MADIWANI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUSHIRIKIANA KATIKA KUSIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO

Mwenyekiti wa halmashauri ya Kishapu William Jijimya akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani 

Suzy Luhende, Shinyanga press Blog

Madiwani wa halmashauri ya Kishapu Mkoani Shinyanga wametakiwa kufanya kazi kwa kushirikiana na wataalamu katika kusimamia miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayotekelezwa katika halmashauri hiyo, ikiwa ni pamoja na kusimamia watoto kupewa fursa ya kujiunga na kidato cha tano na sita.

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Joseph Mkude wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo, ambapo katika baraza hilo ulifanyika pia uchaguzi wa makamu mwenyekiti na kamati zake.

"Leo mmefanya uchaguzi wa makamu mwenyekiti na kamati zake msiingize sumu ya kuchukiana huko kwenye kata, nisisitize madiwani tuendelee kushirikiana katika kusimamia miradi ya maendeleo kwani mnafanya vizuri mnajitoa sana, hivyo tukaitendee haki fedha inayotolewa na Rais wetu Mama Samia Suluhu kwa ajili ya miradi mbalimbali"amesema Mkude.

Amesema kamati ya fedha iliyopita imeonyesha matokeo chanya, hivyo 
ni matumaini yangu kuona viongozi waliochaguliwa wanafanya vizuri zaidi ili kuhakikisha Wilaya ya Kishapu inapata hati safi,hivyo mkasimamie watoto wote wanaofaulu kwenda kidato cha tano na sita wanaenda shule

"Rais ametuonyesha kwamba elimu ni ajenda yake kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu na madarasa yakutosha, tuhakikishe watoto wanaofaulu kwenda kidato cha tano wanapelekwa shule, kuna baadhi ya wazazi hawawapeleki shule watoto hao na kuwapeleka kuchunga ng'ombe na wengine kuwaozesha naomba tusaidizane katika hili tuwalinde ili wasome"amesema Mkude.

Aidha katika uchaguzi wa makamu mwenyekiti alikuwa mgombea mmoja ambaye ni diwani wa kutoka kata ya Mwadui Lohumbo Frances Manyanda alipigiwa kura na kupata kura zote 37 hivyo haikuharibika hata moja, kamati ya fedha na mipango aliyetetea nafasi ya uenyekiti ni Richard Dominick, kamati ya uchumi afya na mazingira alichaguliwa Joel Ndetoson kuwa mwenyekiti na kamati ya maadili alitetea nafasi yake Mohamed Amani.

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya kishapu Sabinus Chaula ambaye ni 
afisa kilimo mifugo na uvuvi wilaya ya Kishapu amesema maagizo yote yaliyotolewa na madiwani na Mkuu wa wilaya viongozi wa CCM wameyapokea na watayafanyia kazi.

"Tumepata Mafanikio eneo la mapato kuna tofauti kubwa ukilinganisha na miaka ya 2022/2023 tulikuwa nyuma kimapato na sasa tumefanya kazi kwa ushirikiano tumevuka lengo kwenye mapato tuna asilimia 104 na mafanikio haya ni kwa sababu tunafanyakazi kwa wakati na kwa muunganiko wa ofisi ya wilaya na ya mkurugenzi hivyo inafanya vizuri na tunasimamia vizuri miradi ya maendeleo"amesema Chaula.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo William Jijimya amewataka madiwani wasiwaachie maafisa utumishi migogoro mbalimbali inayojitokeza kwenye kata, badala yake waende wakashirikiane ili kuhakikisha migogoro inaisha kwa wakati, lakini pia amewapongeza madiwani na watumishi kwa kufanya vizuri kukusanya mapato ya ndani.

"Pia niwaombe wakuu wa idara wote msaidieni mkurugenzi wenu iwe mkuu wa taasisi ama mkuu wa idara, ana mambo mengi ya kufanya, pia tunawapongeza wakuu wa taasisi kwa kuendelea kushauri na kusimamia ukweli, leo tumechagua kamati mbalimbali nendeni mkafanye kazi kwa pamoja ili tuone mabadiliko chanya na madiwani msisite kushauri na kusimamia miradi yetu vizuri,"amesema Jijimya.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Joseph Mkude akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Kishapu Sabinus Chaula akizugumza kwenye kikao cha baraza la madiwani
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Kishapu Sabinus Chaula akizugumza kwenye kikao cha baraza la madiwani
Diwani wa kata ya Mwadui Lohumbo Frances Manyanda ambaye pia alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo
Diwani wa kata ya Talaga Richard Dominick ambaye pia amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya Fedha na mipango
Mohamed Amani ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maadili
Sara Marco diwani wa kata ya Idukilo akizungumza
Duwani viti maalumu Suzana Makoye akizungumza kwenye kikao cha baraza la Madiwani
Mmoja wa madiwani wa halmashauri ya Kishapu akiungumza kwenye kikao hicho
Diwani wa kata ya Talaga Richard Dominick ambaye pia amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya Fedha na mipango
Madiwani wa halmashauri ya Kishapu wakifuatilia makabrasha 
Diwani wa kata ya Seke Bugoro Ferdinand Mpogomi akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani 
Madiwani wa halmashauri ya Kishapu wakiwa kwenye kikao cha baraza la madiwani 
Madiwani wa halmashauri ya Kishapu wakiwa kwenye kikao cha baraza la madiwani 

Watendaji wakiendelea na shughuli za kuandika maadhimio mbalimbali kwenye kikao cha baraza la madiwani
Madiwani na viongozi mbalimbali wakiombea baraza hilo kabla ya kuanza 
Mkuu wa Takukuru wilaya ya Kishapu Mohamed Doo akifafanua jambo kwenye kikao hicho
Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Kishapu Shija Ntelezu akizungumza kwenye kikao hicho
Katibu wa chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Kishapu akizungumza kwenye kikao hicho 
Mkamu mwenyekiti Frances Manyanda baada ya kuchaguliwa kuwa makamu mwenyekiti akiwa amebebwa na diwani wa kata ya Kiloleli Edward Manyama
Mwenyekiti wa kamati ya fedha na mipango Richard Dominick akiwa amebebwa mgongoni na Diwani wa kata ya Kiloleli Edward Manyama
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464