MAAFISA KILIMO WATAKIWA KUIELIMISHA JAMII KUONDOKANA NA MFUMO DUME WA KUMILIKI ARDHI WANAUME PEKEE BALI UWEPO USAWA

Chama cha watu wasioona mkoa wa Shinyanga wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa serikali na wanasiasa baada ya kumaliza kikao chao.

Suzy Luhende, Shinyanga press

Maafisa kilimo wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wametakiwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya wanawake kumiliki ardhi kwani bado dhana ya mfumo dume inaendelea katika jamii, hakuna usawa wa kumiliki ardhi mwanamke na mwanaume.

Licha ya kuwa na mfumo dume pia chama cha wasioona mkoa wa Shinyanga wameeleza changamoto za sekta ya kilimo zilizopo kwa wananchi wa halmashsuri ya Shinyanga.

Hayo yameelezwa jana na mwenyekiti wa chama cha watu wasioona Mkoa wa Shinyanga(TLB) Marco Nkanjiwa kwenye kikao cha viongozi wa serikali na wanasiasa kilichofanyika kata ya Tinde halmashauri ya Shinyanga kilichoandaliwa na viongozi wa Chama Cha watu wasioona Mkoa wa Shinyanga kwa ufadhili wa shirika la The Foundation for Civil Society.

Nkanjiwa alisema wanawake wengi hawamiliki ardhi hasa katika maeneo ya vijijini wanaume ndio wanamiliki, hali ambayo inapotokea mwanaume ametangulia, amepoteza maisha mwanamke kukosa haki yake na ardhi kuchukuliwa na ndugu wa mwanaume, hivyo ni vizuri maafisa kilimo wakati wakitimiza majukumu yao wakatoa elimu ili jamii iweze kubadilika na kuondokana na mfumo dume uliotawala.

"Elimu itolewe kwa jamii ili uwepo usawa kati ya wanawake na wanaume kwani bado mfumo dume upo tunahitaji ushirikiano wa mme na mke sio kumiliki mwanaume tu ardhi yote, hivyo niwaombe maafisa kilimo muendelee kushawishi wanawake wamiliki ardhi na mali za familia,"alisema Nkanjiwa.

Aidha mwezeshaji kutoka Chama Cha watu wasioona Mkoa wa Shinyanga Dickson Maganga alisema wakiwa wanaendelea na mradi wao wa ufuatiliaji matumizi ya rasilimali za umma zilizotengwa kwa ajili ya uboreshahaji wa huduma za kilimo, wamekutana na changamoto mbalmbali zikiwemo za upatikanaji wa mbolea ambazo haziletwi kwa wakati katika maeneo husika.

Pia alizitaja changamoto nyingine kuwa wakulima kukosa namba za kuchukulia mbolea,vifungashio vya mbolea kuletwa vya kilo 50 peke yake ambapo wakulima wengine wanakuwa na uwezo mdogo wa kifedha, hivyo kushindwa kununua, angalau vingeletwa vifungashio vya kilo 25 ili na wenye uwezo mdogo waweze kununua.

Changamoto nyingine ni upungufu wa masoko ya uhakika, mkulima kukosa mashamba darasa, kwani baadhi ya wakulima hawatumii mbolea za viwandani kwa madai kuwa inaharibu ardhi.

"Tuombe changamoto hizi zishughulikiwe ili wakulima waweze kulima kilimo chenye tija na kuondokana na hali ya kimasikini inayosababishwa na kilimo kisicho na tija,"alisema Maganga.

Diwani wa kata ya Didia Jafari Kanola amesema baadhi ya maafisa kilimo wakienda kwenye vikao baadhi yao kutokuwa waaminifu wanachanganya mbolea na zisizokuwa mbolea ili wapate faida kubwa hili lishughulikiwe, na mwaka huu ziletwe mbegu na mbolea kwa wakati ili mkulima afanye shughuli zake za kilimo kwa wakati.

