KILIMANJARO TUPO TAYARI KUACHANA NA MIRUNGI, SERIKALI ITUSAIDIE ELIMU MAZAO MBADALA – WANANCHI


Na DCEA – Kilimanjaro

Wananchi waishio katika vijiji wa Rikweni, Heikondi, Tae na Mahande vilivyopo Kata ya Same Mkoani Kilimanjaro wamesema wapo tayari kuachana na kilimo cha mirungi.


Hivyo, wameiomba Serikali kuwapelekea wataalamu wa kuwapa mafunzo juu ya kilimo cha mazao mengine mbadala.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari mkoani hapa wamesema ardhi yao ina rutuba na kwamba wapo tayari kuachana kabisa na zao hilo haramu.

Ndani ya vijiji hivyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Dola imeanza Oparesheni maalum ‘Tokomeza Mirungi’.


“Eneo letu asilimia kubwa ni wakulima wa kilimo hicho na wamekifanya huu mti kama wa biashara unaowaingizia kipato,” amesema Mkazi wa Kijiji cha Rikweni, Mchungaji Elisante Senkondo.

Ameishukuru Serikali kwenda kukemea kilimo hicho na kuongeza “Maana na yenyewe ni chombo cha Mungu wakati uasi unapokuwa umekithiri.

“Mungu anakitumia kama chombo kinachomkemea anayefanya uasi wa aina yoyote, siyo tu mirungi, kama mauaji na kadhalilka.

“Niiombe Serikali itupe nafasi tukae na watu wetu katika makanisa tuwashauri kwa nguvu zaidi ili kwa hiyari yao wenyewe waweze kukubali kutokomeza hizi dawa za kulevya",amesema.


Naye, Mwalimu Janeth Sarambo wa Shule ya Msingi Rikweni amesema wananchi wameathirika mno kwa kilimo hicho kijijini humo.

“Mwanzo walikuwa hawajagundua ni dawa za kulevya sasa wamegundua,, tunaiomba Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ituletee wataalamu wa kilimo, wananchi wapewe elimu kuhusu kilimo cha mazao mengine.

Amesema yapo mazao mengine ya chakula na biashara ambayo yanakubali katika kijiji hicho kwani ardhi hiyo ina rutuba.


“Tunaotesha migomba, mahindi, maharagwe ni mazao machache tu hayakubali huku, tunaomba Serikali itusaidie ili wananchi wasipate mahangaiko, walime mazao mazuri wapate biashara na fedha ili wasihangaike na mirungi.

Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Tae, Japhet Msengi ameongeza “Tumekuwa tukipambana kwa ajili ya kusaidia jamii inayotuzunguka juu ya athari ya kilimo hiki, kimekuwa cha muda mrefu kwenye kata hii.

“Tulishapokea barua kwa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kwamba tuungane na viongozi wengine kutokomeza kwa njia ya kuwapa elimu ili ufahamu wa wananchi ubadilike.

Amebainisha “Tulifanya hivyo kwa muda usiopungua miaka sita tangu tuanze hizi oparesheni, baadhi walipunguza na wengine waliendelea kwa madai kwamba kinawanufaisha na kupata pesa.

“Wanadai si kwa ajili ya matumizi bali kuwapatia kipato, tulijaribu ku-organize na taasisi nyingine za kilimo ili kuwasaidia zao mbadala waondokane nacho.

Amesema ni kilimo ambacho hakiipatii mapato kata hiyo wala Serikali kwani si biashara halali.
“Huwezi kumkatia mtu wa mirungi kwa sababu si biashara halali, wakati mwingine tunahangaika kupata mapato kwa kukata risiti na Serikali iweze kupata kodi,” amesema.

Naye, Diwani wa Kata ya Tae Samwel Mbwambo amesema Serikali ina nia njema na wananchi wa Kata hiyo, lengo lake ni kusababisha wananchi waachane na kilimo hicho kinachosababisha wapate madhara makubwa.

“Lakini pia jamii kupoteza mwelekeo, ilani ya CCM 2025 ilishaandika utokomezaji wa dawa za kulevya ni sehemu ya wajibu wa Serikali.

Amewasihi wananchi wa Kata hiyo wasiendelee na kilimo hicho kitawaletea madhara makubwa.

“Mtafungwa kifungo ambacho ni kikubwa na jamii itapoteza nguvu kazi, vijana wakienda kwenye kifungo itakuwa imeisha.

“Niwaombe tuendelee na vilimo vingine ambavyo vitaweza kutusaidia katika uchumi wa familia zenu na kuacha na hili ambalo ni tatizo kubwa katika jamii hii.

Ametoa rai kwa wananchi hao pia kuhudhuria mikutano ya uelimishaji itakayofanyika ili wapate uelewa utakaowasaidia kubadilika.

“Niwaombe Serikali, wananchi hawa wametegemea kilimo hiki kwa sababu hawajapata elimu ya kilimo kingine, watusaidia ili tupate mabadiliko makubwa na kizazi kitakachokuwa kizuri.

“Itusaidie kutoka kilimo cha mirungi na kwenda kwenye kilimo kingine, kabichi, nyanya, vitunguu vinakubali vizuri.

“Mazao ya kimkakati kama parachichi inayouzwa bei kubwa nchi za nje, kwanini tusihamie kwenye kilimo hicho.

“Nawasihi tubadilike twende kwenye kilimo kizuri ambacho hakisababishi watu kukimbia nyumba, kukimbia opareshe, tuachane na hili ili tuwe wananchi wema,” ametoa rai.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464