MWENYEKITI UWT TAIFA KUZINDUA MASHINDANO MAALUMU YA DR.SAMIA CUP SHINYANGA MJINI



Mratibu wa madhindano hayo Jackline Isalo akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa UVCCM

Mwenyekiti wa UWT Taifa Mary Chatanda kesho anatarajiwa kuzindua  mashindano 
maalumu ya Dr. Samia Cup ambayo yameandaliwa na vijana wa UVCCM wilaya ya Shinyanga kwa kushirikiana na Taasisi ya bega kwa bega  katika viwanja vya zima moto mjini Shinyanga

Mratibu wa mashindano hayo Jackline Isalo amesema mashindano hayo yanayotarajiwa kuzinduliwa rasimi kesho jumamosi 26,2023 katika viwanja vya zima moto yatafanyika kwa viwango vikubwa na yatakuwa ya mfano, hivyo amewaomba wananchi wa Shinyanga wajitokeze kwa wingi katika maeneo mbalimbali yaliyopangwa.

Jackilin amesema lengo la mashindano hayo ni kukuza vipaji vya vijana na kutengeneza ajira kwa vijana pamoja na kuchochea maendeleo ya mchezo wa soka, ambapo zitakuwepo zawadi mbalimbali kwa washindi, wachezaji bora wa mechi, kipa bora, kocha, mfungaji na timu bora zitapata zawadi na vitakuwepo vifaa vya michezo ikiwemo mipira na jezi vitakabidhiwa kwa viongozi wa timu hizo.

“Lengo la taasisi hii ya Bega kwa Bega na Mama Samia ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia kwa kuhamasisha michezo na sasa tunakwenda kufanya uzinduzi wa mashindano ya mpira wa miguu ambayo yatashirikisha timu 32 yakifanyika kwa muda wa mwezi mmoja na nusu kuanzia Agosti 27,2023 katika viwanja vinane Wilaya ya Shinyanga Mjini",amesema Isaro.

"Baada ya kuona Rais wetu Samia Suluhu anapenda michezo tumeona tianzishe mashindano haya na kuyaita Samia Viwanjani ambapo pia taasisi ya Bega kwa Bega imeshirikiana na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini tunakwenda kufanya mashindano haya ambayo yatakuwa mashindano endelevu kwa kumuunga mkono Rais wetu kwa kupenda michezo.amesema

Isalo amesema mashindano haya yataenda kwa mfumo wa mtoano kwa awamu ya kwanza, wakitoka knock out watakuwa wamebakiza timu 16, watakwenda tena watabakiza timu nane, na kwenda fainali mwisho watatoa zawadi ikiwemo Kombe la washindi.

Aidha amewaomba vijana wote wanaoshiriki mashindano hayo kutambue mpira kwamba ni ajira,na wawe na nidhamu, kwani nidhamu yao ndiyo itakayoweza kuwafikisha mbali na wataibua vipaji ambavyo ambavyo vitashiriki ligi mbalimbali.

“Lengo letu ni kuwaleta pamoja vijana takribani 1600. na pia tutaongea na vijana kuhusu changamoto zilizopo katika jamii, tumeshirikisha makundi ya timu mbalimbali wakiwemo Bodaboda, timu za Masoko, Taasisi ikiwemo SHUWASA, walimu, watumishi, Veterani, kwa hiyo hatujabagua timu ya aina yoyote"amesena.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Jonathan Madete amesema kuwa, mashindano ya Dr. Samia Cup 2023 yameanzishwa na UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini kwa kushirikiana na Taasisi ya Bega kwa Bega na Mama kwa lengo la kuwaweka vijana pamoja lakini pia michezo ni sehemu ambayo inaajiri vijana wengi kwa kasi kubwa hivyo moja ya sehemu walizotupia jicho ni michezo hasa mpira wa miguu.

“Michezo hii imeandaliwa na viongozi wa vijana CCM lakini haiwanyimi fursa vijana kutoka vyama vingine, tunawakaribisha kuja kushiriki. Kupitia mashindano haya tunakwenda kuwapatia vijana fursa ili timu zinazoshiriki ngazi mbalimbali ziweze kuwaona na kuibua vipaji vyao",amesema Madete.

"Niwaombe wapenzi na mashabiki wa soka wajitokeze kwa wingi kuja kushuhudia vipaji kutoka kwa vijana wa Shinyanga pia sisi kama ofisi ya UVCCM tumepania kuhakikisha tunarudisha michezo ndani ya wilaya yetu. Boli limerudi Shinyanga",amesema Madete.

Naye Katibu wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Naibu Katalambula amesema wameshirikiana na taasisi ya Bega kwa Bega na katika kuratibu na kuwezesha mashindano hayo hivyo watahakikisha mashindano hayo yanakuwa endelevu.

“Sisi kwetu CCM kufanyika kwa michezo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020/2025 lakini kama jumuiya ya vijana ni jukumu ambayo ina jukumu la moja kwa moja kwa maendeleo na kuwaweka vijana pamoja tumeamua kuratibu mashindano haya kwa nguvu na wivu mkubwa. Tunawaomba vijana washiriki katika mashindano haya kikamilifu.


Aidha Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa miguu wilaya ya Shinyanga na Mratibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu TFF Mkoa wa Shinyanga Magubika Amani amesema mashindano hayo ni ya wazi hakuna kiingilio na viwanja vitakavyotumika kuwa ni Chuo cha Ualimu Shinyanga (Shycom), CCM Kambarage, Old Shinyanga Jeshini, Shule ya msingi Kitangili, Ibadakuli, Jasco Ngokolo, Shule ya msingi Ndala na Lubaga Joshoni.


“ Katika mashindano haya tutahakikisha sheria zote 17 za mchezo wa mpira zinafuatwa kwa hiyo taratibu zote zimefuatwa na tumetoa kibali kwa umoja wa vijana , Mashindano haya yatakuwa makubwa, naomba wadau wote wa soka wajitokeze kwa wingi"amesema Magubika.


Mratibu wa mashindano hayo Jackiline Isalo akiwa na mwenyekiti wa umoja wa vijana CCM wilaya ya Shinyanga Jonathan Madete
Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa miguu wilaya ya Shinyanga na Mratibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu TFF Mkoa wa Shinyanga Magubika Amani wakiwa kwenye picha ya pamoja na mdau
Wajumbe wakiwa kwenye picha ya pamoja

mratibu wa madhindano hayo Jackline Isalo akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa UVCCM

Mratibu wa Mashindano ya Dr. Samia Cup Shinyanga Mjini, Jackline Isaro akizungumza na waandishi wa habari
Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Shinyanga Jonathan Madete akizungumza
Katibu wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Naibu Katalambula akizungumza
Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa miguu wilaya ya Shinyanga na Mratibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu TFF Mkoa wa Shinyanga Magubika Amani akizungumza

Viongozi na wajumbe wa taasisi ya bega kwa bega
Viongozi na wajumbe wa taasisi ya bega kwa bega


Kazi iendelee

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464