Na Elias Gamaya,Shinyanga Press Club Blog
kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga ACP Janeth Magomi amelitaka Jeshi la jadi maarufu Sungusungu kutoka Vitongoji viwili vya Imenya na Igomelo Kata ya Itwangi kuzingatia maadili ya kazi yao ikiwemo kujiepusha na vitendo vya kihalifu.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya mwezi mmoja ya vijana 182 ambao wameingia katika Jeshi la jadi Sungusungu rasmi ili kusaidia kudhibiti wahalifu,Kamanda Magomi amewasihi kuzingatia sheria na kuacha kujichukulia sheria mkononi badala yake wawafikishe polisi.
"Jeshi la jadi lipo kisheria kupitia sheria ya Mgambo na linatambulika kisheria na lilianza kupata umaarufu, sisi Jeshi la Polisi hatutoshi kama polisi mmoja anatakiwa kulinda raia 450 tu katika suala zima la ulinzi na usalama lakini kinachotokea sasa kutokana na uchache wetu askari mmoja analinda raia 1700”amesema Kamanda Magomi
Kamanda Magomi amesema Mkoa wa Shinyanga bado unakabiliwa na mauaji,ndoa za utotoni, mimba kwa wanafunzi,ubakaji,kulawiti na baadhi ya watu kujihusisha na mapenzi ya ndoa za jinsia moja mambo ambayo yanatakiwa kukemewa katika jamii ili kukomesha vitendo hivyo.
Awali akifafanua historia ya Jeshi la Jadi Mwelimishaji ambaye pia ni Mhasibu wa Tarafa ya Itwangi, Philipo Malongo amesema kabla ya kuitwa jeshi la jadi lilikuwa linaitwa shilika la kurudisha mali za watu ikiwemo mifugo kutokana na kukithiri kwa matukio ya wezi wa mifugo kwa kipindi cha mwaka 1981.
Amesema malengo na madhumuni ya Jeshi hilo ni kuwaelimisha vijana ili waielewe sungusungu,kuawezesha vijana kubadilika na kuwafundisha nidhamu vijana ambapo mafunzo hayo hufanyika kila baada ya miaka mitano.
“Sungusungu haikuwekwa kwa ajili ya kuwatese vijana bali ilikuka kwa nia ya kuwafundisha kuwa na nidhamu na kuwatengeneza kuendana na kanuni na sheria za nchi yetu”Amesema Malongo
Nao baadhi ya sungusungu wa jeshi hilo wamesema mmafunzo hayo yatawasaidia kukabiliana na wahalifu,pia kusaidia kupunguza vitendo vya kihalifu ili hatua za haraka zichukuliwe kukabiliana na matukio hayo na kuyakomesha.