MAZIWA YA MAMA NI KINGA DHIDI YA MAGONJWA MBALIMBALI KWA MTOTO
Na Kareny Masasy,
MTOTO akinyonya vizuri ndipo anapoongezewa kinga ya mwili wake asiweze kushambuliwa na magonjwa mbalimbali hivyo nilazima anyonyeshwe ndani ya saa moja maziwa ya mama baada ya kuzaliwa.
Unyonyeshaji wa maziwa ya mama umewawezesha mamilioni ya watoto wachanga na wadogo kuishi na kuwa na maendeleo mazuri ya ukuaji.
Sakina Juma mkazi wa kijiji cha Bugarama halmashauri ya Msalala anasema elimu ya unyonyeshaji mtoto baada ya kuzaliwa aliipata hospitalini lakini amekuwa akijitahidi kunyonyesha mtoto wake ipasavyo na sasa ana umri wa mwaka mmoja na nusu.
Lucy Garame mkazi wa kijiji cha Bugarama anasema amemuachicha mtoto wake wa mwaka mmoja ili ale na vyakula vingine anakiri elimu ya unyonyeshaji mpaka miaka miwili ameelezwa na wataalamu wa afya kliniki.
“Wataalamu wamejitahidi kutupatia elimu ya unyonyeshaji tunapokwenda kliniki wanasisitiza nakuangalia maendeleo ya mtoto ndiyo maana kila mama anayefanya ujasiriamali utamkuta anaambatana na mtoto wake mgongoni lengo akiamka na njaa apate kunyonya”anasema Garame.
Hassan Majembe na Mola Onesmo wanasema mtoto ni haki yake kunyonya ndiyo maana wataalamu wanawaeleza wanawake wanyonyeshe miezi sita mfululizo bila kumpa kitu kingine.
Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Bugarama halmashauri ya Msalala Dk Kayanda anasema Mahudhurio ya watoto kuletwa kliniki ni mazuri na ndipo wakina mama wanapewa elimu ya unyonyeshaji kwa wakati huo.
“Kwa mwezi watoto 150 hadi 200 wanahudhuria kliniki nab ado wahudumu ngazi ya jamii wamekuwa wakiendelea kuwapa elimu zaidi baada ya kujifungua wakiwa nyumbani”anasema dk Kayanda.
Ofisa lishe halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga Peter Shimba anasema unyonyeshaji wa maziwa ya mama unaupatia nguvu mfumo wa ukuaji na maendeleo ya ufahamu na utambuzi (IQ) wa mtoto.
Shimba anasema kwa kiasi kikubwa husaidia katika kuimarisha mafanikio ya elimu, ushiriki katika nguvu kazi na kuongeza kipato katika maisha ya baadaye ya mtoto.
“Wapo wazazi ambao wamekuwa wakinga’ang’ania kuwekeza kwa mtoto umri ambao ubongo umekwisha komaa hauwezi tena watoto wote wanazaliwa na akili wajitahidi kwenye unyonyeshaji”anasema Shimba.
Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto kutoka hopsitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga dk Mwita Ngutunyi anasema kuwa mila na desturi za kumuachisha mtoto maziwa ya mama pale anapokuwa mama mjamzito kwa madai yataleta madhara inawatesa watoto.
“Wazazi wanaweza kutumia mbinu ya uzazi wa mpango kupangilia ili watoto wao waendelee kuwa na afya nzuri na mzazi arudishe afya yake”anasema Ngutunyi..
Dkt Ngutunyi anasema wazazi wasipotumia uzazi wa mpango mtoto hata ukuaji wake unakuwa sio mzuri na kumrudisha mtoto kukaa kwenye hali yake huwa ni ngumu na gharama ni kubwa hivyo ujauzito unatakiwa upatikane kwa mpango.
“ukosefu wa madini ya vitamin A utamfanya mtoto kuwa na uoni hafifu au kutokuona kabisa na ukosefu wa madini chuma unachangia upungufu wa damu mwilini na madini joto unamfanya mtoto kutokukua vizuri hivyo lazima anyonyeshwe vizuri ”amesema Ngutunyi.
Ofisa lishe mkoa wa Shinyanga Yusuph Hamis anasema asilimia 72 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano wanaupungufu wa damu ikiwa baadhi ya wazazi wamekuwa hawanyonyeshi kwa utaratibu unaotakiwa maziwa ya mama ambayo yana virutubishi vingi.
Hamis anasema mkoa wa Shinyanga una asilimia 83 ya watoto wanaonyonya maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita pekee.
Hamis anasema watoto wenye umri wa miezi 0 hadi 23 ni asilimia 99 walioanzishiwa maziwa ya mama ndani ya saa moja na walioendelea kunyonya baada ya saa moja ni asilimia 3.9.
“Waliondelea kunyonya baada ya mwaka mmoja ni asilimia 78 wazazi wanaelezwa umuhimu wa kunyonyesha watoto baada ya kuazaliwa na baada ya kufikisha umri wa mwaka mmoja ikiwa wataalamu kwenye vituo vya afya wameendelea kutoa elimu”anasema Hamis.
Kwa mujibu wa Taasisi ya chakula na lishe nchini( TFNC ) inaeleza mnamo mwaka 1990 mkutano wa wataalamu wa lishe ulifanyika nchini Italia lengo kujadili mwelekeo wa kisera kuhusu kuendeleza unyonyeshaji Watoto maziwa ya mama.
Mkutano huo uliohisaniwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa ya WHO (Shirika la Afya Duniani) na UNICEF (Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto) Ulifanyika mwaka 1990
Azimio lililopitishwa na nchi wanachama kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kuweza kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo .
Pia azimio hilo limewataka wanawake kunyonyesha baada ya kujifungua na kuendelea kuwanyonyesha watoto wao hadi watimize umri wa miaka miwili au zaidi.
Naibu waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel anasema mama mjamzito anahitaji apate lishe ya mtoto katika siku 1000 Yaani tangu kutungwa kwa mimba hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka miwili kwani ndio msingi bora wa ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili.
“Siku 1000 madhara ya lishe duni hasa udumavu yanaathiri maendeleo ya rasilimali watu ya nchi, hivyo ni muhimu mtoto kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo na kuendelea kunyonyeshwa huku akipatiwa chakula cha nyongeza hadi anapotimiza miaka miwili .” anasema Dkt. Mollel
Dk Mollel anasema watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee umeongezeka kutoka asilimia 58 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 64 mwaka 2022.
Dk Mollel anasema takwimu ya watoto wanaonyonyeshwa ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa imeongezeka kutoka asilimia 53.5 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 70 mwaka 2022.
Mwakilishi wa wadau wa Lishe nchini kutoka shirika la watoto duniani (UNICEF) Patrick Codjia ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa dhamira ya dhati ya kuboresha lishe, afya na maisha ya wananchi wake ikiwa ni pamoja na watoto.
Mwakilishi kutoka Shirika la Kimatifa la
Kazi(ILO) Chiku Semfuko ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kutoa muda kwa
wanawake kwenda kunyonyesha pia kutenga vyumba maalumu vya kunyonyesha ili
kuwapa nafasi wanaonyonyesha
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464