Na: Mwandishi Wetu - MANYARA
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amemuagiza mkandarasi anayejenga uwanja wa mpira wa Kwaraa kumaliza kwa wakati ili kutumika katika kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru.
Mhe. Katambi ametoa maelekezo hayo Agosti 11,2023 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya uwanja huo kuelekea kilele cha mbio hizo za zitakazohitimishwa Oktoba 14, 2023.
Aidha, amesema kuwa ujenzi wa uwanja huo ni mpango wa Serikali katika kuwasongezea karibu viwanja vya michezo wananchi wa Mkoa wa Manyara lakini pia utakautumika kwenye kilele hicho.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Lazaro Twage amemhakikishia Naibu Waziri kuwa kuwa watamsimamia mkandarasi ili ujenzi huo ukamilike ndani ya muda uliopangwa.
Katika ziara hiyo, Mhe. Katambi amekagua pia Kanisa Katoliki Parokia ya Roho Mtakatifu Ngarenaro -Manyara itakapo fanyika ibada ya Baba wa Taifa, uwanja wa stendi ya zamani itakapofanyika wiki ya vijana na kukagua maendeleo ya vijana wa halaiki katika Shule ya Sekondari ya kutwa ya Babati.