Picha Mtandao
Mabinti washawishiwa kufanya ngono wapate bahati ya kuolewa
· Ni kupitia ndoa za kimila (Bukwilima) za kabila la Wasukuma
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
NDOA za kimila za kabila la Wasukuma zinazofahamika kama Bukwilima ambazo zimekuwa zikifanyika katika maeneo mbalimbali ya vijijini mkoani Shinyanga, zimetajwa kuwa kichocheo cha kuendelea kuwapo kwa ndoa za utotoni katika eneo hilo la kanda ya ziwa.
Bukwilima ni ndoa ambazo zinatajwa kushawishi mabinti kufanya ngono na wanaume (hata katika umri mdogo) ili baadaye wabahatike kuolewa.
John Myola ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Agape ambalo linajihusisha na utetezi wa haki za watoto mkoani Shinyanga anasema: “Neno ‘Bukwilima’ maana yake ni bwana harusi kusindikizwa na wanaume wezake pale anapokuwa anakwenda kuoa.
“Kwa hiyo husindikizwa kwenda ukweni, yaani nyumbani kwa mwanamke kwa ajili ya kuoa ambako hukaa kuanzia siku tatu hadi wiki nzima kwa ajili ya kufahamiana zaidi na mke wake mtarajiwa wake na katika siku hizohufanya shughuli zote za nyumbani (kukata kuni, kuteka maji na kulima nk) hadi siku ya kuoa,” anasema Myola.
Myola anasema katika siku hizo, mume mtarajiwa huwa karibu na mchumba wake, huku wanaume waliomsindikiza nao wakiwa wameandaliwa mabinti wambao hawajaolewa kila mmoja na wake kwa ajili ya kile ambacho hudaiwa kuwa ni “kuwafariji”.
Myola ambaye shirika lake la Agape pia linajihusisha na kusomesha watoto manusura wa ndoa za utotoni, anaelezea kuwa ndoa hizo za kimila ni kikwazo cha jitihada za kukomesha ndoa za utotoni.
Kijiji cha Ilobashi Kata ya Masengwa wilayani Shinyanga, ni miongoni mwa maeneo yanayotajwa kukabiliwa na ndoa za kimila. Muelimishaji masuala ya ukatili dani ya jamii katika Kijiji hicho, Mary Lutinya anasema msimu wa mavuno kijijini humo hufanyika ndoa nyingi za kimila, ambazo ni chanzo cha ndoa za utotoni.
Kwa mujibu wa takwimu za Utafiti wa Idadi ya watu na Afya (TDHS) ya Mwaka 2015/16, mwanamke mmoja kati ya watatu nchini Tanzania huolewa kabla ya kutimiza miaka 18, kadhalika utafiti huo unaonyesha kuwapo na ongezeko la asilimia 5 la ndoa za wasichana walio katika Rika Balehe (umri wa miaka 15-19) tangu utafiti wa awali mwaka 2010.
Simulizi ya aliyewahi kushiriki ndoa za kimila.
Mmoja wa wanawake aliyewahi kushiriki kwenye ndoa ya aina hiyo ya kimila (jina limehifadhiwa) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Masengwa wilayani Shinyanga, anasimulia kuwa wanapokuwa ndani ya nyumba na wanaume hao kila mmoja anakuwa na wa kwake.
Anasema mazungumzo yao mengi huwa yanahusu mapenzi na kurubuniana kwamba wataoana na ikifika muda wa usiku ndipo hufanya ngono kwa siku zote hadi harusi itakapofungwa, kisha na wao kuondoka.
“Huwa tunatengewa nyumba moja ya kukaa na wanaume, na ikifika usiku tunalala wote kwenye hiyo nyumba na kugeuziana miguu na baadaye wengine huendelea kufanya mapenzi ili kutafuta bahati ya kuolewa,” anasema mwanamke huyo na kuongeza:
“Kimsingi ambayo hufanyika ndani ya chumba hicho ni uchafu ambao siyo rahisi kuamini, lakini kutokana na kutojitambua kipindi hicho pamoja na kulazimishwa na wazazi ili tupate bahati ya kuolewa, tulikuwa tunafanya tu hata japo mimi siziafiki ndoa hizo.”
