JAMII YALIA NA UGONJWA WA SIKOSELI KWA WATOTO


 Waziri wa Afya Ummy Mwalimu.

 Na  Kareny  Masasy,

SELIMUNDU  ( sikoseli ) ni ugonjwa  wa kurithi ambao hutokea  baada ya mwili wa binadamu kuwa na upungufu katika  umbile  la seli hai nyekundu za damu.

Wataalamu   wa  afya wanabainisha  mgonjwa mwenye upungufu huo anakuwa na  sikoseli haonyeshi dalili yeyote mpaka  mtoto afikishe miezi minne ya umri tangu kuzaliwa na huanza na dalili mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika mwili wake.

Baadhi    ya wazazi  kutoka kijiji cha Nyasamba wilayani Kishapu  mkoani Shinyanga wanaeleza  wanavyoteseka na watoto  wenye ugonjwa wa sikoseli  ambao unawafanya kudumaa kutokana na hali duni ya kipato ndani ya familia namna yakuukabilia ugonjwa huo.

Seni  Mwinamila  mkazi wa kijiji cha Nyasamba  kata ya Bubiki halmashauri ya wilaya Kishapu anasema   ugonjwa wa sikoseli umefanya  watoto wake wawili wafariki na mwingine mwenye miaka mitatu anaendelea kusumbuka na ugonjwa huo.

Mwinamila anasema  alikuwa akimpeleka  kwenye Zahanati   lakini alipatiwa rufaa ya  kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa  na aligundua kuwa mwanaye ni  mgonjwa wa sikoseli   akashauriwa na daktari  kila Mwisho wa mwezi ampeleke kliniki na sasa anaendelea na matibabu.

Mwinamila anasema   changamoto ya kulea mtoto mwenye sikoseli  ni kazi ngumu kutokana na  hali duni ya maisha maana dalili zake muda mwingine zinakuja kwa kushtukiza na pesa ya usafiri ni shida,

Mwinamila anasema  mtoto wake mwenye umri wa miaka mitatu amekuwa akiishiwa  damu mara kwa mara  nakuongezewa wakati mwingine uzito  wa mwili kupungua na kutokwa manjano.

 “Ugonjwa huu unahitaji mtu awe na pesa muda wote maana dalili zinakuja kwa kushtukiza pia chakula bora apate kwa kawaida ninampatia  matunda na mboga za majani ili asipungukiwe damu lakini tatizo linakuwa palepale”anasema Mwinamila.

Shanila Fale  mkazi wa kijiji cha Nyasamba anasema  amebahatika kupata watoto nane wawili walifariki  kwa nyakati tofauti  wakiwa  na umri chini ya miaka mitano  kwa ugonjwa wa sikoseli na mmoja mwenye  miaka mitatu   sasa  naye anatatizo la sikoseli ameonekana kudumaa.

 “Nimekuwa nikienda hospitalini mara kwa mara  wanampatia dawa lakini tatizo bado linakuwa la kuishiwa damu anaiomba serikali isaidie watoto wenye matatizo kama haya  wapate msaada wa chakula chenye  lishe”anasema  Fale.

Mtendaji wa kijiji cha Nyasamba  Speratus  Rwehumbiza anasema   watoto waliobainika  na sikoseli  wanatambulika katika ofisi yake ila wazazi wengine wamekuwa wakionekana kushindwa  kumudu hali za watoto wao sababu ya kifedha huja kuomba msaada na wengine kukimbilia kwa waganga wa kienyeji..

Daktari Bingwa wa  magonjwa ya watoto  hospitali ya rufaa ya mkoa  wa Shinyanga Marwa Ngutuyi anasema   sikoseli imekuwa ni tatizo kwa watoto ambao imewafanya kupungukiwa na damu na kulazwa mara kwa mara.

Dkt  Ngutuyi anasema   ugonjwa huo unatokana na vinasaba yaani kurithi na kanda ya ziwa imekuwa ikiongoza kwa watoto wenye  sikoseli ikiwemo mkoa wa Shinyanga huu  ambapo inalazimika kuanzisha kliniki ya watoto hao kwaajili ya wazazi kuwapa ushauri ili kupunguza tatizo la kulazwa kila mara.

