RC MNDEME ARIDHISHWA NA MAANDALIZI YA MWENGE WA UHURU 2023 HALMASHAURI YA SHINYANGA NA MANISPAA YA KAHAMA


RC MNDEME ARIDHISHWA NA MAANDALIZI YA MWENGE WA UHURU 2023 KATIKA HALMASHAURI YA SHINYANGA NA MANISPAA YA KAHAMA.

Na. Shinyanga RS.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme ameridhishwa na maandalizi ya miradi itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru 2023 katika Manispaa ya Kahama huku akiwapongeza sana kwa ushirikiano na ubunifu wao katika kutekeleza miradi hii ya maendeleo inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita na Mkurugenzi wa Kahama Ndg. Andèrson Msumba.

"Mimi niseme kuwa nimetembelea miradi yote 6 ya Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023 nimeridhishwa na maandalizi yake, na katika hili niwapongeze sana," amesema Mndeme.

Awali akizungumza mbele ya Mkuu  wa Mkoa Mratibu wa Mbio za Mwenge Manispaa ya Kahama Ndg. Sadick Juma Kigaile amesema kuwa Manispaa ya Kahama imejiandaa vizuri sana katika miradi hii 6 yenye thamani za zaidi ya Bilioni 3.5 ambayo itakaguliwa na Mwenge ambayo ni Shule ya  Sekondari Kagongwa , Mradi wa kilimo na shamba la miti.

Miradi mingine itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023 ni Ofisi ya Kata Nyihogo, Jengo la Maabara Hospitali ya Kahama na mradi wa Barabara huku akimhakikishia kuwa katika eneo la Kituo cha Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (Nyihogo) ambapo pia kutafanyika Uzinduzi wa Jukwaa la Wanawake Manispaa ya Kahama pia shughuli mbalimbali za kijamii zitafanyika huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kushiriki sambasamba na kuchangamkia fursa.

Aidha, katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Miradi ambayo itatembelewa na Mwenge wa Uhuru ipo 9 ikiwamo Kikundi cha Vijana Wabunifu katika Kata ya Busanda ambao wao wemeweza kubuni na kutengeneza pikipiki ya tairi nne ambayo inauwezo wa kubeba abiria watatu jambo ambalo lilimfurahisha sana kuona vijana wenye uwezo mkubwa kabisa wakichapa kazi. 

Pamoja na maeneo mengine lakini pia alifika Didia katika Mashine ya kukoboa mpunga na kuongeza thamani mazo kijulikanacho KIDEVU POSHO MILL ambao pia wanajihusisha na ufugaji wa kuku na njiwa wa kisasa zaidi, ikiwamo Pia na Miradi ya Elimu na Afya.

Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023 kwa Mkoa wa Shinyanga utatembelea miradi zaidi ya 42 ambayo inathamani ya zaidi ya Bilioni 13.4 itakayojumlisha Sekta ya afya, elimu, mazingira, miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464