Diwani viti maalumu Wilaya ya Shinyanga Helena Daudi amesema maafisa kilimo wanatakiwa kuwatembelea wakulima na kuwashauri walime mapema kwa kutumia mvua ya kwanza ili wapate mazao ya kutosha kutokana na mabadiliko ya tabia nchi 

Baadhi ya wananchi wa kata ya Tinde akiwemo Mahona Ongala alisema wakulima wengi hawatumii mbolea ya viwandani, lakini wakipewa elimu ya kutumia mbolea hiyo watatumia kwani wengine wanaweza kutumia nyingi zaidi au pungufu zaidi ambayo itaufanya mmea usiendelee kuwa na afya,hali ambayo inamfanya mkulima asitumie tena mbolea hiyo kwa kuiona haifai.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Shinyanga David Rwazo ambaye ni afisa utumishi alisema amezisikia changamoto zilizotajwa watazishughulikia, hasa hilo la pembejeo, lakini wakulima wanahitaji kupewa elimu ijapokuwa wenyewe wakulima hawafuatilii, hivyo wanatakiwa kubadilika ili waweze kupata mazao ya kutosha.

"Kweli wakulima wengi wanapuuzia kutumia mbolea kwa kujua ardhi yao itaharibika lakini sio,tumeliweka kwenye bajeti ili kuchukua wakulima wachache wapelekwe kujionea wakulima wengine waliofanikiwa kwa kutumia mbolea ya viwandani ambao wakirudi watakuja kuanzisha mashamba darasa ili na wengine wabadilike,"alisema Rwazo.

"Kuhusiana na suala la kucheleweshewa mbegu tumelisikia tayari utekelezaji umefanyika wakala mkuu ameshaanza kuwasiliana na wenye maduka madogo ngazi ya kata ili yawe yanapokea mbegu na mbolea, hivyo mwenyekiti tunakushukuru sana kwa kuwa utekelezaji unafanyika mnafanya kazi nzuri sana tunaziona na wananchi wameanza kubadilika wanafuatilia ,"alisema na kuwapongeza.Rwazo.

Naye afisa kilimo wa halmashauri ya Shinyanga Robart Lubebe alisema kweli changamoto ya mbolea kutofikishiwa karibu na maeneo ya wakulima ilikuwepo mpaka unafungwa msimu, lakini wamelipeleka serikali kuu na tayari utekelezaji umeshaanza wa kuwafikishia mbegu na mbolea wakulima na changamoto ya kutumia mbolea wakulima watapewa elimu ya matumizi ya mbolea hiyo ili waweze kulima kimo chenye tija badala ya kupata mazao machache wapate mengi.
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Shinyanga David Rwazo akizungumza kwenye kikao hicho
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Shinyanga David Rwazo akizungumza kwenye kikao hicho
Mwenyekiti wa chama cha watu wasioona Mkoa wa Shinyanga Marco Nkanjiwa akizungumza kwenye kikao hicho
Mwezeshaji kutoka chama cha watu wasioona Mkoa wa Shinyanga Dickson Maganga
Diwani wa kata ya Tinde Jafari Kanola akizungumza kwenye kikao hicho 
Diwani viti maalumu wa wilaya ya Shinyanga akizungumza 
Afisa kilimo wa halmashauri ya Shinyanga Robart Lubebe akijibu jambo 
Afisa ushirika wa halmashauri ya Shinyanga Stephano Shadrack akifafanua jambo
Wajumbe wa kikao hicho wakiendelea na kikao 
Wajumbe wa kikao hicho wakiendelea na kikao 
Wajumbe wa kikao hicho wakiendelea na kikao 
Wajumbe wa kikao hicho wakiendelea na kikao 
Watu wasioona na viongozi wakiwa wanafurahia jambo baada ya kuona kazi yao ya ufuatiliaji wa rasilimali za umma umeanza kutekelezwa na serikali.
Chama cha watu wasioona mkoa wa Shinyanga wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa serikali na wanasiasa baada ya kumaliza kikao chao.






































































Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464