KITUO CHA TAARIFA NA MAARIFA KILOLELI CHACHANGIA KUFANIKISHA UJENZI WA NYUMBA YA WALIMU MUGUDA


Nyumba mpya (kulia) nyumba ya zamani (kushoto)

Na Kareny Masasy na Kadama Malunde - Kishapu
Ushirikiano mkubwa baina ya Serikali na wananchi wa kijiji cha Muguda kata ya Kiloleli wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga umetajwa kusaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa nyumba za walimu katika shule ya Msingi Muguda.


Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea shule hiyo, Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Muguda Simeo Kamuli amesema shule ina jumla ya walimu sababu ambao ujenzi wa  nyumba ya walimu (2 in 1) umesaidia kupunguza changamoto ya uhaba nyumba za walimu  kufuatia ushirikiano mzuri baina ya jamii na serikali.

"Kukamilika kwa ujenzi wa nyumba hii kunaleta ahueni na motisha kwa walimu, kwani nyumba ya awali ya udongo haikuwa bora. Tunawashukuru wananchi na serikali kwa ujenzi huu",amesema Kamuli. 
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Muguda Simeo Kamuli.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Muguda Leonard Ngayalina amesema  nyumba hiyo imejengwa kwa nguvu za wananchi hadi hatua ya renta na serikali kuu ikatoa shilingi Milioni 25 kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo.


"Walikuja Kituo cha Taarifa na Maarifa Kiloleli kinachosimamiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wakatoa hamasa kuhusu ujenzi wa nyumba za walimu, tukawa na vikao vya ndani kwa ajili ya taratibu zote kuhamasisha wananchi wachangie, baadae tukafanya mikutano ya hadhara kuelezea na wananchi wakakubalina, baada ya wananchi wakaanza kuchangia, zikapatikana zaidi ya  shilingi milioni 7  kutokana na michango kutoka kwa wakazi 2519 na kaya 298 katika kijiji.

Baada ya  pesa kupatikana wanananchi wakaomba usaidizi kutoka Halmashauri ya wilaya ya Kishapu iwape ramani ya jengo, wakaanzisha ujenzi mpaka usawa unaostahili kwenye renta (boma), tukakaa na kutuma maombi Halmashauri isaidie kumalizia ujenzi, tukapata fungu kutoka serikali kuu shilingi milioni 25, halmashauri ikawa msimamizi mkuu mpaka jengo lilipokamilika",ameeleza Ngayalina .

Nyumba mpya ya Walimu.

Amesema tayari ujenzi wa jengo hilo upande wa mbele umekamilika ambapo walimu wawili wameanza kuishi, ujenzi upande wa nyuma kuna sehemu haijakamilika hivyo ujenzi ukikamilika walimu wengine wawili wataanza kuishi kwenye nyumba hiyo na kufanya idadi ya walimu waliopata nyumba kuwa wanne.

"Bado tuna upungufu wa nyumba za walimu, licha ya kukamilika kwa ujenzi huu,  tutaendelea kuhamasisha jamii kuchangia shughuli za maendeleo ili kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa",ameongeza Ngayalina.

Mwenyekiti wa kijiji cha Muguda Lakeshi Malendeja amesema  mafanikio hayo yametokana na jamii kupata uelewa wa kuchangia maendeleo bila kushurutishwa baada ya kuhamasishwa na kituo cha taarifa na maarifa na serikali kutoa ushirikiano ili walimu waishi katika mazingira bora.
Mwenyekiti wa kijiji cha Muguda Lakeshi Malendeja.

Afisa Mtendaji wa kata ya Kiloleli Donald Muhangirwa amewashukuru wananchi wananchi kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

"Wananchi wameshiriki nguvu wakajenga hadi boma, serikali ikaja kukamilisha ujenzi. TGNP kupitia Kituo cha Taarifa na maarifa walikuwa ni sehemu ya kuhamasisha ujenzi wa nyumba hii, kwa kweli wako vizuri katika kuhamasisha jamii kuleta maendeleo",amesema Muhangirwa.
Nyumba ya zamani.

Katibu Msaidizi wa kituo cha taarifa na maarifa Kiloleli, Zacharia Pimbi amesema amesema walitembelea kijiji cha Muguda kuangalia sekta ya elimu wakabaini kuna changamoto ya nyumba za kudumu kwa walimu, wakapeleka kwa viongozi wa kijiji na kuitisha mkutano wa hadhara na wananchi wakakubaliana walimu wajengewe nyumba bora ndipo michango ikaanza kutolewa kisha serikali ikaunga mkono na kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha jengo.


"Sisi kama Kituo cha taarifa na maarifa, tulipofika katika kijiji hiki tulibaini changamoto ya nyumba za walimu, walimu waliibua changamoto hii ya ukosefu wa nyumba za walimu, 
mkutano wa hadhara kujadili namna ya kutatua changamoto ukafanyika, jamii ikaitikia kutoa michango, ujenzi ulipofikia hatua ya renta serikali ikatoa shilingi Milioni 25. Na sasa nyumba moja kwa familia mbili imekamilika, ujenzi wa nyumba ya pili (sehemu ya nyuma) unaendelea",amesema Pimbi.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464