MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewakaribisha wanachama na wadau kutembelea banda namba 13 wakati huu wa Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwenye viwanja vya Julius Nyerere maarufu Sabasaba, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Maonesho hayo yameanza Juni 28 na yatafikia kilele Julai 13, 2023 huku yakiwa yamebeba kaulia mbiu isemayo "Tanzania Mahali Salama kwa Biashara na Uwekezaji".
Akizungumzia Huduma ambazo mwanachama au mdau wa NSSF atazipata afikapo kwenye banda hilo, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma NSSF, Bi. Lulu Mengele amesema, ni pamoja na kupata Elimu ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Rasmi na Sekta Isiyo Rasmi.
Pia amesema Mwanachama akifika kwenye banda hilo ataweza kupata taarifa za michango yake ya kila mwezi lakini pia taarifa za uwekezaji.
"Kuhusu taarifa za michango hii itamsaidi kujua kama mwajiri wake anatekeleza wajibu wake wa kuwasilisha michango kwa wakati au la na kama kuna changamoto zozote timu ya watumishi wa NSSF iko tayari kuwahudumia", amefafanua Bi. Lulu Mengele.
Amesema Huduma nyingine ambayo Mwanachama atapata ni pamoja na kupata taarifa za Mafao yatolewayo na Mfuko.
Lakini pia kwa wananchi watakaotembelea banda hilo watapata taarifa za fursa za kujipatia viwanja na nyumba.
"Kama mjuavyo NSSF tunauza viwanja, tunauza nyumba tungependa kuwakaribisha wanachama wetu na wadau mbalimbali kutembela banda letu ili kuchangamkia fursa hizo”, amesema.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464