Mwanamke huyo ana sema hivi sasa yeye ameolewa na mwanaume tofauti na yule aliyeshiriki naye ngono kwenye ndoa ya Bukwilima ambaye alikuwa mkazi wa kijiji cha Irobashi tofauti nayeye alikokuwa akiishi.
“Baada ya ile ndoa sisi tuliendelea na uhusiano na yule Mwanamke kama miezi Sita hivi, lakini baadhaye nilikuja kupata taarifa kwamba tayari ameoa mwanamke mwingine na nilipofuatilia nilibaini kwamba ni kweli. Hapo na mimi nikaona sina budi kuolewa,”anasimulia Mwanamke huyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Agape, John Myola anasema katika Ndoa za Bukwilima, Mabinti ambao huchaguliwa ni wale wenye bikira na wengi wakiwa na umri chini ya miaka 18, na wakirudi nyumbani kwao bila ya kufanya mapenzi na wanaume mama zao huwagombeza kwa madai kwamba ni mkosi katika familia.
“Baada ya Binti kurudi kutoka kwenye harusi ya kimila akisema hakufanya mapenzi na mwanaume mmojawapo, mama yake itabidi ampeleke kwa mganga wa kienyeji ili aogeshwe madawa ya kuondoa mikosi na kupewa za mvuto wa mapenzi,” ansema Myola na kuongeza;
“Mila kama hizi zilishapitwa na wakati kwahiyo zinapaswa kufutiliwa mbali kabisa maana zinavunja haki za watoto na hazi stahili kuwepo katika ulimwengu wa sasa, Serikali inapaswa kuliangalia hili, ili kulinda haki za watoto na kutimiza ndoto zao,”
Mama wa kimila, Bibi Hamida Ndaki mkazi wa Kijiji cha Nyamarogo wilayani Shinyanga, anasema yeye anapingana na ndoa za kimila (Bukwilima), sababu zina madhara ambayo huwapata mabinti wanapolala na wanaume, yakiwamo ya kupewa ujauzito kisha kukataliwa na wahusika, kukatishwa masomo na kubaki nyumbani wakilea watoto wao.
“Wanaume ambao humsindikiza kijana muoaji huwa ni watu wazima, na hukutana na vibinti vidogo vikitafuta bahati ya kuolewa, na wanapofanya mapenzi na watoto hawa wengine huwapa ujauzito, wakiwaeleza wana ujauzito wao huwakataa na baadhi hukubali,” anasema Hamida.
Anasimulia kuwa wanaume hao wanapokuwa na mabinti kwenye mji wa bibi harusi huwa kama wake zao, sababu wanawapatia huduma zote ikiwamo kuwapelekea maji ya kuoga na hata muda mwingine huoga pamoja bafuni kama hatua ya binti kutafuta bahati ya kuolewa, na harusi ya mwezao ikiisha wapo wanaobahatika kuolewa na wengine wakiachwa na ujauzito.
Anasema ndoa za namna hiyo kwa sasa zimeshapitwa na wakati, sababu haoni maana yoyote ya mabinti kwenda kujitongozesha kwa wanaume wakitafuta bahati ya kuolewa, na wengine kuishia kuharibiwa ndoto zao.
Bukwilima hufanyikaje?
Sonda Kabeshi ambaye ni mmoja wa wazee wa kimila, mkazi wa Kijiji cha Shatimba wilayani Shinyanga anasema kwa tamaduni za kabila za wasukuma, mtoto akishapevuka anapaswa kuolewa, na ndiyo maana wazazi wengi hupenda kuwaozesha mabinti zao ndoa za utotoni.
