Wazazi wakijitokeza kupeleka watoto wao kupata chanjo ambapo wataalamu wamewafuata wakitumia njia ya Mkoba ( Outreach) na Mobile kliniki kufikia maeneo ya pembezi.
Wazazi wakipeleka watoto wao kupata huduma ya chanjo.
Na Kareny Masasy,
SERIKALI imetumia njia ya chanjo mkoba (Outreach) na chanjo tembezi (Mobile kliniki) kwa lengo la kuwafikia watoto wote waliochini ya miaka mitano kupata chanjo na kuwakinga na maradhi mbalimbali.
Outreach ni pale watoa huduma wanatoka na kwenda kuwafikia walengwa umbali wa kilomita tatu au tano na Moble kliniki imekuwa ikisaidia wazazi ambao hawawezi kufikiwa na huduma hiyo kwa umbali wa kilomita 20 au zaidi.
Dira ya Maendeleo ya taifa ya mwaka 2025 inafikiwa kwa malengo yake ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano hapa nchini.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Igalula kata ya Ukune halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga Helena Cosmas na Lucy Benjamini wanasema wataalamu wa afya wamekuwa wakifika kijijini hapo nakutoa huduma ya chanjo kwa watoto.
Cosmas anasema wamefurahia kupata huduma ya chanjo kwa watoto kwa ukarbu kwani walikuwa wanashindwa kwenda umbali wa kilomita 15 kufuata huduma ya kliniki na chanjo kwa watoto.
“Kutokana na umbali tukishamaliza kujifungua haturudi tena labda mtoto augue lakini akiwa mzima hatuendi sababu ya umbali mrefu kituo cha afya kipo kijiji cha Iboja umbali wa kilomita 15 na kwenda kijiji cha chona umbali wa kilomita 8 “anasema Cosmas.
Benjamini anasema kijiji hakina Zahanati utolewaji wa huduma za kliniki na chanjo kwa watoto hutangaziwa kwenye mkutano wa hadhara kuwa wataalamu watakuwepo na wao hujitokeza.
“Wataalamu wametusaidia kutotembea umbali mrefu kwani wao wamekuwa wakituletea huduma ya kliniki na kuwapa chanjo watoto wetu kwa hilo tunaipongeza serikali”anasema Benjamini.
Mtendaji wa kijiji cha Igalula Alex Kabakina anasema kijiji kina wakazi 8000 ambapo wazazi hutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya na kliniki kwa watoto ikiwa wataalamu wamekuwa wakija kutoa chanjo.
“ Lakini zipo jitihada zilizofanyika za ujenzi wa Zahanti ambao ulianza mwaka 2016 kwa nguvu za wananchi kuchangia na halmashauri mapato ya ndani ikatoa sh Millioni 14 na serikali kuu ilitoa sh Millioni 50 mpaka kukamilisha.”anasema Kabakina.
Diwani wa kata ya Ukune Mkomba Paul anasema kata yake ina wakazi zaidi 1500 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi na vijiji nane ambavyo ni Iboja,kundikili, Igalula,Chibisa,Sofi Ilwilo,Italike na Kayenze lakini kijiji kimoja ndiyo kina kituo cha afya pekee.
“Tumeanzisha ujenzi wa Zahanati hii baada ya kuona wajawazito wanateseka kutembea umbali wa kilomita 15 kwenda kituo cha afya Ukune kilichopo kijiji cha Iboja na wakati mwingine kwenda Zahanati iliyopo kata ya Mapamba ni mwendo wa kilomita 10 au Chona kilomita nane ”anasema Paul.
Diwani Paul anasema kukosekana kwa Zahanati katika vijiji vya kwenye kata yake wataalamu wa afya wamekuwa wakijitahidi kuwafikia wananchi walipo na kuwapa huduma ya kliniki watoto na chanjo.
Mbunge wa jimbo la Ushetu Emanuel Cherehani anasema yalikuwepo maboma ya Zahanati 23 yaliyoanzishwa mwaka 2016 lakini kipindi cha miaka miwili maboma 14 ya Zahanati yamekamilika na Zahanati 11 zinawatumishi zimeanza kutoa huduma.
“Sera ya afya ya mwaka 2007 inaeleza kila kata kuwe na kituo cha afya na kila kijiji kuwe na Zahanti na serikali inafanya jitihada za kuhakikisha sera hiyo inatekelezwa ipasavyo na wananchi wasitembee umbali mrefu kufuata huduma”anasema Cherehani.
Mratibu wa huduma za afya Musa Baraza anasema kuna hospitali moja, vituo vya afya vitatu na Zahanati 31 na vituo hivyo vina huduma za palepale na huduma za kuwafikia walengwa waliopo mbali.
Baraza anasema halmashauri ina jumla ya huduma za mikoba (Outreach) kila Mwezi huduma ya chanjo zinafanywa 81 na Mobile kliniki nne na robo ya mwaka huu huduma zilizofanywa za Outreach 243 na Mobile kliniki 12.
“Katika robo ya pili mwezi June wamefanya Outreach 238 na Mobile kliniki 12 na Malengo wamefikia asilimia 99 kwa watoto waliowafikia mfano chanjo ya kuzuia kuhara Rotavaccine mwezi April walitoa Dozi ya kwanza ya Rota nakufikiwa watoto 816, Mei watoto 829 na Juni watoto 775”anasema Baraza.
Baraza anasema wahuduma ngazi ya jamii (WAJA) wako 554 ambao wamekuwa wakihamasisha jamii na kila kitongoji wapo na lengo lililopo kuwafikia watoto na wajawazito.
Mratibu wa chanjo wa halmashauri ya Ushetu Saulo Mkama anasema wamekuwa wakitoa huduma za chanjo Outreach imekuwa ikiwasaidia wananchi kutotembea umbali mrefu.
“Outreach ni pale watoa huduma wanatoka na kwenda kuwafikia walengwa umbali wa kilomita tatu au tano na Moble kliniki imekuwa ikisaidia wazazi ambao hawawezi kufikiwa na huduma hiyo kwa umbali wa kilomita 20 au zaidi”.
Mganga mkuu wa halmashauri Ushetu dk Athumani Matindo anasema kuna vijiji 112 kati ya hivyo vijiji 35 ndiyo vimefikiwa na huduma ya kutolea afya na vijiji vingine havina lakini wataalamu wamekuwa wakienda kutoa elimu ya afya, kliniki na chanjo.
“Tumekuwa tukishirikiana na viongozi wa kijiji kupata maeneo ya kutolea huduma wakati wataalamu wakifika ikiwa huduma wanazo zikosa ni zile na mama na mtoto lazima waende kwenye kituo cha afya kwenye vifaa”anasema dk Matindo..
Mratibu wa chanjo mkoa Timothy Sosoma anasema Outreach imesaidia kuwafikia watoto wengi walio na umri chini ya miaka mitano kupata chanzo za aina zote zinazohitajika hadi kufikia mwezi June mwaka huu watoto 39512 wameapata chanjo ya Rota sawa na asilimia 109.
Kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga dk Nuru Mpuya anasema kuna vituo 307 vya kutolea huduma za afya na watoto wamekuwa wakipata chanjo za aina zote pale wanapohitajika wengine kupitia Outreach na Mobile Kliniki.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu anasema huduma ya Outreach na Mobile imechangia kupunguza vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa kufikiwa na huduma ya chanjo maeneo walipo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464