Dkt  Ngutuyi  anasema  kuna watoto zaidi ya 100 wanaohudhuria kliniki mpaka sasa ikiwa ugonjwa  wa sikoseli una sehemu mbili kuna watoto wanao onyesha kuwa na  dalili na  wengine  wanakuwa na chembechembe au vimelea.

“Ugonjwa wa sikoseli  unapona kama ukifuata utaratibu unaoelekezwa na wataalamu ila wanapokuwa wakubwa bado kuna mifupa itakayo kuwa imelika nakuonekama akiwa anatembea  kuchechemea na mwili kuwa dhaifu”anasema  dkt  Ngutuyi.

. Dkt  Ngutuyi  anasema mtoto kuanzia umri wa miaka o  hadi mitano  akiugua muda mrefu bila kupata matibabu ni hatari kwani hata ubongo wake unakuwa haufanyi kazi vizuri ni vyema wazazi wakawa wanachukua tahadhari mapema pindi wanavyoona dalili zozote mbaya kwa watoto wao.

Dkt Ngutuyi anasema  ugonjwa wa sikoseli  upo zaidi maeneo ya kanda ya ziwa kwani  unatokana na vinasaba  pia  ugonjwa huu utakuta mtoto analazwa mara 15 kwa mwaka na  afya yake inaonekana kuwa dhaifu.

Dk Ngutuyi  anasema serikali kupitia wizara ya afya tayari imeleta vifaa vya utambuzi wa selimundu kwa watoto pindi wanapozaliwa  lengo la kupambana na ugonjwa huo.

Dkt  Emmanuela Ambrose ambaye ni daktari bingwa wa watoto - kitengo cha damu Bugando  jijini Mwanza  anasema  tatizo  la ugonjwa wa sikoseli kuonekana kubwa  jamii imekosa uelewa.

 dkt  Ambrose  anasema  katika tafiti za hivi karibuni zinaonyesha katika kanda ya ziwa asilimia ishirini na moja (21%) ya watu wanarithi chembechembe (vimelea) za sikoseli .

 Dkt   Ambrose  anasema  tabia ya wazazi  kuwaficha watoto wenye matatizo  ya sikoseli wakihusisha tatizo hilo  na imani za kishirikina ambayo inasababisha kuwaleta watoto hospitali wakiwa wamechelewa na kusababisha matatizo makubwa.

Dkt Ambrose  anasema  ugonjwa huu hurithiwa kutoka kwa wazazi wote yaani baba na mama kitaalamu wanaita carriers.. mama na baba wanaweza kua hawana dalili yeyote  lakini wamebebea vimelea vya ugonjwa huo kwenye damu zao na kumzaa mtoto mgonjwa.

Kwa mujibu wa shirikia la utangazaji la Uingereza  (BBC) kupitia taarifa waliyoripoti mwaka 2015  wanaeleza kuwa  Tanzania ni nchi ya  tano kuwa na watu wenye ugonjwa wa sikoseli.

Ambapo  wameleza utafiti unaonyesha  kwa kila mwaka nchini Tanzania  takribani  watoto  1100 wanazaliwa wakiwa na sikoseli na moja ya sababu  ya ongezeko hilo ni uelewa mdogo wa jamii juu ya ugonjwa  huo unaosababisha seli za damu kuwa katika umbo la  nusu duara.

Pia Taasisi  ya sikoseli nchini Tanzania mwaka 2014   nayo ilieleza  kuwa  watoto 800 hadi 1100 huzaliwa na sikoseli kila mwaka nchini Tanzania  ikiwa ni nchi  ya nne duniani kwa wagonjwa wenye sikoseli.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewataka vijana nchini kupima vinasaba na wenza wao kabla ya kuoana na kupata watoto ama kuanzisha familia  ili kuvunja mnyororo wa maambukizi ya ugonjwa wa Selimundu,

Sheria ya mtoto ya mwaka 2009   namba 21  inaeleza wazazi na walezi wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba watoto wanapelekwa kwenye chanjo, wanapatiwa huduma za afya na kupewa miongozo  au ushauri katika  matunzo.

Sera ya afya ya mwaka 2007   nchini Tanzania  linaeleza  kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaimarisha utoaji wa elimu ya afya ili kuhamasisha na kumwezesha  kila mtu kujenga tabia inayozingatia  kanuni za afya  na maisha bora.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464