Kuhusu ndoa za Bukwilima, Kabeshi anasimulia kwamba mabinti wanapokuwa na wanaume hao nyumbani kwa mwanamke anayetarajiwa kuolewa, hupewa nyumba moja kwa ajili ya maongezi ya pamoja na pia hulala humohumo.
Anasema wakiwa katika nyumba hiyo hufanya maongezi na mabinti ambao wameandaliwa kwa ajili yao “Inapofika usiku wengine hukaa nje kwa ajili ya kupeana zamu za kufanya mapenzi, huweka ulinzi kuhakikisha kwamba hakuna mtu asiyehusika kuingia ndani ya nyumba hiyo,” anasema Kabeshi.
Anasema utamaduni wa zamani wa kuozesha mabinti ulikuwa mzuri, sababu kabla ya mwanaume kumtaka msichana lazima aende nyumbani kwao kujitambulisha na wafahamiane, akikubaliwa ndipo anarudi nyumbani kwa ajili ya kupanga taratibu za mahari na harusi.
Anasema lakini siku hizi tamaduni hizo zimekiukwa, mwanaume akimuona binti kwenye nyumba fulani, huchukua wenzake watano na kufika kwenye mji huo kujitambulisha na kueleza kuwa wanataka kuoa katika nyumba husika, bila hata ya binti kumfahamu muoaji ni nani, na wakikubaliwa wanatoa mahari, bila hata ya msichana kujua anaolewa na nani. .
“Siku chache kabla ya harusi, ndipo wanaume hao watano huenda tena nyumbani kwa mwanamke saa 4 usiku kwa ajili ya kumtambulisha muoaji kwa msichana huyo, na wakifika huko wanakuta wameandaliwa mabinti wengine idadi sawa na yao na kisha kugawana kila mtu na wa kwake,” anasema Kabeshi.
Anasema wakati wa mazungumzo yao wakiwa kila mtu na wa kwake, wanaume huanza kuwatongoza mabinti hao, huku wakiwaonyesha video za ngono kupitia simu za mkononi, ili kuwashawishi kufanya nao ngono, na hukaa huko ukweni kwa muda wa siku tatu hadi wiki wakijitambulisha, wakishinda siku zote na wasichana hao wakifanya ngono.
“Mabinti wanapokuwa na wanaume hao hua tayari wameshapewa maelekezo na wazazi wao kabla, kuwa wasigome kufanya nao mapenzi sababu huenda ikawa bahati yao kuja kuolewa na mwanaume husika hapo baadaye,”anasema Kabeshi.
Manusura wa ndoa za utotoni (jina lake limehifadhiwa) ambaye kwa sasa anaisha kituo cha Agape Manispaa ya Shinyanga, ambaye aliozeshwa kwa mahari ya Ng’ombe 12 akiwa kidato cha kwanza mwaka 2020 anasema wazazi kuendelea kukumbatia mila za kizamani kunaharibu maisha ya watoto wa kike.
Anasema yeye aliharibiwa ndoto zake za kuja kuwa mwalimu, ambapo wazazi wake waliingiwa na tamaa ya kutaka utajiri wa mifugo, ndipo wakaamua kumuozesha ndoa ya kimila tena kwa mwanaume ambaye alikuwa hamfahamu.
“Mimi niliozeshwa na wazazi wangu ndoa ya kimila nikiwa kidato cha kwanza, na siku naozeshwa wazazi wangu hawakuwepo walikuwa wameshahama Shinyanga kwenda kuishi Morogoro, na nilifunga ndoa kwao na mwanaume, lakini maisha ya ndoa yalinishinda nikatoroka na kuja Agape,” anasema binti huyo mwenye miaka 18 na kuongeza:
“Ndoa ilinishinda sikuweza kuvumilia maisha ya kulala na mwanaume kila siku, sababu kila nilipokuwa nikifanya naye tendo la ndoa nilikuwa naumia, ndipo nikaona nitoroke kuja Agape na sasa naendelea na masomo yangu hapa Shule ya Agape kwa mfumo usio rasmi na mwaka huu naingia kidato cha tatu.”
