KAMATI YA PETS YA KUFUATILIA RASILIMALI ZA UMMA SEKTA YA KILIMO YATAKIWA KUELIMISHA WANANCHI


Wajumbe wa kamati ya PETS ya kufuatilia rasilimali za umma sekta ya kilimo wakimsikiliza mwezeshaji kutoka chama cha watu wasioona

Suzy Luhende,Shinyanga press blog

Wajumbe wa kamati ya kufuatilia matumizi ya rasilimali za umma zilizotengwa na serikali kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za kilimo katika Mkoa wa Shinyanga Public Expenditure Trucking System (PETS)
imetakiwa kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuwa na uelewa wa kufuatilia rasilimali za kilimo zinazotolewa na serikali kuu.

Kauli hiyo imetolewa jana na mwenyekiti wa mradi wa ufuatiliaji matumizi ya rasilimali za umma zilizotengwa kwa ajili ya uboreshahaji wa huduma za kilimo Marco Nkanjiwa, kwenye mafunzo ya kamati hiyo yaliyofanyika kata ya Tinde halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, ambayo yamefadhiliwa na shirika la The Foundation for Civil Society na kusimamiwa na viongozi wa Chama Cha watu wasioona Mkoa wa Shinyanga, (TLB)

Mwenyekiti wa mradi huo Nkanjiwa amewataka wajumbe wa kamati ya PETS wakatoe elimu kwa wananchi ili wananchi hao waweze kufuatilia rasilimali za umma kwani ni haki yao kujua katika kata imetolewa bajeti ya kilimo kiasi gani na imewafikia wakulima wote na wanapatiwa huduma na maafisa ugavi wa serikali inavyotakiwa ili waweze kuwa na kilimo chenye tija.

"Tumeamua kuanzisha mradi huu na kuunda kamati ya PETS ili kuhakikisha wakulima wetu wanapata elimu ya kutosha ya kuweza kufuatilia juu ya rasilimali za kilimo, hivyo ni vizuri mbinu mlizopewa kwenye mafunzo haya ya siku tatu mkazitumie ipasavyo ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kuweza kufuatilia rasilimali za kilimo na kuweza kulima kwa tija,"alisema Nkanjiwa.

Aidha mwezeshaji wa mafunzo hayo Dickson Maganga alisema wananchi wengi hawajui rasilimali za kilimo kuwa zinatolewa kwa ajili yao, hivyo wajumbe ambao walichaguliwa na wananchi wenyewe kwa ajili ya kuwa kwenye kamati ya PETS wakawape elimu waliyoipata, ili kila mwananchi aweze kuwa na uelewa wa kufuatilia kwamba serikali imetoa bajeti ya kilimo kiasi hiki je kwa kata ya Didia ama kata ya Tinde imetoa kiasi gani.

"Tunachokifanya hapa ni kuwatengenezea uendelevu ili hata mradi huu ukiisha kamati hii iendelee kufanya kazi na wananchi wawe na uelewa wajue eneo lenye changamoto wafuate zile hatua za ufuatiliaji tulizowafundisha, hivyo tunasisitiza washike haya tunayowafundisha, kwani ni faida yao na ya wananchi walioko kwenye kata zao,"alisema Maganga.

Aidha Mwakilishi wa afisa kilimo wa halmashauri ya Shinyanga Dickson Felician ambaye pia ni afisa kilimo wa kata ya Usanda, amesema malengo ya mafunzo hayo ni kuboresha utoaji wa huduma mbalimbali kwenye maeneo na kufuatilia matumizi ya rasilimali ya umma kwa mtazamo wa kijinsia.

"Lengo la mafunzo haya ni kuhakikisha rasilimali zinazotolewa na serikali zinatumika kwa lengo husika na kwa samani husika ili kuhakikisha utendaji wa serikali pamoja na mamlaka yake zinawatendea haki wananchi wake, mfano mipango iliyowekwa inaendana na bajeti iliyopangwa,"alisema Felician

"Na kujua kwamba licha ya serikali kutoa bajeti ni mchangamoto gani bado inawakabili wakulima ili waweze kutatuliwa waachane na kilimo kisichokuwa cha tija wabadilike walime shamba dogo walime kwa kufuata ushauri wa afisa kilimo kulingana na mabadiliko ya tabia nchi na walime kilimo chenye tija,"aliongeza Felician.

Feliciani pia alisisitiza kamati ya PETS inapotoa elimu iwaelimishe wakulima wabadilike waachane na kilimo cha kupanda mbegu kwa holela, badala yake wapande mbegu kwa hatua zinazotakiwa, kwani serikali sasa imeboresha imetoa pikipiki kwa kila afisa kilimo wa kata, hivyo wawatumie hao maafisa kilimo ili waweze kupata mazao ya kutosha na wajikomboe kiuchumi kupitia kilimo.

Baadhi ya wajumbe wa PETS akiwemo Salehe Dotto amesema mradi huo umewasaidia kuwapa elimu, kwani walikuwa hawajui jinsi ya kufuatilia rasilimali za umma, lakini kwa sasa wamepata mafunzo hivyo wataenda kuhoji na kuelimisha wananchi wengine ambao hawana elimu, pia watalima kilimo chenye tija.

Jumla ya halmashauri tatu za mkoa wa Shinyanya zimefaidika na mafunzo hayo zikiwa na kata sita ambazo ni manispaa ya Kahama kata ya Nyandekwa, halmashauri ya Ushetu kata ya Igunda, Kinapula na Bukomela, katika halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ni kata ya Didia na kata ya Tinde ambapo jumla ya Wajumbe wa PETS 48 wamefaidika na mafunzo hayo ambao wanatakiwa kwenda kuelimisha jamii juu ya ufuatiliaji wa rasilimali za umma.
Wajumbe wa kamati ya PETS wakiwa kwenye majadiliano katika kata ya Tinde
Wajumbe wa kamati ya PETS wakiwa kwenye majadiliano katika kata ya Tinde
Mjumbe wa kamati ya PETS akiwasilisha mada walizokuwa wanazijadili
Muwezeshaji kutoka kutoka chama cha watu wasioona mkoa wa Shinyanga Dickson Maganga akiwezesha
Wajumbe wa kamati ya PETS wakiwa kwenye majadiliano katika kata ya Tinde
Wajumbe wa kamati ya PETS ya kufuatilia rasilimali za umma sekta ya kilimo wakimsikiliza mwezeshaji kutoka chama cha watu wasioona
Mjumbe wa kamati ya PETS akiwasilisha mada walizokuwa wanazijadili
Muwezeshaji kutoka kutoka chama cha watu wasioona mkoa wa Shinyanga Dickson Maganga akiwezesha

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464