichukua huenda kufanya mambo yao mengine, na likifika suala la marejesho huenda kwenye Shirika jingine kukopa ili fedha hizo alipe kwenye mkopo wa awali.
“Unakuta mwanamke ana mikopo zaidi ya mitano na biashara hana, na dhamana ambayo ameweka kwenye mikopo hiyo ameweka vitu vile vile ambavyo aliweka katika mkopo wa kwanza, akibanwa marejesho anakwenda kukopa kwingine ili apunguze deni hivyo anajikuta ana madeni lukuki,”anasema Najulwa.
“Baada ya kukwama kulipa madeni wakopeshaji wanakwenda kufilisi katika mji husika, na chakushanghaza hata mumewake hajui ndipo Mgogoro wa familia unapotokea, na tumekuwa tukipokea kesi nyingi mno za familia kufarakana na hata kuvunjika sababu ya mikopo,”anaongeza Najulwa.
Mwanasheria kutoka Timu ya Wanasheria watetezi wa Mazingira kwa vitendo (LEAT) Teresia Fabiani, anasema kwa mujibu wa Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 namba 29 chini ya kifungu namba 59 kilichofanyiwa marekebisho mwaka (2019) kinasema mwanamke au mwanaume akienda kukopa bila makubaliano ya upande mmoja mkopo huo ni batili, na hata mali haipaswi kuchukuliwa sababu mkataba hauna makubaliano ya pande mbili.
Anasema pia Sheria ya Mikopo inayohusiana na kuweka mali rehani ya mwaka 2008(Mortgage Financing( Special Provision)Act 2008) nayo inasema mkopaji anapaswa kusema ukweli kama ana mke au mume na kutoa nyaraka ya cheti cha ndoa na pia mkopeshaji ana haki ya kuchunguza kama kweli taarifa alizopewa ni kweli.
Anasema sheria hiyo inasema mkopopaji akitoa nyaraka za uongo anapaswa kufungwa kifungo cha miezi 12, hivyo mkopaji anapaswa kutoa taarifa za ukweli ili kukwepa adhabu hiyo, na pia kama mkopaji ameficha taarifa kuonesha kama ameolewa na akapata mkopo, huo mkopo utakuwa batili.
“Kama mtu ameolewa au kuoa wakati akienda kukopa kisheria ni lazima ridhaa ya mume au mke itolewe kuweka Rehani mali kabla ya kutoa mkopo sababu hizo ni mali za familia, kutoa mkopo bila ya ridhaa ya mume au mke huo mkopo ni batili,”anasema Teresia.
Mkurugenzi kutoka Taasisi ya ukopeshaji fedha ya (Msilikale) Robert Prosper, ambayo imekuwa ikilalamikiwa kuwafilisi wakopeshwaji, anataja taratibu za ukopaji mikopo kwamba wanawake hua wanafika na wadhamini wao pamoja na barua kutoka kwenye uongozi wa Serikali za Mitaa, na kwamba
hakuna mtu ambaye ana lazimishwa kukopa bali hupewa mikataba na kuisoma kisha kuisaini.
Anasema tatizo baadhi ya wanawake huwa siyo wa kweli bali hudanganya kwamba wanabiashara ili wapate mikopo, na kudiliki kumuazima hata rafiki yake sehemu ya biashara kwa muda ili Maafisa okopeshaji wajiridhishe ni kweli ana biashara, lakini kumbe alikuwa akidanganya na ukifika muda wa marejesho ndipo kazi inaanza ya kukimbizana.
“Shida ambayo naiona baadhi ya wanawake hawana elimu ya ujasiriamali wala biashara, na wanakopa fedha hizi kama mkumbo, na sisi hua hutufilisi tu moja kwa moja, bali hua tunawasiliana kwanza na mteja wetu pamoja na kupitia kwa viongozi ambao walimpatia barua ya utambulisho, akikwama ndipo tunakwenda kuchukua vitu alivyoweka dhamana,”anasema Prosper.
“Nawaomba tu wanawake sababu ndiyo wateja wetu wakubwa, waache kukimbilia mikopo kama hawana biashara, na wengi ukiwafutilia fedha hizi wakishachukua wanazitumia kwa mambo mengine tofauti na walivyoomba, fedha hizi zinahitaji uzizungushe kuendesha biashara yako ndipo upate marejesho,” anaongeza.
Kamanda wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga Donasian Kessy, anasema awali katika utawala wa Hayati Rais Magufuli walikuwa wakisaidia wananchi ambao walikuwa akitaka kuuziwa nyumba zao sababu ya mikopo umiza, lakini baada ya kufuatilia wakaona waache, sababu watu huenda kukopa kwa hiari yao wenyewe na kusaini mikataba.
Anasema Taasisi hizo za ukopeshaji fedha zipo kisheria na wamesajiliwa, hua hawalazimishi watu kwenda kukopa bali huenda kwa hiari yao wenyewe, na kutoa ushauri kama wanajua hawawezi kulipa marejesho wasikope, bali watumie fursa ya mikopo ya Halmashauri asilimia 10 ambayo haina Riba.
Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga John Tesha, anasema anawashaghaa wanawake kukimbilia kwenye Taasisi za fedha kukopa mikopo na kuishia kufilisiwa, na wakati kuna fursa za mikopo asilimia 10 ambazo Nne hutolewa kwa wanawake na vijana, na mbili kwa watu wenye ulemavu.
Anasema tatizo la wanawake wamezoea kupewa fedha mkononi ambazo hukopeshwa ili wakageuze matumizi ikiwamo kupeleka marejesho kwenye maeneo mengine ambayo wamekopa, lakini Halmashauri siku hizi hawatoi fedha ‘Cash’ bali wanaviwesha vikundi kununua vitendea kazi, ndiyo maana wanakwepa kukopa na kukimbilia mikopo kausha damu.
“Tunawaomba wanawake waunde vikundi vya ujasiriamali waje wakope Halmashauri fedha zipo, ila waje na mawazo yenye tija ya kibiashara, na takwimu tangu mwaka 2020 hadi Aprili 2023, tumeshatoa fedha za mikopo kwa wanawake tu Sh. milioni 311 kwa vikundi 31,”anasema Tesha.
Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga Lidya Kwesigabo, anasema migogoro ya familia na miji kuvunjika, imekuwa ikisababisha ongezeko la watoto wa mitaani mkoani humo, na ambao huishi katika mazingira hatarishi.
"Mkoa wa Shinyanga tumekuwa na watoto wengi wa mitaani na wameacha kusoma shule, moja ya sababu ni migogoro ya kifamilia ambayo imekuwa ikichangiwa pia na mikopo hii kausha damu," anasema Kwesigabo.
Anataja takwimu za watoto wa mitaani mkoani humo kuwa wapo 612, na watoto ambao wanaishi katika mazingira hatarishi ni 99,939.
-xxxx-