Mchungaji Edward Mashala wa Kanisa la P.A.G.T Masengwa wilayani Shinyanga, anasema kuwapo kwa ndoa za kimila ni matokeo ya jamii kupenda kukumbatia mila na desturi zilizopitwa na wakati.
“Wananchi wa maeneo ya vijijini wengi bado wanafikra za kizamani, hivyo wanapaswa kupewa elimu zaidi juu ya madhara ya kuendekeza mila zilizopitwa na wakati na madhara yake ili waishi kisasa,” anasema Mchungaji Mashala.
Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Masengwa wilayani Shinyanga Atupokile Maseta, anasema tatizo la ndoa za kimila lipo katika maeneo hayo ya vijijini, lakini limepungua siyo kama zamani kutokana na elimu ya ukatili ambayo inaendelea kutolewa.
Anasema wao kama viongozi wamekuwa wakilipigia kelele suala hilo, pamoja na kutoa elimu ya kujitambua na afya ya uzazi kwa mabinti ikiwamo kutofanya mapenzi katika umri mdogo, huku wazazi wakielimishwa madhara ya kuozesha watoto.
Afisa Maendeleo ya Jamii wilayani Shinyanga Aisha Omary, anasema ndoa za kimila nikikwazo cha vita ya ndoa za utotoni wilayani humo japo zinapungua kwa kiasi kikubwa.
“Ndoa za utotoni wilayani Shinyanga zimepungua, takwimu za mwaka jana zimefungwa ndoa tatu ambazo tuna taarifa nazo, na zenyewe tulifanikiwa kuzitibua, lakini miaka ya nyuma zilikuwa zikifungwa ndoa hadi 10 kwa mwaka na chanzo cha ndoa hizi ni mila,” anasema Aisha.
Anasema mikakati ya Serikali wilayani humo, ni kuendelea kuelimisha jamii kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali na vyombo vya habari, kuachana na masuala ya kukumbatia mila za kizamnai na kandamizi.
Kamanda wa Polisi
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi, amesema katika mikakati kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto mkoani humo zikiwamo ndoa za utotoni, hivi sasa wanatekeleza mradi wa kutoa elimu ya ukatili kwa jamii ili kuacha vitendo hivyo.
Anasema wamekuwa akitoa elimu ya ukatili ya kujitambua kwa wanafunzi shuleni, pamoja na kupaza sauti wanapoona viashilia vya kufanyiwa vitendo vya ukatili, ili hatua za haraka zichukuliwe na kuzuia madhara yasitokee.
Anasema pia wamekuwa wakitoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili kwenye nyumba za Ibada, kwa kushirikiana na vingozi wa dini ili wananchi wawe na hofu ya mungu, na kuacha kuwafanyia ukatili watoto ikiwamo kuwaozesha katika umri mdogo.
Katibu Mkuu
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii jinsia wanawake na makundi maalumu Dk. Zainab Chaula, anasema tatizo la ndoa za utotoni linasababishwa na wazazi kwa tamaa ya kutaka mali lakini watoto wao wanapenda kusoma.
“Waandishi andikeni habari zenye kuonyesha fursa, tangazeni fursa zilizopo ili wazazi wazichangamkie wapate maendeleo na kuacha kuozesha watoto ndoa za utotoni,”amesema Dk Chaula.
Mzazi Ramadhani Kabalo mkazi wa Shinyanga, anasema licha ya wananchi kuendekeza masuala ya mila kandamizi, pia umaskini umekuwa ukichangia wazazi kuozesha watoto wao ndoa za utotoni ili wapate utajiri wa mifugo.
Kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na Shirika la watoto Duniani (UNICEF) Mwaka 2012, Mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa ndoa za utotoni kwa asilimia 59 ikifuatiwa na Tabora 58 ya tatu ni mara 55.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464