RC MNDEME AWATAKA WANAFUNZI WOTE KUKATAA UKATILI NA WANAFUNZI WA KIKE KUFUATA MPANGILIO WA KUVAA MAGAUNI MANNE
Na. Shinyanga RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amewataka wanafunzi kukataa ukatili wa aina yoyote na wakiona kuna viashiria vyovyote vya kufanyiwa ukatili watoe taarifa kwa wazazi, walezi, walimu, viongozi wa Serikali au katika ofisi yoyote ili mtu huyo aweze kuchukuliwa hatua stahiki huku akiwakumbusha wanafunzi wa kike kuwa ili wafanikiwe wanapaswa kufuata mpangilio wa kuvaa Magauni Manne ambayo ni la shule, mahafali, harusi na mateniti.
Mhe. Mndeme amebainisha hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Isuke iliyopo Halmashauri ya Wilaya Ushetu na kuwataka kutoiga kabisa utamaduni wa nchi nyingine zinazokwenda kinyume na tamaduni zetu za Kitanzania.
Aidha akawataka pia wanafunzi wa kiume kuwalinda dada zao, kutowafanyia ukatili wadogo zao au wengine na kujilinda wao wenyewe kwani vita ya kupambana na ukatili ni yetu sote hivyo wasikubali kabisa kutokea ukatili wa aina yoyote ile katika maeneo yao wanayoisha.
"Nataka niwaeleze wanangu wote na mnisikilize kwa makini, msikubali kabisa kufà nyiwa ukatili na mtu yoyote, na kama kuna viashiria vyovyote vya ukatili toeni taarifa mapema kwa wazazi, walezi, walimu, kwa viongozi au kwa ofisi yoyote ya Serikali, nanyi vijana muwalinde dada zenu, wadogo zenu, msiwanyie ukatili na msiache kujilinda ninyi wenyewe," alisisitiza Mhe. Mndeme.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Mndeme akiwa ameongoza na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita amekagua miradi mbalimbali itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru 2023 katika Halmashauri ya Ushetu huku akimtaka Meneja wa Tarura -Ushetu kurekebisha miundombinu ya barabara ili iweze kupitika kabla na wakati baada ya Mwenge kupita.
Mwenge wa Uhuru utatembelea miradi 6 ikiwa ni Ujenzi wa madarasa 5 Shule ya msingi Ukune, zahanati ya Igalula, nyumba ya Mkurugenzi wa Halmashauri, tanki na mtandao wa maji, kiwanda kidogo cha kuchakata nafaka na kuongeza thamani ya mazao (Kikundi cha Mpunze Industry) na mradi wa mazingira (upandaji miti).